Adeladius Makwega, DODOMA
Wakaguru ni miongoni mwa makabila ambayo yanachukua ukoo kwa mama, lipo upande wa nusu ya kaskazini mwa Mpwapwa (sasa imegawanya na kuwa sehemu ya Wilaya ya Kongwa), sehemu ya Wilaya ya Kilosa na sehemu ya mashariki ya kati ya Dodoma.
Wakaguru wanauganika katika koo kubwa zaidi ya 100 zinazojikita katika kundi la Wabantu.
Koo hizo mia moja zinaitwa MAKUNGUGO (wingi) na IKUNGUGO (umoja), huku kila ukoo ulikuwa na utawala wake, shughuli yake ya msingi kama ni kilimo au ufugaji huku Chifu ndiye alikuwa msimamizi wa namna ya kugawanya ardhi yenye rutuba. Ndiyo kusema koo zote mia moja kila ukoo ulikuwa na eneo lake la kuishi na ardhi yake.
Mpaka mwaka 1957 kabila hili lilikadiliwa kuwa na watu 86,936 huku majirani zao Wagulu walikuwa 57,877, Wasagara 31,609 na kulingana na takwimu hizo za mwaka huo wa 57 katika eneo la KIlosa asilimia 33.3 walikuwa Wakaguru na 25.9 ya watu wote wa Mpwapwa (Kongwa ya sasa ) walikuwa pia Wakaguru.
Kwa takwimu hizo ndiyo kusema Wakaguru wengi walikuwa katika Wilaya ya Kilosa zaidi ya maeneo mengine kama vile Wilaya ya Mpwapwa. Hata hayo makao makuu ya Chifu wa Ukaguru yalikuwa Mamboya Wilayani Kilosa.
Swali la kujiuliza je ilikuwaje Wakaguru hao wakaweka makaazi yao katika eneo hilo? Kulijibu swali hilo Ndugu D.Z Mwaga mtaftiti wa kabila hili katika maandishi yake juu ya Utani wa Wakagauru anabainisha kuwa Wakaguru eneo lao la asili si Kilosa wala Mpwapwa bali walitokea huko Wilayani Kondoa.
“Kiongozi mmoja wa Wakaguru ambaye alikuwa na nguvu ndiye alisababisha wao kuhamia Uheheni-Iringa. Kutokana na mazingira yao kuwa magumu Uheheni haswa kushindwa vita, Wakaguru walikimbilia huko Mpwapwa na Kilosa.”
Wahehe waliweza kuwafurusha Wakaguru wakakimbili upande wa Magharibi huko Chibwepanduka wakipita katika mawe na milima kadhaa wakafika eneo la Rubi ambapo ni eneo la Mpwapwa na kuelekea kaskazini hadi Mamboya huko KIlosa.
Japokuwa habari hii inasimuliwa katika simulizi za mdomo huku kukiwa na ushahidi kiduchu. Miongoni mwa ushahidi wa safari hiyo kutoka Kondoa kwenda uheheni na uheheni hadi Mamboya ni kuwepo kwa majina kadhaa ya maeneo hayo waliyopita katika safari yao kila pahala wanapoishi Wakaguru hawa.
Inaaminika kuwa binadamu anapofika ugenini kuanza maisha mapya, huwa akilini mwake hukumbuka majina ya pahala alipokuwepo mwanzo, hata watu waliokimbia mafuriko, vita au janga lolote wanapofika eneo geni hutumia majina yao ya walikotoka kuyabatiza maeneo mageni waliopo kwa wakati huo. Hata kama njiani katika safari hiyo watu hufariki au kupotea wale wanaojaliwa kufika mwisho hujikusanya kulingana na eneo lao la awali.Kama inashindikana hilo ndipo hutumiwa alama mbalimbali.
Kuhusi hili majina kama Lulenga na mengineyo yanatajwa.
Maisha ya Wakaguru katika Wilaya ya Kilosa, Kongwa na Mpwapwa inasadikiwa yalianza wakati wa karne ya 17 na 18 muda mfupi kabla ya Waarabu hawajaanza kupita na misafara yao ya biashara ya bara na pwani.
Waarabu walipoanza kupita katika eneo hilo la Ukaguru wanamtaja Chifu Chimola kuwa ndiye aliyekuwa kiongozi wa kabila hilo wakati huo.
Ili msomaji wangu kuwafahamu zaidi Wakaguru na eneo lao wanaloishi naomba nilitazama jambo moja zaidi ili kukupa picha yao haswa kwa swali hili, Je, Wakaguru ni kabila la namna gani?
Wakaguru kuna wakati mwingine wanafahamika kama WAITUMBA (WATUMBA)na WAMEGI.
ITUMBA ni aina ya mti unastawi sana upande wa kusini mwa milima ya Ukaguru .eneo wanaloishi Wakaguru. Ndugu hawa walijenga nyumba zao chini ya miti hiyo ndiyo maana walifahamika kama WEITUMBA na mlima hiyo jirani nao uliitwa ITUMBA. Katika eneo hilo ndipo wale mababu na mababu wa Wakaguru wamezikwa huko.
Lakini kuna kundi lengine la Wakaguru walioshuka kutoka katika milima hiyo na wakaweka makazi yao jirani na vyanzo vya maji katika kingo zake, hawa wanafahamika kama WAMEGI, megi maana yake ni maji kwa kuwa waliishi kando na vyanzo vya maji.
Kumbuka mwanakwetu hapo awali nilikujulisha hapo juu ya matumizi ya alama ndiyo maana majina hayo WEITUMBA na WAMEJI yanaibuka.
Mwanakwetu hao ndiyo WAKAGURU/WAITUMBA/WEITUMBA/WAMEGI, naweka kalamu yangu chini hapo. Nakuuma sikio mwanakwetu kuwa katika matini yangu ijayo nitatazama utani wa Wakaguru na makabila mengine ikiwamo na Wamasai, ndani ya utani huo wa Wakaguru na Wamasai kuna mambo, nasema kuna mambo, utafurahi.
Nakutakia siku njema.
0717649257
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment