MKUTANO WA NNE WA JPC NGAZI YA MAKATIBU WAKUU WAFANYIKA JIJINI KAMPALA, UGANDA | Tarimo Blog

Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje wa Tanzania na Uganda wamefungua Mkutano wa Nne wa Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika leo tarehe 18 Januari 2022 katika Ngazi ya Makatibu Wakuu jijini Kampala, Uganda.

Akihutubia katika Mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab ameishukuru serikali ya Uganda kwa mapokezi mazuri sambamba na maandalizi mazuri ya Mkutano.

Pia, akaeleza tangu kumalizika kwa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Nchi hizo mbili mwaka 2019, masuala mengi yametekelezwa kwa pamoja katika nafasi mbalimbali na kupitia utaratibu wa Mikutano ya kisekta ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

''Nchi zetu zinatakiwa kufuatilia utekelezaji katika sekta za ushirikiano kuanzia ngazi ya Wizara, Idara na Taasisi za Seriakali ili  kutatua changamoto na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano", alisema Balozi Fatma.

Kwa upande wa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Uganda, Bw. Kagiire Waiswa alieleza Mkutano huu unajadili na kutathimini utekelezaji katika sekta za ushirikiano zitakazowasilishwa katika Mkutano Ngazi ya Mawaziri utakaofanyika kesho tarehe 19 Januari 2022.

''Ni imani yangu kuwa majadiliano katika Mkutano huu yatafikiwa muafaka kwa namna bora na yatazingatia ushauri wa kitaalamu kutoka pande zote mbili", alisema Bw. Waiswa.

Pia akaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta timu ya Wataalamu iliyokamilika na kurahisisha majadiliano katika sekta zote za ushirikiano zilizokubaliwa na Nchi hizo.

Viongozi hao kwa pamoja wameonesha imani kubwa waliyonayo kupitia majadiliano hayo ili kuimarisha ushirikiano katika sekta za Biashara, Uwekezaji, Siasa na Diplomasia, Nishati, Maji na Mazingira, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Utalii, Afya, Kilimo, Mifugo, Uvivu, na Elimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. 


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika leo tarehe 18 Januari 2022 katika ngazi ya Makatibu Wakuu jijini Kampala, Uganda.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Uganda Bw. Bagiire Vincent Waiswa akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika leo tarehe 18 Januari 2022 katika ngazi ya Makatibu Wakuu jijini Kampala, Uganda.
Balozi Fatma (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakifuatilia majadiliano wakati wa Mkutano huo.

Kutoka Kulia ni Dkt. Hashil Abdalla Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara pamoja na Bw, Kheri Mahimbali Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati wakifuatilia majadiliano wakati wa mkutano huo.
Kutoka Kulia ni Dr. Ally Possi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) na Bw. Mohammed Addulla, Naibu Katibu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakifuatilia majadiliano kwenye Mkutano huo.  
Bw. Kagiire Waiswa pamoja na Mhandisi Irene Okello Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa Uganda wakifuatilia Mkutano.

Makatibu Wakuu na ujumbe wa Uganda wakifuatilia Mkutano.

Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Uganda ikifuatilia Mkutano.

 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2