WASAFI TV YAONYWA, YATAKIWA KUFUATA KANUNI, SHERIA NA MAADILI | Tarimo Blog




Mwenyekiti wa Kamati ya maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) Ndalahwa Gunze akisoma uamuzi wa kamati hiyo juu ya mashtaka ya ukiukaji wa kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na Posta yaliyofanya na kituo cha utangazaji cha Wasafi Tv Company Limited.




MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekitaka Kituo cha Utangazaji cha Wasafi TV Compay Limited kuzingatia misingi, sheria, kanuni, madili na weledi katika kusimamia na kuhariri maudhui mtandaoni ili kuepuka kurusha maudhui yenye utata.

Agizo hilo limekuja baada ya kituo hicho kupitia televisheni ya Wasafi na chaneli ya maudhui mtandaoni (Youtube,) kupitia kipindi cha 'Refresh' kurusha mahojiano baina ya mtangazaji wa kipindi hicho Aaliyah Mohamed na msanii wa Muziki wa Bongo Fleva Zuhura Othman maarufu kama Zuchu ambaye alisikika akitumia lugha chafu ya matusiya nguo ni, isiyo na staha hasa kwa watoto na haikupaswa kutangazwa katika kituo cha utangazaji.

Akisoma uamuzi wa kamati ya maudhui ya Mamlaka hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo Ndalahwa Gunze amesema, Machi 6, 2021 kituo hicho kilirusha maudhui hayo na mtangazaji wa kipindi hicho Aaliyah alionekana kutochukua hatua na kumuacha msani huyo kuendelea kutoa lugha chafu na maneno yasiyo na staha na kituo hicho hakikuchukua hatua yoyote ya kuondoa maudhui hayo mtandaoni na kuendelea kuonekana hadi tareheDisemba 20, 2021.

Amesema kwa kitendo cha kuutangazia Umma maudhui yenye lugha chafu ya matusi ya nguoni isiyo na staha na isiyofaa hasa kwa watoto Wasafi TV Company Limited inatuhumiwa kukiuka kanuni 11 (1) (c), 11 (2) (a), (b) na (e) 12 (1) (a) na (b) na 12 (a) (b) na (c) za kanuni za Mawasiliano ya Kielekroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji wa Redio na Televisheni) ya 2018.

Ndalahwa amesema Mamlaka hiyo kupitia kamati ya maudhui ilikiandikia kituo hicho wito wa maandishi na kufika mbele ya kamati ya maudhui kutoa utetezi wa mdomo dhidi ya tuhuma zinazowakabili ambapo walijitetea na Zuchu kuomba radhi kwa kuwa inawezekana katika matamshi yake hakufungua mdomo wake vizuri au kwa lafudhi yake ya Kizanzibari alitamka neno 'Mtambo' vibaya na kusababisha tafsiri yenye utata na iliyomaanisha matusi.

Aidha, ameeleza kuwa tathimini ya kamati baada ya kusikiliza maelezo yote ya Wasafi TV Company Limited na kukiri kutangaza maudhui hayo kamati imetoa onyo kali kwa kampuni hiyo na kuwataka kuomba radhi watazamaji na Umma kwa ujumla kupitia kituo chao cha televisheni cha Wasafi na chaneli yao ya mtandaoni waliyotumia kurusha maudhui hayo kwa siku taatu mfululizo kuanzia 15/01/2022 hadi 17/01/2022.

Kuhusu Aaliyah, Ndalahwa amesema mtangazaji huyo na kipindi cha Refresh watawekwa chini ya uangalizi maalumu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa miezi mitatu kuanzia tarehe ya kusomwa uamuzi huo na kueleza kuwa haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwenye Baraza la Ushindani wa Haki za Kibiashara iko wazi ndani ya siku 21 kuanzia siku kusomwa kwa uamuzi huo.

Vilevile amevitaka vyombo vya habari kote nchini kuzingatia kanuni, maadili na weledi katika kutoa maudhui yasiyo na utata katika jamii.



Mkutano ukiendelea.
Wajumbe wa kamati ya maudhui wa TCRA wakisaini nakala za uamuzi huo.
Mkurugenzi wa kamati ya maudhui ya TCRA Ndalahwa Gunze (kushoto,) akimkabidhi nakala ya uamuzi huo Mkurugenzi wa maudhui wa kampuni ya Wasafi TV Spencer Lameck.






Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2