Nipe Fagio, taasisi isiyoya kiserikali inayohusisha jamii, sekta binafsi, na serikali katika kufikia maendeleo endelevu kwenye sekta ya udhibiti wa taka, leo imeyatangaza rasmi maeneo ya usafi kuelekea Siku Ya Usafi Duniani kwa mwaka huu 2021, ambayo itasherehekewa ndani ya siku mbili nchini Tanzania, ikiwa ni tarehe 11 na 18 Septemba.
Kwa mwaka huu, Siku Ya Usafi Duniani imepangwa kufanyika katika maeneo 20 katika jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine 20 kwenye mikoa tofauti nchini.
“Tunaandaa usafi utakaofanyika kwenye maeneo 40 nchi nzima, kwa kushirikiana na taasisi ambazo tumekuwa tukishirikiana nazo kwa muda mrefu sasa. Uchambuzi wa Taka na Chapa (Waste and Brand Audits – WABA) unaendelea kuwa ni kupaumbele chetu na uchambuzi huo utafanyika katika maeneo yote ya Usafi,” alisema Ana Rocha, Mkurugenzi Mtendaji wa Nipe Fagio. “Malengo ya kuandaa usafi huu kwenye maeneo haya ni kuwawezesha watu kuwa na ufahamu wa uchafuzi wa taka unaofanyika nchi nzima na kukusanya takwimu na kuchochea tatuzi zifanyike, kama Uwajibikaji kwa Mzalishaji, ambazo zitatatua changamoto hii”.
Ana aliongeza kuwa kutokana na uwepo wa janga la UVIKO-19, ililazimika maeneo haya ya Usafi kugawanywa katika tarehe mbili (Septemba 11 na 18) ikiwa katika lengo la kugawanya maudhurio na kupunguza idadi ya katika eneo moja la usafi.
“Tumeamua kugawanya usafi katika siku mbili kwa kuwa hili litasaidia kupunguza idadi ya washiriki kwa kila eneo. Tahadhari zote zitachukuliwa kukiwa na vituo vya kuoshea mikono,” alisema. Na kuongeza: “Tunasisitiza sana kwa mtu yoyote atakayeshiriki usafi huu kuja akiwa amevaa barako”.
Usafi huu utafanyika katika maeneo ya Bariadi-Simiyu, Iringa, Korogwe-Tanga, Mafia Island, Mbeya, Moshi, Mwanza, Njombe, Rukwa, Shinyanga, Zanzibar, Bukoba, Kipili (Ziwa Tanganyika) na jijini Dar es Salaam.
Ikiwa kama taasisi muongozaji wa Siku Ya Usafi Duniani nchini Tanzania, Nipe Fagio inategemea kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwenye makundi mbali mbali ya jamii, watu wanaojitolea, na wadau wengine katika sekta ya mazingira katika kuifanya hii Siku Ya Usafi Duniani kuwa ya kipekee na yenye mafanikio zaidi.
“Tunahitaji kufanya kazi pamoja tukiwa na lengo moja la kushinda uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki na kuifanya Tanzania kuwa nchi safi na yenye afya nzuri kupitia kukuza uelewa, ukusanyaji takwimu na kuchochea mabadiriko chanya,” Ana aliongeza.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment