Unilever Yadhamini Mbio Za Watoto Rock City Marathon. | Tarimo Blog

Kampuni ya Unilever Tanzania imekabidhi hundi yenye thamani Tsh milioni 20 kwa waandaaji wa mbio za Rock City Marathon ikiwa ni udhamini wa kampuni hiyo katika mbio za km 2.5 mahususi kwa ajili ya watoto. Mbio hizo  zinatarajiwa kufanyika Oktoba 24 mwaka huu, kwenye viunga vya Rock City Mall jijini Mwanza.

Hatua hiyo inatajwa kuwa ni muendelezo wa mkakati wa kampuni hiyo katika kushirikiana na jamii na serikali kwa ujumla katika kuhamasisha michezo nchini ili kuibua vipaji, kujenga afya pamoja na kukuza sekta ya michezo nchini.

Wakizungumza kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya hundi yenye thamani ya sh mil 20 kutoka kampuni ya Unilevel Tanzania kwenda kwa waandaaji wa mbio hizo kampuni ya Capital plus international (CPI), Mkurugenzi Mtendaji  wa Unilever Tanzania Bw David Minja pamoja na Mratibu wa mbio hizo kutoka CPI Bw Kasara Naftal walisema ushirikiano huo mpya ni ishara nzuri kwa mustakabari wa mchezo huo sambamba na ukuaji wa sekta ya utalii Kanda ya Ziwa.

“Tumeamua kudhamini tukio hili kwa sababu linawaleta pamoja watu kutoka nyanja mbalimbali katika maisha wakiwemo watoto ambao ni miongoni mwa wadau wetu wakubwa.,’’ alisema Bw Minja, huku akibainisha kuwa mbio hizo za km 2.5 kwa ajili ya watoto zitafahamika kama ‘Unilever Rock City Junior Challenge.’

Alisema ‘Unilever Rock City Junior Challenge’ inalenga kutoa fursa kwa watoto ambao ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo ikiwemo sabuni ya OMO, sabuni ya Sunlight na mafuta ya kujipaka ya Vaseline ambao wataibuka washindi kwenye mbio hizo kuweza kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo vifurushi maalum vyenye bidhaa hizo.

“Kwa kuwa bidhaa zetu zinahusisha zaidi matumizi ya kifamilia nitoe wito kwa wazazi na wanafamilia kwa ujumla wajitokeze kwa wingi huku wakihamasisha watoto pia washiriki kwenye mbio hizi ili kuongeza ushindani. Unilever tunawahakikishia kwamba zawadi kwa watoto zitakuwa ni nyingi na za kutosha,’’ alisema.

Kwa upande wake Bw Naftal pamoja na kuishukuru kampuni ya Unilever kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na kampuni hiyo katika kuboresha mbio hizo, alisema kufuatia uwepo wa kampuni ya Unilever kwenye mbio hizo mwaka huu, inatarajiwa kwamba ‘Unilever Rock City Junior Challenge’ itakuwa ni moja ya kivutio kikubwa miongoni mwa matukio yanayotarajiwa kupamba mbio hizi.

Akifafanua zaidi kuhusu ‘Unilever Rock City Junior Challenge’ Bw Naftal alisema pia itahusisha utafutaji wa vipaji vya riadha kutoka kwenye baadhi ya shule za msingi jijini Mwanza kwa wanafunzi wenye umri wa miaka 5 hadi 10 ambapo washindi pamoja na kujipatia zawadi mbalimbali kutoka Unilever pia watapata tiketi zitakazowawezesha  kuchuana kwenye kilele cha mbio hizo.

“Tangu kuanzishwa kwa mbio hizi huu ukiwa ni msimu wa 12 sasa tumekuwa tukihusisha ushiriki wa watoto kwa namna mbalimbali. Ila mwaka huu tunaamini mbio za watoto zinakwenda kutikisa vichwa vya habari. Kupitia ushindani tunaoutarajia kwenye mbio hizi sasa tunaamini kwamba lengo letu la kuibua vipaji vipya vya riadha linakwenda kutimia…asanteni sana Unilever kwa kuwekeza kwa watoto’’ alishukuru.

Alisema maandalizi ya mbio hizo zinazotarajiwa kuhusisha washiriki zaidi ya 3000 wakiwemo wakimbiaji wa kimataifa, wakimbiaji kutoka mashirika mbalimbali, wanafunzi sambamba na watu wenye ualbino yanaendelea huku akitoa wito kwa washiriki kuendelea kujisajili kupitia njia ya simu na tovuti

Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon Bw Kasara Naftal (Kushoto) akipokea mfano wa hundi yenye thamani Tsh milioni 20 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji  wa kampuni ya Unilever Tanzania Bw David Minja (Kulia) ikiwa ni udhamini wa kampuni hiyo kwenye mbio za km 2.5 mahususi kwa ajili ya watoto ambazo ni sehemu ya mbio za Rock City Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 24 mwaka huu, kwenye viunga vya Rock City Mall jijini Mwanza. Katikati ni Meneja Masoko wa Kampuni ya Unilever Tanzania Bi Lilian Kibbassa.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Unilever Tanzania Bw David Minja (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa hafla hiyo. Kushoto ni Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon Bw Kasara Naftal pamoja na Meneja Masoko wa Kampuni ya Unilever Tanzania Bi Lilian Kibbassa (Kulia)

 

Meneja Masoko wa Kampuni ya Unilever Tanzania Bi Lilian Kibbassa (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa hafla hiyo. Kushoto ni Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon Bw Kasara Naftal pamoja na Mkurugenzi Mtendaji  wa kampuni ya Unilever Tanzania Bw David Minja (Kulia)

Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon Bw Kasara Naftal (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa hafla hiyo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji  wa kampuni ya Unilever Tanzania Bw David Minja pamoja na Meneja Masoko wa Kampuni ya Unilever Tanzania Bi Lilian Kibbassa (Kulia)

 

 



 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2