Dotto Mwaibale na Godwin Myovela, Singida.
RAIS Samia Suluhu Hassan amekabidhi Shilingi Bilioni 12.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kupunguza kero ya maji kwa kiwango cha juu katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa kwa wananchi wa mkoa wa Singida.
Hafla ya utiaji saini mikataba ya maji vijijini yenye thamani ya fedha hizo baina ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na wazabuni mbalimbali iliyofanyika mkoani hapa mwishoni mwa wiki ikishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa mkoani hapa Dkt. Binilith Mahenge na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida Juma Kilimba.
Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA mkoa wa Singida Mhandisi Lucas Japhary alisema mikataba ya fedha hizo imegawanyika katika sehemu mbili ambazo mosi ni bajeti ya kawaida na pili ni fedha zinazotokana na miradi ya UVICO- 19.
“Kwa mwaka huu wa fedha tumetengewa fedha za miradi ya maji bilioni 12.1, na leo tunasaini mikataba ipatayo 6 ya sehemu ya hiyo bajeti yenye thamani ya shilingi bilioni 3.9, lakini sehemu ya pili tutasaini mikataba ya fedha zinazotokana na UVICO 19 ambayo kwa mkoa wetu wa Singida kwenye eneo la maji tumetengewa Bilioni 4.9,” alisema Japhary.
Alisema katika fedha hiyo ya Uvico wanatarajia kutumia shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji mijini chini ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani hapa (SUWASA) kwa maeneo ya Singida Mjini, Manyoni na Kiomboi, huku kwa upande wa vijijini miradi 3 inayotokana na fedha hiyo itakayohudumia vijiji 6 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.9 itasainiwa kwa maana ya kila mradi kwenda kuhudumu vijiji viwili.
Aidha, Meneja huyo wa RUWASA alimweleza Mkuu wa Mkoa kwamba kukamilika kwa miradi hiyo ipatayo 9 (kwa maana ya mitatu ya Uvico na sita bajeti ya kawaida) ambayo inatarajia kukamilika ndani ya muda wa kipindi cha miezi 6 kuanzia sasa inatarajia kupunguza kero kubwa ya maji kwa idadi ya wananchi zaidi ya laki tatu ndani ya mkoa wa Singida.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa SUWASA Mhandisi Patrick Nzamba alisema kuhusu hali halisi ya utekelezaji wa miradi ya maji mijini kwa sasa tayari wameshasaini mkataba wa kusambaza mabomba wenye thamani ya shilingi milioni 244, pia mkataba mwingine ni ununuzi na usambazaji wa pampu zinazotarajiwa kufungwa kwenye chanzo cha eneo la Mwankoko na visima ndani ya Manispaa wenye thamani ya shilingi milioni 150.
Pia Nzamba pia alimweleza Mkuu wa Mkoa kwamba mkataba wa tatu ambao wamesaini ni ule wa kuleta mita za malipo ya kabla-ambapo mamlaka hiyo inatarajia kupata Dira za malipo ya kabla zipatazo 300 kutoka moja ya Kampuni ya China-mkataba ambao una thamani ya shilingi milioni 142.
“Mkataba wa nne ambao tumesaini ni wa kuleta vifaa vya maunganisho ya bomba pamoja na bomba za chuma kwa ajili ya maunganisho mapya kwa wateja wapatao 1500-ambapo kati ya hao wateja 1000 watafanyiwa maunganisho kwa miji ya Manyoni na Itigi na wateja 500 itakuwa ni kwa maeneo ya Singida Mjini pamoja na sehemu ya mji wa Kiomboi huku mikataba yote hiyo ikitarajiwa kukamilika mapema 2022,” alisema Nzamba.
Awali, Dkt Mahenge pamoja na kumpongeza Rais Samia na CCM kwa juhudi za makusudi katika utekelezaji wa miradi hiyo muhimu kwa jamii ikiwemo huduma hiyo ya maji, aliwataka wazabuni waliokabidhiwa dhamana ya kujenga miradi hiyo kuhakikisha wanazingatia ubora na viwango.
“Kajengeni miradi imara, yenye ubora, yenye viwango lakini mkajenge kwa wakati unaotakiwa ili wananchi waweze kupata huduma hii muhimu ya maji,” alisema Mahenge na kuongeza;
“Shabaha iliyopo kwa mkoa wa Singida ni kuhakikisha usambazaji wa huduma ya maji vijijini inakwenda kufikia zaidi ya asilimia 80 huku ile ya mijini ikifikia zaidi ya asilimia 90 muda mfupi baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa mikataba hii.”
Mkazi wa Kijiji cha Mwankoko Neema Khambi aliishuku Serikali kwa namna inavyopambana kusogeza huduma hiyo muhimu kwa jamii ikizingatiwa maji ni kila kitu kwa ustawi wa afya,elimu na maendeleo kwa ujumla.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment