WAZAZI PELEKENI WATOTO SHULE, WALIMU TUPO TAYARI KUWAFUNDISHA- MWENYEKITI CWT MOROGORO | Tarimo Blog



Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT,) Mkoa wa Morogoro Mwl. Jumanne Nyakirang'ani.



IKIWA zimesalia siku chache kabla ya kufunguliwa kwa shule za Msingi na sekondari kote nchini walimu wamewataka wazazi kuwapeleka watoto shuleni kwa kuwa walimu wapo tayari kuwafundisha na kubwa zaidi ni uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ambao Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha madarasa ya kutosha yanajengwa kila shule.

Hayo yameelezwa leo na Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT,) Mkoa wa Morogoro Mwl. Jumanne Nyakirang'ani jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa mazingira yametengenezwa, madarasa ni mazuri na hakuna jambo la kuwarudisha nyuma wazazi na kushindwa kuwapeleka watoto shuleni.

Nyakirang'ani amewapongeza walimu kwa kuendelea kujenga taifa kwa kutoa elimu chini ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo inafanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo hasa katika sekta ya elimu.

''Rais wetu anafanya kazi kubwa sana, tunampongeza sana kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu...kwa sasa amejenga madarasa nchi nzima ambapo walimu tutafanya kazi katika mazingira mazuri ya kuwafundisha wanafunzi wetu.'' Amesema.

Aidha amesema kuwa Rais amekuwa akishirikiana na walimu kupitia Chama cha Walimu Tanzania, jambo linalowapa faraja zaidi.

''Tunachohitaji katika chama chetu na walimu kwa ujumla ni utulivu uliopo na tuipe Serikali ushirikiano mkubwa ili iweze kuendelea kutuhudumia kupitia chama chetu cha Walimu...Walimu tushirikiane katika kutoa huduma hii muhimu ya elimu kwa kizazi hiki na tujiepushe na makundi yanayojitokeza na kuongea mambo yasiyofaa yanayoweza kuleta taharuki na tupotezea taarifa zinazochapishwa katika mitandao ya kijamii zinazoleta taharuki na kukosesha amani ya kufanya kazi.'' Amesema.

Amesema Chama cha Walimu kipo bega kwa bega na wanachama wake wote katika kuwahudumia na kwa mwaka huu wa 2022 kitatoa mafunzo kwa wanachama  wote baada ya kutoa mafunzo hayo kwa viongozi wa chama hicho mwaka uliopita.




Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2