* Waahidi kuendelea kutoa huduma bora ya usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam
WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART,) sambamba na watoa huduma katika Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART,) wameadhimisha siku ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya mazoezi kupitia bonanza maalum lililowakutanisha wafanyakazi kwa malengo ya kujenga afya na kujenga uhusiano mwema katika utekelezaji wa majukumu yao hasa la kutoa huduma ya usafiri kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa Bonanza hilo Mkurugenzi wa Utawala, Usimamizi wa Rasilimali watu na Mawasliano wa Wakala wa mabasi yaendayo haraka Dkt. Eliphas Mollel ambaye alimwakilisha Mkurugenzi mkuu wa Wakala hiyo amesema bonanza hilo limelenga kuwaweka wafanyakazi pamoja na kujenga afya ya watumishi hasa kwa wakati huu ambapo dunia inapambana na ugonjwa wa UVIKO-19 ambao baada ya kupata chanjo mazoezi pia ni muhimu katika kujenga afya,
Amesema, katika bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali ya kujenga afya na mahusiano bora kwa wafanyakazi;
''Mwaka jana bonanza liliwakutanisha wafanyakazi wa DART ila leo tumeenda mbali zaidi kwa kuwashirikisha wenzetu wa UDART ambao ni watoa huduma wetu na tunaamini tumejenga kitu kimoja muhimu katika kutekeleza majukumu yetu ya kazi ya kuwahudumia wananchi katika usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam.'' Amesema.
Dkt. Mollel amesema wafanyakazi walipata nafasi ya kufanya mazoezi ya michezo waliyoshiriki na kwa bonanza linalofuata watashirikisha Wizara mojawapo kushiriki katika bonanza la namna hiyo ambalo hufanyika kila robo ya mwaka.
Aidha amezitaka taasisi nyingine kufanya mazoezi kwa watumishi kwa afya, kuwaleta pamoja wafanyakazi na kujenga mahusiano ya bora ya ushirikiano katika utendaji kazi.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Operesheni wa UDART Eng. Nestory Ngolomela amesema, wakiwa watoa hudma wa mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam wamefurahishwa na ushirikiano huo ambao ni muhimu katika kujenga mahusiano imara baina ya Wakala hiyo na watoa huduma ili kuweza kufanikisha kutoa huduma yenye ubora zadi kwa wananchi.
Amesema ushiriki wa wafanyakazi wengi wa UDART katika bonanza hilo la michezo hakujaathiri utoaji wa huduma za usafiri katika Mkoa huo.
''Kimsingi UDART ina wafanyakazi zaidi ya 800, huduma inaendelea vizuri...uwepo huu wa pamoja pamoja na DART umeongeza ufanisi katika jukumu ambalo Serikali imetupatia sisi kama watoa huduma na wenzetu kama wakala, 'Umoja wetu ndio Nguvu yetu.' tunategemea mafanikio makubwa katika jukumu la kutoa huduma kwa wananchi.'' Amesema.
Baadhi ya wafanyakazi walioshiriki bonanza hilo wameeleza namna walivyoweza kukutana na kubadilisha uzoefu wa kazi zao pamoja na kufanya mazoezi ya kujenga afya zao na kuburudika pamoja.
Bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo Netiboli, mpira wa miguu, riadha, kukimbia kwenye magunia, kukimbiza kuku na kuvuta kamba ambapo washindi walijishindia zawadi za fedha taslimu.
Mkurugenzi wa Utawala, Usimamizi wa Rasilimali watu na Mawasliano wa Wakala wa mabasi yaendayo haraka Dkt. Eliphas Mollel akizungumza mara baada ya kumalizika kwa bonanza hilo na kueleza kuwa wataendelea kuwakutanisha wafanyakazi kupitia mabonanza yanayofanyika kila robo ya mwaka ili kujenga magusiano bora ya kuwatumikia wananchi na kuboresha afya za wafanyakazi. Mkuu wa Idara ya Operesheni wa UDART Eng. Nestory Ngolomela akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa bonanza hilo ambapo ameeleza kuwa ushirikiano huo utaleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mradi wa utoaji wa huduma ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Baadhi ya wafanyakazi wakizungumza mara baada ya kumalizika kwa bonanza hilo na kueleza kuwa kupitia ushirikiano huo uhusiano wao katika utendaji kazi wa kuwahudumia wananchi utaimarika zaidi, leo jamii Dar es Salaam.
Michezo mbalimbali ikiendelea.
Baadhi ya viongozi wakifuatilia mashindano mbalimbali.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment