Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika Kata Sita za Tanzania Bara utakaofanyika tarehe 9 Oktoba mwaka 2021.
Akitangaza Uchaguzi huo mdogo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles amesema uchaguzi huo unafanyika kutokana na madiwani wa kata hizo kufariki na mmoja kukosa sifa ya Uraia.
Amefafanua kuwa uchaguzi huo umekuja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupokea taarifa kutoka kwa Waziri Mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, akiitaarifu Tume kuwepo kwa nafasi wazi katika kata husika.
Dkt. Mahera amezitaja kata hizo kuwa ni Kata ya Kagera Nkanda iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoa wa Kigoma, Kata ya Kileo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro, Kata ya Neruma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoa wa Mara, Kata ya Luduga iliyopo Halmshauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoa wa Njombe, Kata ya Lyowa iliyopo Halmashauri ya Wilala ya Kalambo mkoa wa Rukwa na Kata ya Vumilia iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Urambo mkoa wa Tabora.
Amesema ratiba ya uchaguzi huo itaanza na utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea kuanzia Septemba 13 hadi 19, 2021 huku uteuzi wa wagombea watakao wania nafasi hizo ukifanyika Septemba 19 mwaka 2021.
Ameongeza kuwa kampeni za Uchaguzi huo zitaanza tarehe 20 Septemba hadi tarehe 8 Oktoba, 2021 na siku ya kupiga kura itakuwa tarehe 9 Oktoba mwaka 2021.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment