Mbunge wa Jimbo la Mjini Magharibi Viti Maalum Mhe. Tawheeda Garlos (MNEC) ambaye alikuwa mgeni rasmi, akizungumza katika Maadhimisho ya miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Singida DC yaliyofanyika juzi mkoani Singida. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, William Nyalandu.
Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Jimbo la Mjini Magharibi Viti Maalum Mhe. Tawheeda Garlos (MNEC) amewataka Wanawake kufanya kazi kwa bidii na kwa kujiamini pamoja na kuondoa dhana ya kwamba wao hawawezi kuongoza kwa kuwa ni mwanamke kwani mtu yeyote anaweza kuwa kiongozi.
Hayo aliyasema wakati wa maadhimisho ya sherehe za kutimiza miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyoadhimishwa na Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Singida (UWT)
Mhe Tawheda alisema kwa sasa nchi yetu inaongozwa na mwanamke na anatuongoza vizuri sana! Anatimiza hamu na kiu ya watanzania, analiendesha gurudumu la maendeleo vizuri kwa maslahi mapana ya watanzania.
"Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi makini na mwenye uwezo mkubwa na ameudhihirishia ulimwengu kwamba wanawake tunacho kipaji cha kuongoza licha ya kuwa na majukumu mengi tuliyonayo ya kifamilia lakini tunapokuwa na jukumu la kuongoza tunalifanya kwa ufanisi mkubwa na kuhakikisha malengo yanatimia" alisema Garlos.
Aliwataka Wanawake kuiga mfano wa mhe Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anachapa kazi kwa juhudi na weledi mkubwa.
Katika maadhimisho hayo mhe Tawheeda alitembelea Kituo cha Afya cha Ilongero cha Wilaya ya Singida na kujionea jinsi kinavyotoa huduma pamoja na kuona changamoto zake na kuahidi kushirikiana na wabunge wa Singida kuzisemea ambapo pia alipata nafasi ya kuwaona wagonjwa na kuwapa zawadi kwa lengo la kuwafariji.
Awali Mbunge Tawheeda alipowasili ofisi za chama alilakiwa na viongozi wa chama wa UWT na Jumuiya ya Wazazi wilayani humo wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo William Nyalandu na baadaye alipata fursa ya kupanda mti katika ofisi ya chama wilaya na kuongoza Harambee ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya mtendaji wa chama.
Miongoni mwa shughuli alizozifanya akiwa wilayani humo ni kugawa kadi kwa wanachama wapya zaidi ya 100 waliojiunga na CCM.
Maadhimisho hayo pia yalihudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mhe.Ramadhani Ighondo na Mhe.Aysharose Mattembe Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida pamoja na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali.
Viongozi wengine waliokuwepo ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya ya Singida DC, Anthony Katani. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya Singida Alexander Mbogho, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake UWT Wilaya ya Singida DC Neema Sambaa na Katibu wa UWT wilaya Naomi David.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment