Mhandisi wa Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Singida, Costantine Stephano akiwa kazini. |
Mjumbe wa Kamati ya siasa Mkoa wa Singida, Diana Chilolo (katikati) akicchangia jambo wakati kamati hiyo ilipokuwa ikikagua ujenzi wa Zahanati ya Unyianga,.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida imekagua miradi ya maendeleo iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida na Singida Manispaa na kuridhishwa na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti jana wakati kamati hiyo ikikagua miradi hiyo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapa , Alhaji Juma Kilimba alisema ameridhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo katika halmashauri hizo.
"Kwa kweli tunawapongeza kwa kuitendea haki miradi hii ambayo Serikali inatumia fedha nyingi kuitekeleza hasa ujenzi wa madarasa yalitokana kwa fedha za mradi wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19," alisema Kilimba.
Kilimba alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwan kutoa fedha hizo na kuwaomba viongozi ilipo miradi hiyo kuwahamasisha wananchi wao kuitunza kutokana na umuhimu wake.
Alisema Serikali inafanya kazi kubwa ya kutoa fedha za miradi na ni wajibu wa wananchi nao kuhamasika kuunga jitihada za serikali kwa kujitolea kufanya kazi zingine za maendeleo ambazo zipo ndani ya uwezo wao.
Kilimba alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa madarasa hayo ambayo kwa mkoa mzima zimetumika Sh.13,444,000,000 kumewaondolea adha ya kusoma katika mazingira yasiyo rafiki kwa wanafunzi kuanzia shule shikizi, msingi na sekondari.
Alisema hivi sasa nchini kote baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya kazi kubwa ya kutoa fedha hizo wananchi hawazungumzii tena ujenzi wa madarasa au ukosefu wa madawati kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na kuwa nguvu inaelekezwa kuhimarisha mitaala.
Katibu wa CCM Mkoa wa Singida Lucy Boniphace amewapongeza mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wataalamu kwa kutekeleza kwa umakini wa hali ya juu kufanya kazi nzuri ya kusimamia ujenzi wa madarasa hayo kama alivyotaka Rais Samia Suluhu.
"Kwa kweli mnyonge mnyongeni lakini hakiyake mpeni, Rais Mama Samia Suluhu Hassan hakika ametuheshimisha watanzania tuna kila sababu ya kumshukuru na kumuombea kwa Mungu" alisema Boniphace.
Wajumbe wa kamati hiyo wakizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo waliwapongeza wakuu wa shule na viongozi waliosimamia fedha za kutekeleza miradi hiyo kwa kuwa waaminifu na kufanikisha miradi hiyo.
Baadhi ya miradi iliyokaguliwa na kamati hiyo katika Wilaya ya Singida ni ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Sekondari ya Ntonge ambayo yamegharimu Sh.Milioni 40, ujenzi wa madarasa matatu Shule ya Sekondari ya Ilongero ambayo yamegharimu Sh.60 Milioni, ujenzi wa chumba cha wagonjwa mahututi Hospitali ya Wilaya ya Singida na nyumba moja ya watumishi ambao umegharimu Sh.340 Milioni 340 na ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Sekondari Mrama ambayo yamegharimu Sh. 40 Milioni.
Katika Manispaa ya Singida miradi iliyotekelezwa ni ujenzi wa madarasa sita katika Shule ya Sekondari Mandewa ambayo yaligharimu Sh.120 Milioni pamoja na samani zake na pia walipokea Sh.12.5 Milioni zilizotokana na tozo za miamala ya simu ambazo zilitumika kujenga chumba kimoja cha darasa.
Miradi mingine iliyotekelezwa katika manispaa hiyo ni ujenzi wa barabara mpya ya Unyianga yenye urefu wa kilometa 2.6 ambayo itakuwa mbadala baada ya barabara ya awali kukatika kutokana na mvua zilizonyesha mwaka 2019 na 2020 ambao ujenzi wake utagharimu Sh.263,117,200.
Mradi mingine ni ujenzi wa Zahanati ya Unyianga na Mradi wa kutengeneza samani wa Kikundi cha Vijana Chapakazi cha Kata ya Mitunduruni ambacho kilikopeshwa Sh.10 Milioni na Manispaa hiyo.
Ziara hiyo iliwahusisha viongozi na wataalamu mbalimbali wa wilaya hizo pamoja na Mkuu wa Wilaya hizo Mhandisi Paskas Muragili.
Leo kamati hiyo itafanya ziara ya namna hiyo katika Halmashauri za Wilaya ya Iramba, Mkalama na Ikungi wakati jana ziara hiyo imefanyika katika wilaya za Manyoni, Itigi, Singida na Singida Manispaa.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment