MAJALIWA KAGUA UJENZI WA MADARASA KATIKA SHULE YA MSINGI SHIKIZI KAZAROHO WILAYANI BABATI | Tarimo Blog

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Shikizi  Kazaroho wilayani Babati wakati alipokagua ujenzi wa madarasa katika shule hiyo akiwa katika ziara ya mkoa wa Manyara,  Januari 25, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


*Lengo ni kuhakikisha matamanio yake kwa Watanzania yanatimia

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wasaidizi wote wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wamejipanga kuhakikisha kwamba wanamsaidia kwa weledi wote, uaminifu ili malengo na matamanio yake ya kuwaletea Watanzania maendeleo yaweze kufanikiwa.

Hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuwa na imani ya Serikali kwa sababu imedhamiria kuwatumikia kwa lengo la kuboresha na kuimarisha maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumanne, Januari 25, 2022) alipozungumza wananchi baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba sita vya madarasa katika shule ya Msingi Shikizi Kazaroho iliyoko wilayani Babati akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Manyara.

Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali imeendelea kuweka mipango ya kuboresha sekta ya elimu nchini ili kila mtoto apate elimu bora, hivyo alisisitiza kila kulipokuwa na shule ya msingi lazima kuwe na madarasa ya awali. “Wazazi tuhakikishe watoto wetu wanakwenda shule.”

Nao, wanafunzi wa shule hiyo wakizungumza mbele ya Waziri Mkuu walimshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa uamuzi wake wa ujenzi wa madarasa hayo yaliyojengwa kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwani madarasa haya yaliyojengwa karibu na makazi yetu yametusaidia kutuondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu. Tunaomba na walimu wetu wajengewe nyumba kwani wanaishi mbali na hapa shuleni.”

Naye, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Babati Mji zikiwemo sh. bilioni 2.5 za ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Domonick Magula alisema shule ya msingi Shikizi Kazaroho ilianzishwa mwaka 2018 ikiwa na wanafunzi 58 wa darasa la awali, ambapo kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 332 kuanzia darasa la awali hadi darasa la tano. Madarasa hayo sita yamegharimu sh. milioni 120.

Awali, Mheshimiwa Majaliwa alikagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Babati, ambapo alisema kuwa ujenzi wa hospitali hiyo una lengo la kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, hivyo utawapunguzia safari ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Waziri Mkuu alisema Mheshimiwa Rais Samia anataka kuona wananchi wakipatiwa huduma mbalimbali zikiwemo za afya karibu na maeneo yao ya makazi. “Tumekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi na huduma zote zipatikana hapa hakuna sababu ya kwenda mkoani.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Festo Dugange alisema Serikali imetoa shilingi 300 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kisasa la kutolea huduma ya dharura katika hospitali ya wilaya ya Babati na sh. milioni 90 za ujenzi wa nyumba tatu za watumishi.

Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Babati, Dkt. Hoseah Madama aliishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa hos[itali ya wilaya hiyo.

Alisema mradi huo unajengwa kwa awamu mbili ambapo ya kwanza inajumuisha ujenzi wa majengo mawili ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje na maabara na awamu ya pili inahusisha ujenzi wa majengo matano nayo ni utawala, mama na mtoto, kufulia, mionzi na stoo ya dawa.

“Ujenzi wa mradi huu kwa awamu ya kwanza ulianza Juni 11, 2020 na ulikamilika Januari 5, 2021 na awamu ya pili ilianza Mei 10, 2021 na inatarajiwa kukamilika Februari 10, mwaka huu. Mpaka sasa mradi huu umegharimu sh. bilioni 1.4 ikiwa ni fedha kutoka Serikali Kuu.”

Alisema Halmashauri imejipanga kuanza kutoa huduma za afya kwa wananchi kwa kuanzia na majengo mawili yaliyokamilika ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje na maabara mwezi Februari mwaka huu baada ya kukamilika kwa mifumo ya maji safi na maji taka.

Huduma zitakazotolewa katika hospitali hiyo baada ya kukamilika ni pamoja na matibabu ya wagonjwa wa nje na kulaza, vipimo mbalimbali vya maabara na radiolojia na kliniki mbalimbali zikiwemo kliniki za madaktari bingwa zitakazokuwa zikitolewa kila baada ya robo mwaka.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2