Makumbusho ya Taifa Watengeneza Kanuni kurahisisha Utendaji | Tarimo Blog


Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Noel Lwoga akifungua kikao kazi cha kutengeneza Kanuni za Sheria Na 7 ya Makumbusho ya Taifa ya mwaka 1980 kinachofanyika katika ukumbi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jiji Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Bibi Nuru Sovella na kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Malikale Dkt Bwasiri.
Baadhi ya Wataalamu wa Makumbusho ya Taifa wakimsikiliza Mkurugezni Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Noel Lwoga (hayumo pichani)  wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kutengeneza Kanuni za Makumbusho ya Taifa


Na Joyce Mkinga

MAKUMBUSHO ya Taifa la Tanzania wako katika maandalizi ya Kanuni za Sheria ya Kuanzisha kwa Taasisi hiyo(Sheria ya Makumbusho ya Taifa Namba 7 ya mwaka 1980).

Watumishi wa Taasisi hiyo wamejifungia ndani ya moja ya ukumbi wa Taasisi hiyo kwa lengo la uchambuzi wa Sheria na mifumo ya utendaji kwa lengo la kuandaa Kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt Noel Lwonga amesema maandalizi ya kanuni za kutekeleza sheria ya Taasisi hiyo ni muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi na weledi.

Amesema kuwa tangu kutengenezwa kwa Sheria hiyo mwaka 1980 haikuwa na kanuni ambazo zingeweza kuwezesha utekelezaji wake, hivyo ni wakati muafaka sasa kwamba viongozi na wataalamu wa taasisi hiyo kuweza kutengeneza Kanuni za kutekeleza Sheria hiyo.

“ Kazi ya Kanuni ni kufafanua zaidi juu ya yale yaliyomo kwenye Sheria ili utekelezaji wake uwe wa ufanishi na weledi,” alisema Dkt. Lwoga.

Akitoa mfano, amesema Sheria ya Makumbusho ya Taifa imeeleza kuwa Makumbusho ya Taifa ni taasisi ya kisayansi, kielimu na kiutamaduni yenye jukumu la kukusanya, kutafiti kuhifadhi na kutoa elimu juu ya urithi wa asili na utamaduni wa nchi.

Dkt Lwoga amesema kuwa Sheria inaeleza kwa ujumla juu ya utekelezaji na utendaji wa majukumu ya taasisi lakini kanuni zinaeleza kwa undani jinsi ambavyo kazi za Makumbusho zitakavyotekelezwa.

Kanuni zinazoandaliwa zitaeleza juu ya kazi ya kukusanya mikusanyo kwamba ni ya jinsi gani na itakusanyajwe, itatoa mwongozo wa weledi wa jinsi ya kukusanya, jinsi ya kufanya tafiti na utoaji elimu, amesema Dkt Lwoga.

Amesema kazi hii ni sehemu ya maelekezo ya Ilani ya CCM ambayo imeelekeza juu ya kuzipitia na kuboresha sheria za taasisi za maliasili na utalii na kuandaa kanuni za utekelezaji wa sheria hizo.

Dkt. Lowga amesema kazi hii pia iko katika mwelekeo wa taasisi yake unaolenga katika kuboresha sheria na kuandaa kanuni ili kutekeleza maadili ya fani ya makumbusho na malikale.

“Tunatarajia kuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya makumbusho na malikale kwa kuwahusisha jamii katika uanzishwaji na uendelezaji wa Makumbusho na malikale,” amesema Dkt Lwoga.

Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Makumbusho ya Taifa, Bw. Mtibora Selemani amesema kuwa kazi hiyo inashirikisha viongozi na wafanyakazi katika idara na vitengo vyote ili kupata maoni mtambuka.

“Kazi hii inashirikisha wataalamu wa vitengo vyote ili tuweze kupata maoni kulingana na weledi wa kila idara na kitengo,” amesema Bw, Mtibora.
Washiriki wa Kikao kazi cha Kutengeneza Kanuni za Sheria ya Makumbusho ya Taifa wakiwa katika picha ya pamoja nje ya jengo la Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2