MKOA WA RUVUMA WAZALISHA ZAIDI YA TANI MILIONI 1.3 ZA CHAKULA | Tarimo Blog


MKOA wa Ruvuma umefanikiwa kuvuna tani 1,384,705 za mazao ya chakula katika msimu wa kilimo 2020/2021,huku mahitaji ya chakula kwa wakazi wa mkoa huo ni tani 470,000 hivyo kuwa na ziada ya tani 914,705.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge alisema hayo jana, wakati akizungumza na wataalam wa idara na taasisi mbalimbali za Serikali katika kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Manispaa ya Songea.

Alisema, kutokana na uzalishaji huo mkoa wa Ruvuma umeendelea kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa mara ya tatu mfululizo na kuwapongeza wakulima kwa jitihada kubwa wanazofanya katika uzalishaji mashambani.

Aidha alisema, kwa upande wa zao la mahindi wakulima waliuza mahindi yao kupitia soko la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA) baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa Sh.bilioni 50 kwa ajili ya mikoa inayolima mahindi ikiwemo mkoa wa Ruvuma.

Alisema,mkoa utaendelea kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umeonesha mafanikio makubwa, ambapo katika msimu 2020/2021 zao la ufuta kilo 8,326,686 ziliuzwa kati ya bei ya Sh.1,998 na 2,393 kwa kilo na kuwaingizia wakulima Sh. bilioni 17,221,852,087.

Mkuu wa mkoa alitaja mazao mengine ni Soya ambayo iliuzwa kilo 1,090,199 na Sh.1,547,202,688 zilipatikana na huku zao la mbaazi nalo likionesha mafanikio makubwa ambapo kwa mara ya kwanza wakulima wa mkoa huo waliuza jumla ya kilo 7,109,360 kwa bei ya Sh.1,428 na 990 na kuwapatia wakulima Sh.9,313,114,073.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Ibuge ni kwamba, mafanikio ya uzalishaji yanatokana na matumizi bora ya pembejeo za kilimo ambapo Serikali inaendelea kuhamasisha wakulima kutumia mbolea mbadala kuliko walizozoea ambazo bei zake ziko juu.

Katika kuendeleza shughuli za kilimo Mkuu wa mkoa alieleza kuwa,mkoa umeandaa mpango wa utekelezaji wa shughuli za kilimo kwa pamoja na kilimo cha mkataba(Block& Contract Farming) katika msimu wa kilimo 2021/2022 na mpango huo utahusisha mazao ya alizeti,soya na ufuta.

Alisema,lengo la mpango huo ni kuwaongezea tija na kipato wakulima kupitia mazao yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na tayari mko umeshatambua maeneo yanayofaa kwa kilimo hicho ambapo jumla ya ekari 48,343.35 zimetengwa katika Halmashauri zote nane.

Hata hivyo alisema,mafanikio ya shughuli za kilimo kwa sasa yanategemea sana mvua ambazo mwaka huu imeshaelezwa zitakuwa chache, kwa hiyo amewakumbusha wakulima kupanda mazao mara tu mvua zitakapoanza kunyesha na kupanda mazao ya muda mfupi yasiohitaji mvua nyingi.

Katika hatua nyingine,Ibuge amewakumbusha watendaji na watumishi wa umma umuhimu wa kusimamia mapato yatokanayo na kodi pamoja na ushuru kuwa kazi hiyo ni ya kila mmoja kwani fedha zinazopatikana zinatumika kujenga miradi ya maendeleo ikiwemo vituo vya afya,barabara,ununuzi wa ndege na ujenzi wa Reli.

Brigedia Jenerali Ibuge,amewapongeza Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za mitaa kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo Halmashauri zote zilikusanya mapato vizuri na kufanya mkoa kukusanya jumla ya Sh.16,984,706,090 kati ya lengo la kukusanya Sh.16,365,090,734.95.
Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma  ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Madaba Joseph Mhagama kulia,akimpa zawadi Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ya kutambua mchango wake katika juhudi mbalimbali za maendeleo anazozifanya katika mkoa huo ikiwemo uzalishaji wa chakula na mapambano dhidi ya ugonjwa Covid 19.Picha zote na Muhidin Amri,
Songea
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na wakuu wa idara na taasisi mbalimbali za Serikali  wa mkoa huo katika kikao kazi kati yake na watumishi,ambapo alitumia kikao hicho kuwataka watumishi wa ngazi mbalimbali kuendelea kuchapa kazi ili kufikia malengo ya mkoa.
 Baadhi ya wakuu wa idara  na taasisi mbalimbali za Serikali mkoani Ruvuma wakimsikiliza Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge(hayupo pichani)katika kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Songea,

 Baadhi ya Maafisa Mipango wa Halmashauri za mkoa wa Ruvuma wakifuatilia taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu kutoka kwa Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge(hayupo pichani)ambapo Mkuu wa mkoa amewataka watumishi wa umma kuendelea kuchapa kazi na kutumiza wajibu wao katika kuwatumikia wananchi.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2