*Waliopo JKT kupewa fursa kuanzia Septemba 20 hadi 30
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeongeza muda wa uombaji mikopo kwa siku 15 zaidi kuanzia Septemba 1 hadi 15 mwaka huu ili kuwapa fursa kwa waombaji mikopo ambao wamejisajili katika mfumo kukamilisha maombi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema kuwa uamuzi huo umetokana na maombi na ushauri walioupokea kutoka kwa wadau.
“Tulianza kupokea maombi kwa njia ya mtandao Julai 9, mwaka huu na hadi jana ambayo ilikua siku ya mwisho ya kuomba tulikua na waombaji 91,445 waliowasilisha maombi, na kati ya hayo, maombi 12,252 yalikua hayajakamilika na wateja wetu wameomba muda wa kukamilisha.” amesema Badru.
Kwa mujibu wa Badru, amesema hatua inayofuata ni uhakiki wa nyaraka na taarifa zilizowasilishwa na waombaji 79,193 ambao maombi yao yamekamilika kama yanavyoonekana kwenye mfumo.
“Kuna makundi mawili, wale 12,252 ambao maombi hayana viambatisho na hivyo hayajakamilika na kwa siku zilizotolewa waombaji watembelee akaunti zao maarufu kama SPA kurekebisha taarifa zao… na kuna maombi 79,193 yenye nyaraka, sasa tunaanza kuhakiki usahihi wake na baadae tutaangalia kama wamepata udahili na wale wenye sifa ndiyo watapangiwa mkopo.” amesema Badru.
Kuhusu wanafunzi wahitaji wanaoendelea na mafunzo katika Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Badru amesema vijana hao waliopo katika kambi 19 nchini watapata fursa maalum ya kuomba mkopo kwa siku 10 kuanzia Septemba 20 hadi 30 mwaka huu.
“Tumekuwa tukiwasiliana na Makao Makuu ya JKT, na tumekwenda na kukutana na vijana hao katika kambi zote na tuliwaahidi kuwa watapata fursa … ambayo ni kuanzia Septemba 20 hadi 30 mwaka huu, hivyo wasiwe na wasiwasi,” amesema Badru.
Akibainisha mapungufu yaliyojitokeza kwa taarifa za waombaji na kutakiwa kuyafanyia marekebisho Mkurugenzi wa Uchambuzi na Utoaji Mikopo Dkt. Veronica Nyahende amesema mapungufu hayo ni pamoja na fomu kutosainiwa na muombaji au mdhamini wake, kukosekana kwa picha ya mwombaji au mdhamini, fomu kutokuwa na kitambulisho cha mdhamini, fomu kutohakikiwa na watendaji wa vijiji, kutohakikiwa kwa vyeti vya kuzaliwa na vifo na kuwekwa katika mpangilio uliowekwa pamoja na taarifa kutohakikiwa na kupigwa mhuri wa mwanasheria
Wakizungumza katika Mkutano huo, Mwakilishi wa Kaimu PostaMasta Mkuu, Mbarouk Issa amesema hadi TPC itaendelea kuhudumia wanafunzi waombaji mikopo wanaoendelea kutuma fomu za maombi katika Ofisi zozote za TPC zilizopo katika Mikoa na Wilaya zote nchini.
Kwa mujibu wa Mbarouk, hadi kufikia jana, Agosti 31, 2021 TPC ilikua imepokea fomu za wanafunzi 56,140 na nyingine 2,200 zikiwa njiani kufikishwa HESLB na kuwa TPC imejipanga kuendelea kuwahudumia wateja hao katika muda wote ulioongezwa.
Naye Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa RITA, Beatrice Mboya amesema kupitia mfumo wa E-Huduma, RITA, imepata mafanikio makubwa na itaendelea kuhakiki vyeti vya kuzaliwa vya wanafunzi waombaji mikopo hadi dirisha hilo litakapofungwa ili kuweza kuwasaidia wateja kuweza kukamilisha na kuwasilisha maombi yao kwa usahihi.
“RITA ni wadau wakubwa wa masuala ya mikopo ya wanafunzi, kupitia mifumo yetu ya ndani tumepata mafanikio makubwa kwa kuhakiki maombi ya uhakiki wa vyeti vya wanafunzi, ambapo kati ya maombi 111,751 tumeweza kuhakiki vyeti vya kuzaliwa 111,358” amesema Mboya.
Katika mwaka wa masomo 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha TZS 570 Bilioni kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi 160,000 wa taasisi za elimu ya juu. Kati ya hao, wanafunzi 62,000 wanatarajiwa kuwa ni wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 98,000 wanaoendelea na masomo. Bajeti kwa mwaka 2020/2021 ilikua TZS 464 bilioni na zimewanufaisha jumla ya wanafunzi 149,398.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment