Matukio ya Mauaji yaliyotikisa katika mkoa wa Manyara mwaka 2021. | Tarimo Blog




Na John Walter-Manyara

Tukiwa tupo ukingoni mwa mwaka 2021,yapo matukio mengi ya Ukatili yaliyoripotiwa na jeshi la Polisi mkoani Manyara ambayo yaliwashtua watu wengi, mengine yakihusishwa na wivu wa Mapenzi.

WILAYA YA SIMANJIRO.

Matukio hayo ni pamoja na lile la Daktari wa mifugo wa kijiji cha Loiborsoit A wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, Malipe Ole Kisota kuuawa kwa kukatwa mapanga na watu waliomtuhumu kumpa ujauzito mke wa ndugu yao.
Imeelezwa kuwa alikatwa na sime sehemu mbalimbali mwilini mwake na ndugu watatu, Lazaro, Mamei na Supek Mamei, wakimtuhumu kumpa ujauzito mke wa ndugu yao Kinaruu Mamei.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Marrison Mwakyoma akizungumza Novemba 13,2021 alieleza kuwa mauaji hayo yalitokea Novemba 11,2021.
Kamanda Mwakyoma alisema chanzo cha kifo hicho ni wivu wa mapenzi, akidai marehemu alikuwa akituhumiwa kutembea na mke wa mtu na alikuwa anatafutwa akawa anajificha na siku ya tukio walimkibiza, kumkamata na kufanya mauaji hayo.

WILAYA YA MBULU

Tukio lingine ambalo liliripotiwa mwaka huu ni lile lililotokea kijiji cha Silaloda Mbulu ambapo Jeshi la Polisi mkoani Manyara lilimkamata mkazi wa Mtaa wa Silaloda Mji wa Mbulu, Harold Hhando, kwa tuhuma za kumuua mtoto wa kaka yake, Emmanuela Hando (13), kisha kumtoa viungo vya mwili.

Ilidaiwa kuwa Hhando alimuua mtoto huyo wa kaka yake kwa kumpasua katikati ya miguuu na kumtenganisha vipande viwili kisha kukata sehemu za siri, kumtoa maini na kutaka kuyapika, ili ayale.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi, Marrison Mwakyoma, alisema chanzo cha tukio hilo ni ushirikina, kwani Hhando ameeleza kuwa aliambiwa na Mungu wake amuue mtoto wa kaka yake na kula maini, ili avune mazao mengi.

Baadhi ya wananchi wa eneo hilo, akiwamo, John Baynet alisema wananchi wa eneo hilo wamesikitishwa na kitendo hicho cha Hhando kumuua binti huyo mdogo ambaye ni mtoto wa kaka yake.

Katika wilaya hiyo ya Mbulu, Mkazi wa Kijiji cha Garanja, Kata ya Tlawi, Wilayani Mbulu, Mkoani Manyara, Maria Suruhu (56) alishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua kwa kumpiga kichwani na shoka mume wake Lego Kerehemi (54).
Kamanda Mwakyoma amesema chanzo cha kifo ni ugomvi wa ndani baada ya mwanamke huyo kuulizwa alipochelewa baada ya wote kutoka kunywa pombe kilabuni.

Amesema mume na mke walienda kilabuni kunywa pombe na walipomaliza waliamua kurudi nyumbani huku wakiongozana wawili barabara.

WILAYA YA BABATI.

Kijana aliyejulikana kwa jina la Michael Jackson mkazi wa Kijiji cha Magara wilayani Babati mkoani Manyara aliuawa kwa kukatwa katwa mapanga baada ya kumfumania akifanya mapenzi) kwenye banda la ng’ombe na mke wa Samwel Alfred aitwaye Habiba Saidi .

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP), Marrison Mwakyoma tukio hilo limetokea majira ya saa 10 alfajiri ya Septemba 8,2021.

Pia Mkazi wa Kijiji cha Mutuka Wilayani Babati Mkoani Manyara, Samson Daudi (26) alishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua Peter Buu (48) akimhusisha na imani za kishirikina.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, Grafton Mushi alisema Septemba 7, 2021 kuwa tukio hilo limetokea kwenye kijiji hicho baada ya Daudi kumtuhumu Buu anamloga ili nyumba yake isimalizike kujengwa.

Mushi amesema mtuhumiwa alimuua Buu kwa kumkata mara tatu shingoni kwa kutumia panga na kisha akafariki dunia papo hapo.

Alisema kabla ya tukio hilo marehemu alifika shambani mwa mtuhumiwa aliyekuwa akimtuhumu kukwamisha ujenzi wa nyumba yake kwa kumroga na ndipo ugomvi uliibuka na Daudi akaanza kumwambia kuwa anamuroga ili asimalize nyumba yake ndipo akaanza kumshambulia kwa mapanga.

Tukio lingine lililowastua watu ni lile la Mkazi wa mtaa wa Kiongozi Mjini Babati , Lucas Mangu (46) kumuua mke wake Anna Kisino (41) kwa kumpiga kutokana na wivu wa kimapenzi kisa na yeye kufariki dunia kwa kujinyonga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Marrison Mwakyoma akizungumzia tukio hilo Agosti 22, 2021 usiku.

Kamanda Mwakyoma alisema Mangu alimuua mkewe kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili hadi kumuua baada ya kumfungia ndani kutokana na wivu wa kimapenzi.

Amesema Mangu alikuwa amesafiri kwenda Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro kwa ajili ya shughuli za kilimo na alirudi Babati siku hiyo na kufanya mauaji hayo ya mkewe na kujiua.

Amesema watu walijaribu kumwambia aache kumpiga mkewe baada ya kusikia yowe ila kwa kuwa alifunga mlango akimpiga aliwaambia wamuache ampige kwani ni mkewe.

Tukio lingine katika wilaya ya Babati ni lile la mkazi wa kijiji cha Ngolei, Emmanuel Richard kumuua mama mkwe wake Maria Batholomeo (61) kwa kumpiga kifuani baada ya kuingilia ugomvi na mkewe.

Jeshi la Polisi mkoani Manyara lilithibitisha kutokea kwa tukio hilo Juni 21 mwaka huu na kueleza kuwa walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.

WILAYA YA HANANG

Mkazi wa Kijiji cha Bassotu Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara, Elibariki Shaban (50) alishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mtoto wake kwa kumpiga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna msaidizi Maresone Mwakyoma alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 26 mwaka huu kwenye kijiji cha Bassotu.

Kamanda Mwakyoma alisema Shaban anadaiwa kumpiga mtoto wake, Amos Elibariki (25) kwa deki usoni, makofi na mateke na kufariki dunia wakati akipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Haydom.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni baba kumpiga mtoto wake baada ya kubishana kwenye mambo yao ya kifamilia na mzee huyo kuchukia.

Alisema Shaban alipohojiwa na polisi sababu za kumpiga mwanaye alisema alimpiga kwa kuwa mtoto huyo alimtukana na yeye hasira ilimpanda na kuamua kumuadhibu.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2