BUNGE LARIDHIA NYONGEZA YA SHILINGI TRILIONI 1.3 YA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2021/22 | Tarimo Blog

Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba akiwasilisha mapendekezo ya nyongeza ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22 Bungeni Jijini Dodoma.



Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kushoto) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hasan Chande (Mb), wakifuatilia shughuli za Bunge Jijini Dodoma.

………………………

Na. Ramadhani Kissimba na Saidina Msangi, WFM, Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia Serikali kuongeza matumizi ya zaidi ya shilingi trilioni 1.3 Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 na kuifanya Bajeti hiyo kuongezeka kutoka sh. trilioni 36.66 hadi kufikia sh. trilioni 37.98.

Akiwasilisha mapendekezo ya nyongeza ya bajeti kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba(Mb), Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe. Mhandisi Hamad Yusuff Masauni alisema kuwa Serikali ilipata Mkopo usio na riba kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wenye thamani ya shilingi trilioni 1.3 sawa na dola za Marekani milioni 567.3.

Mh. Masauni alisema kuwa fedha hizo zilizopatikana hazikuwa sehemu ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge katika mwaka 2021/22 hivyo Serikali inawajibika chini ya kifungu cha 43 cha Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Ibara ya 137 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwasilisha bungeni mapendekezo ya kuomba ridhaa ya Bunge kutumia fedha za mkopo huo.

Aliongeza kuwa fedha hizo zitatumika kuwakinga Watanzania dhidi ya maambukizi ya UVIKO-19 na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii zilioathirika na ugonjwa huo kwa upande wa Tanzania Bara na Visiwani.

‘Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 1,079.6 ni kwa ajili ya Tanzania Bara, sawa na dola za Marekani milioni 467.3 na shilingi bilioni 231.0, sawa na dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar’ alisema Mh. Masauni.

Mhe.Masauni aliongeza kuwa mchakato wa kupata mkopo huo ulihusisha sekta mbalimbali ambapo baadhi ya sekta hazikukidhi kujumuishwa kwenye mgao wa fedha hizo kwa mujibu wa vigezo na masharti ya IMF. Aliongeza kuwa sekta zilizokidhi vigezo hivyo ni afya, elimu, utalii, maji, biashara ndogo ndogo kupitia makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye ulemavu na kaya maskini kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii (TASAF).

Alifafanua kuwa matumizi ya fedha hizo yamegawanywa kulingana na vipaumbele ilivyojiwekea Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22 ambapo sekta ya afya ilipata shilingi bilioni 466.9, sekta ya elimu shilingi bilioni 368.9, sekta ya maji shilingi bilioni 139.4,sekta ya utalii shilingi bilioni 90.2, TASAF shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya kuwezesha kaya masikini 34,375 na eneo lingine lililopatiwa fedha ni makundi maalum ambao wamepatiwa shilingi bilioni 5, pamoja na timu ya uratibu, ufuatiliaji na tathmini waliopewa shilingi bilioni 3.7.

Aliwahakikishia Wabunge kuwa fedha hizo zitatumika na kusimamiwa kikamilifu na Serikali na kumtaka Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kufatilia matumizi ya fedha hizo ili kuzuia ubadhilifu wakati wa utekelezaji wa miradi ilianishwa kutekelezwa kwa kutumia fedha hizo.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2