WIZARA YA AFYA YARIDHISHWA MWITIKIO WA WANANCHI KUPATA CHANJO, YAANZA KUTOA VYETI KIELETRONIKI KUDHIBITI UDANGANYIFU | Tarimo Blog

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Profesa Abel Makubi amesema kuwa Wizara hiyo imeridhishwa na  muitikio wa wananchi kujitokeza kupata chanjo ya Covid-19 huku akiweka wazi utaratibu wa Wizara hiyo kuanza  utoaji wa vyeti vya Kielektroniki kwa wananchi ambao wamepata chanjo hiyo

Pia Profesa Makubi amesema Wizara haitamjibu mtu yeyote anayeendelea kupotosha umma kuhusu chanjo hiyo wao wataendelea kutoa elimu kwa umma kupitia wataalamu wao wa Afya ili kuwahamasisha wananchi kupata chanjo hiyo ambayo haina madhara na zaidi imelenga kuwakinga dhidi ya ugonjwa huo.

Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kushuhudia utoaji chanjo kwa waandishi wa Habari, Wasanii, wanamichezo na baadhi ya wananchi katika viwanja vya Karimjee huku ikishuhudiwa idadi kubwa ya watu ikijitokeza kupata chanjo hiyo.

"Tangu kuzinduliwa rasmi kwa utaratibu huo, makundi mbalimbali ya wananchi  yameendelea kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote yaliyotengwa maalumu kwa ajili utoaji wa chanjo hii suala ambalo kimsingi  linafanyika kwa weledi mkubwa" amesema Profesa Makubi

Aidha amesema kuanza kutolewa kwa vyeti vya Kielektroniki ni sehemu ya mkakati wa Serikali kudhibiti watu wenye nia ovu ambao tayari wameanza kughushi vyeti kwa lengo la kuuaminisha umma kuwa wamepata chanjo jambo ambalo si sahihi na kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua.

"Kwa wale ambao walishapata chanjo na hawajapata vyeti vya Kielektroniki, Wizara itawataarifu kwa kuwapigia simu au kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) ili nao waweze kupatia vyeti hivyo mbadala wa walivyopewa awali" amesema Profesa Makubi

Amefafanua kuwa kwa vyeti hivyo vilivyopo katika mfumo wa Tehama, kimsingi vimeandaliwa katika mfumo ambao ni ngumu kwa mtu yeyote kuvighushi kwa kuwa vimewekwa mfumo wa utambuzi ambao unamtambulisha mtu.

Amesisitiza kwa wale waliokuwa na wasiwasi huenda wakakataliwa kutokana na umri wao kutokuwepo katika kundi lenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea kwa sasa  wanaruhusiwa kwenda kupata chanjo hiyo kwa kuwa tayari Serikali imepata uhakika wa kupatikana kwa chanjo zaidi hivi karibuni

Akizungumzia mwenendo mzima wa utoaji wa chanjo hiyo, Profesa Makubi amesema wanaendelea kukusanya takwimu za idadi ya watu wote walipata chanjo hiyo na kwamba watakuwa wanatoa taarifa kwa umma kila Jumapili  huku akieleza iwapo kutakuwepo na mtu makubwa au madogo baada ya kupata chanjo watatoa taarifa.

Wakati huo huo  Kaimu Mkurugenzi waTehama katika Wizara hiyo Sylvanus Ilomo alisema katika kufanikisha mfumobwa utoaji vyeti Kielektroniki Wizara imetoa mafunzo maalumu kwa maafisa wake wote waliopo nchi nzima ambao wanatoa huduma ya chanjo.

"Kwa hiyo sasa wakichanjwa taarifa zao zitakuwa zinakusanywa na kuwekwa katika mfumo wa Kielektroniki hivyo nami nasisitiza kama ulivyosema Katibu Mkuu kuwa tusijaribu kughushi vyeti hivyo kwa kuwa taarifa zote tunazo na watakaokwenda kinyume tutawabaini" amesema Ilomo

Amengeza endapo mtu atajaribu kughushi anapaswa kutambua cheti hicho hakitatambulikiwa na Wizara itamtambua na kumchukulia hatua inayostahili kwa kosa alilolifanya.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wazee na Watoto  Profesa Abel Makubi( katikati) akizungumza leo Agosti 12 ,2021 jijini Dar es Salaam wakati akielezea mchakato wa utoaji chanjo unaondelea nchii

Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Profesa Abel Makubi (katikati) akitoa maelezo kuhusu vyeti vya kieletroki ambavyo vinatolew na Wizara kwa wanaopata chanjo.Hivyo baada ya taarifa za mhusika kuingizwa kwenye mtandao anapewa karatasi yenye Barcord ambayo itatumika kumtambulisha aliyepata chanjo hiyo

Mkurugenzi na Mmiliki wa Blog ya Fullushangwe  John Bukuku akipata chanjo leo katika Ukumbi wa kariamjee jijini Dar es Salaam.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2