UPANDE WA UTETEZI KESI YA MBOWE NA WENZAKE WAOMBA IPELEKWE MAHAKAMA KUU | Tarimo Blog

Wakali Peter Kibatala akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Agosti13, 2021, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati wa kesi ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu.

UPANDE wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu wamewasilisha taarifa ya kusudio la kuiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ipeleke mahakama Kuu matamshi yaliyotolewa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kama suala la kikatiba.

Wakali wa utetezi, Peter Kibatala amedai kuwa wamefikia hatua ya kuleta maombi hayo kwa sababu matamshi hayo kwa maoni yao ni kuwa yanaingilia moja kwa moja uhuru wa mahakama, ambapo siyo mahakama ya Kisutu tu bali hata mahakama itakayoenda kusikiliza shauri hilo la ugaidi linalomkabili Mbowe na wenzake.

Amedai, kwa kuwa Taasisi hiyo ni yenye nguvu na inaushawishi basi matamshi yake kwa namna yalivyotamkwa yamewafanya wateja wao waone kama wameishahukumiwa na kwamba hakuna namna yoyote wanaweza wakapata haki yao.

"Tumeomba suala hilo la iwapo au la matamshi ya Taasisi hiyo yameingilia uhuru wa mahakama na iwapo au la matamshi hayo yamesababisha kesi isiwe na mantiki tena kiasi kwamba hakuna namna ya kufanya isipokuwa kuifuta......hivyo tumeiomba mahakama hii kwa kuwa haina uwezo wa kusililiza suala la kikatiba na haina uwezo wa kuitolea uamuzi kikatiba basi tunaomba mahakama hii itusikilize na ikiridhika basi itupeleke kwenye mahakama yenye mamlaka ambayo ni Mahakama kuu ili iangalie je matamshi hayo yameingilia uhuru wa mahakama na je ni kweli matamshi hayo kama tunavyosema sisi yameleta miss trial kwamba hakuna kesi kwenye macho ya kawaida, amedai Kibatala.

Wakijibu hoja hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi Pius Hillar umekiri kupokea kusudio hilo na wameiomba mahakama iwapatie muda kwa ajili ya kuwasilisha majibu yao.

"Mheshimiwa Hakimu, kweli tumepokea kusudio hilo kwa njia ya maandishi, tunaomba muda na sisi tutajibu kwa njia ya maandishi." Amesema Hilla

Hata hivyo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 27, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa kusudio hilo na pia ameamuru siku hiyo washtakiwa waletwa mahakamaninm kutokana na mtandao kusumbua sumbua mara kwa mara.

Mapema wakati kesi hiyo inaendelea kwa njia ya mtandao mshtakiwa Mbowe alikuwa akilalamika mara kwa mara juu ya kukatika kwa mtandao na hivyo kushindwa kufuatilia taratibu za kesi vizuri.

Mbali na Mbowe washtakiwa wengine ni Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya.

Washtakiwa wote wanakabiliwa na shtaka la kula njama ya kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko ya Umma. Huku Mbowe peke yake akikabiliwa na shtaka la kufadhili vitendo vya kigaidi, na washtakiwa Hassan, Kasekwa Lingwenya wakidaiwa kupokea pesa kutoka kwa Mbowe kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi.

Pia mshtakiwa Kasweka anadaiwa kukutwa na silaha aina pisto na risasi tatu huku mshtakiwa Hassan akikutwa akitumia sare na vifaa vya jeshi.

Viongozi mbalimbali wa vyama vya Upinzani wakiwa nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo  Agosti 13,2021 jijini Dar es Salaaam.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2