Na Mbaraka Kambona, Iringa
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewashauri Wafugaji nchini kufuga kibiashara na kuachana na ufugaji wa kuchunga ambao tija yake imekuwa ndogo kwao wenyewe na hata kwa Taifa pia.
Waziri Ndaki alitoa rai hiyo jana alipotembelea Shamba la kisasa la mifugo la Shaffer lililopo Mkoani Iringa.
Akiwa katika shamba hilo akikagua shughuli mbalimbali zinazoendelea kwenye eneo hilo alisema kuwa wanawashauri wafugaji kuanza kufuga kisasa na kuachana na ufugaji wa kiasili ambao sasa umeanza kupitwa na wakati.
"Tumekuwa hatuoni faida kwa mifugo yetu kwa sababu ya kung'a ng'ania ufugaji wa kiasili, wafugaji tuanze kufuga kibiashara ili tuongeze tija ya mifugo yetu", alisema Mhe. Ndaki
Aliongeza kuwa ili waanze kuona tija ya ufugaji wao ni lazima wabadilike na waache ufugaji wa kuzunguka kutafuta maeneo ya malisho na badala yake wawe na maeneo yao ya kufugia ambayo yatakuwa rahisi kufikiwa na Wataalamu kwa ajili ya kuwapatia huduma zinazohitajika kwa mifugo yao.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bw. Bashiru Muhoja alisema kuwa Mwekezaji wa shamba hilo la mifugo la Shaffer anauhitaji mkubwa wa chakula cha mifugo yake kama vile soya na mahindi.
"Mhe. Waziri huyu mfugaji anauhitaji mkubwa wa soya, mahindi na alfaalfa ambapo kwa sasa vyote anavitoa nchini Zambia, hii ni fursa kwa wananchi wetu na tumeshaanza kuchukua jitihada na tunaorodha ya wakulima ambao wapo tayari kulima mazao hayo kwa ajili ya kumuuzia mfugaji huyu", alisema Muhoja
Kwa upande wake, Msimamizi wa Shamba la Shaffer, Bw. Mahboob Malick alisema kuwa wanaishukuru Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa inaowapatia na kwamba wako tayari kuendelea kushirikiana nayo kwa lengo la kuboresha ufugaji hapa nchini."Mhe. sisi tuko tayari kupokea vijana ambao wanataka kujifunza ufugaji waje hapa tutawafundisha namna bora ya ufugaji wa kisasa ili wakipata ujuzi huu waende kuwafundisha na wenzao na hatimaye kuboresha ufugaji wetu", alisema Malick
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment