BALOZI SHIYO AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA RAIS WA ETHIOPIA | Tarimo Blog


Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) Mhe. Innocent Shiyo amewasilisha Hati za Utambulisho Januari 5, 2022 kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Sahle- Work Zewde Ikulu Ethiopia.

Katika mazungumzo yao, Mheshimiwa Rais Zewde alimkaribisha Balozi Shiyo nchini Ethiopia na kumpongeza kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Ethiopia. Aidha, alisifia mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Ethiopia uliojengwa na waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Mfalme Haile Selassie, ambao walifanya kazi pamoja kuanzisha Umoja wa Afrika.

Aidha, Rais Zewde aliishukuru Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono Ethiopia kwenye masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa ikiwemo kwenye suala la matumizi ya maji ya Mto Nile chini ya ushirikiano wa Nchi za Bonde la Mto Nile.

Vilevile, Mheshimiwa Rais Zewde aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Ethiopia za kuhakikisha changamoto za usalama nchini Ethiopia zinapata ufumbuzi. Pia, amemuahidi Mhe. Balozi Shiyo ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake wakati wote atakapokuwepo nchini Ethiopia.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Shiyo aliishukuru Serikali ya Ethiopia kwa mapokezi na ukarimu alioupata tangu kuwasili kwake nchini Ethiopia tarehe 26 Novemba, 2021. Aidha, aliwasilisha Salamu za heri kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwenda kwa Mheshimiwa Sahle- Work Zewde, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia.

Aidha, Mhe Balozi Shiyo alirejea mafanikio ya ziara ya Mhe. Rais Sahle-Work Zewde aliyoifanya nchini Tanzania mwezi Januari 2021 ambapo nchi zote mbili zilikubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, uchukuzi, nishati, mifugo na bidhaa za Ngozi, utalii, uhamiaji na ulinzi na usalama.

Balozi Shiyo ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuimarsha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kwenye maeneo hayo na maeneo mengineyo yenye manufaa kwa pande zote mbili. Balozi Shiyo pia ameongelea kuhusu suala la kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili kwenye Chuo Kikuu cha Addis Ababa kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Addis Ababa.

Balozi Shiyo amemhakikishia Mheshimiwa Rais Zewde kwamba Tanzania itaendelea kuunga mkono Ethiopia kwenye jithada za kurejesha amani na usalama nchini humo.
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) Mhe. Innocent Shiyo akiwasilisha hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Sahle- Work Zewde Ikulu, Ethiopia
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Sahle- Work Zewde akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) Mhe. Innocent Shiyo mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Sahle- Work Zewde katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) Mhe. Innocent Shiyo





Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Sahle- Work Zewde na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) Mhe. Innocent Shiyo katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa waliohudhuria hafla ya kuwasilisha Hati za Utambulisho


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2