Baadhi ya Mabalozi wakiangalia bidhaa zilizotengenezwa na kiwanda cha A to Z cha mkoani Arusha wakati Mabalozi hao walipofanya ziara kiwandani hapo. Lengo la ziara hiyo ni kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na wakati
Afisa Afya kutoka Wizara ya Afya Bw. Mohamed Mtosa akitoa maelezo kwa Mabalozi wa Kodi walipotembelea Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Forodha Namanga mkoani Arusha. Kutoka kushoto ni Balozi Zulfa Omary, ambae ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar, Balozi Bw. Edo Kumwembe na Balozi Subira Mgalu Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani. Afisa Forodha kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. James Mwasambili akitoa maelezo kwa Mabalozi wa Kodi waliotembelea Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Forodha Namanga mkoani Arusha. Kutoka kulia ni Meneja Msaidizi wa Forodha Kituo cha Namanga Bw. Paul Kamukulu, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Bw. Richard Kayombo, Balozi Zulfa Omary, ambae ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar na Balozi Subira Mgalu Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani.Mshauri wa Kodi Bw. Nikolaus Duhia (wa kwanza kulia) akitoa maoni yake wakati wa kikao kazi cha Mabalozi wa Kodi, baadhi ya Wafanyabiashara na Wadau wa Kodi wa Mkoa wa Arusha uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo. Lengo la kikao kazi hicho ni kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na wakati.
Mkurugenzi wa kiwanda cha A to Z cha mkoani Arusha akiwaonesha Mabalozi wa Kodi bidhaa mbalimbali wakati Mabalozi hao walipofanya ziara kiwandani hapo. Lengo la ziara hiyo ni kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na wakati. .
(Picha na TRA)
*************************
Na Mwandishi wetu
Namanga
Mabalozi wa Kodi walioteuliwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wako katika mikoa ya Kaskazini ambayo ni Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa ajili ya kuhamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari ili kuongeza mapato ya Serikali.
Mabalozi hao wamepata fursa ya kutembelea Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha mpakani Namanga mkoani Arusha na kukutana na baadhi ya wadau na walipakodi ambapo wamewahimiza kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati.
Wakizungumza wakati wa ziara hiyo Mabalozi hao wa kodi, wameipongeza Serikali kwa kuwa na Vituo vya Huduma kwa Pamoja mipakani kwani vimeondoa kero zilizokuwepo kipindi cha nyuma na kusifu ushirikiano uliopo katika ya TRA na wafanyabiashara ambao umesaidia Mkoa wa Arusha kuvuka malengo ukusanyaji mapato.
“Katika kituo hiki cha Namanga, nimejifunza mambo mengi, moja wapo ni namna nchi hizi mbili za Tanzania na Kenya zilivyoondoa urasimu uliokuwepo kipindi cha nyuma.
Nikiwa kama Balozi, nitatumia elimu hii niliyoipata kutoka TRA kuwahamasisha wananchi kujenga tabia ya kulipa kodi kwa wakati kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Bw. Edo Kumwembe mmoja wa mabalozi hao.
Kwa upande wake Balozi Zulfa Omari, ambae ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar akizungumza wakati wa kikao kati ya wafanyabiashara wa Arusha na mabalozi hao, alisema kuwa ni nadra sana kukuta wafanyabiashara wakiizungumzia vizuri TRA lakini amefarijika kuona walipakodi wa Arusha wakiipongeza TRA kwa kuboresha huduma zao.
“Kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi kulikuwa na mambo mengi niliyokuwa nikiyasikia kuhusu TRA na yalikuwa yakiniumiza sana lakini hapa Arusha nimesikia kitu cha faraja kwamba TRA inazungumzwa vizuri mbele yetu kitu ambacho si kitu cha kawaida maana wafanyabiashara mara nyingi huwa hawaizungumzii vizuri TRA,” alisema Balozi Zulfa.
Balozi mwingine ni Subira Khamis Mgalu Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani ambae alisema kuwa kupitia ziara hii amejifunza taratibu mbalimbali zinazotumika wakati wa uingizaji wa mizigo kutoka ndani na nje ya nchi kupitia Kituo cha Namanga.
“Kama Balozi nimefahamu kwa kina jinsi mifumo inavyofanya kazi katika kituo hiki cha Namanga ambayo huisaidia Serikali kukusanya mapato stahiki kutoka vyanzo mbalimbali.
Kwa upande wa walipakodi na wadau ambao tumekutana nao Arusha Mjini, naweza kusema kuwa, usemi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan umedhihilika wazi kuwa, kodi inaweza kukusanywa bila kutumia mabavu kwa sababu Mkoa huu wa Arusha umevuka malengo bila kuwasumbua walipakodi wake.”
Balozi Mgalu amewasisitiza walipakodi hao kuongeza ushirikiano kwa TRA ili kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuwaahidi kwamba, changamoto zote walizozitoa wamezipokea na watazifanyia kazi.
Kazi wanazozifanya Mabalozi hao wa Kodi katika ziara yao ya kikazi kwenye mikoa hiyo ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga ni pamoja na kutembelea viwanda, kutembelea vituo vya huduma kwa pamoja mipakani na kukutana na wafanyabiashara kwa ajili kuwahamasisha kulipa kodi kwa hiari na wakati.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment