TANESCO Manyara kupita kijiji kwa kijiji kutoa ufafanuzi gharama za umeme vijijini. | Tarimo Blog


Na John Walter-Manyara


Katika kuhakikisha wananchi wanapata uelewa juu ya gharama mpya za kuunganisha umeme maeneo ya mijini na vijijini, shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Manyara limeanza kuwatembelea wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ambapo wananchi wanapata nafasi ya kuuliza maswali na kupatiwa ufafanuzi.


Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bashnet tarafa ya Bashnet wilaya ya Babati, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Manyara Mhandisi Fadhili Kalisa amesema kwa sasa kwa vijijini kuna mafungu matatu ya wateja ambapo aina ya kwanza ni mteja aliepo umbali wa mita 30 (Chuma),pili ni wale waliopo zaidi ya mita 30 lakini haizidi 70 (nguzo moja) huku fungu lingine likiwa ni wale waliozidi mita 70 lakini hawazidi mita 120 (nguzo mbili). 


Mhandisi Kalisa amesema katika kutembelea maeneo ya kata, katika baraza la madiwani wamekubaliana kushirikiana kwa pamoja na madiwani hao wanapofika katika vijiji ili kutambua maeneo yenye uhitaji.


Aidha Kalisa amesema watatoa kipaumbele kufikisha huduma ya umeme kwenye Zahanati, Shule, Misikiti, Makanisa,Visima vya maji na kadhalika.
Kuhusu gharama mpya za umeme zilizotangazwa Januari 5,2022, Mhandisi Fadhili Kalisa amesema kwa upande wa Vjijini ni shilingi 27,000 na kwa mjini gharama zinaanzia shilingi 320,960 kwa kutegemea umbali toka unapochukulia umeme na idadi ya nguzo. 


Amesema shirika hilo katika mkoa wa Manyara litaendelea kuwahudumia wananchi kama taratibu zao zinavyoelekeza ili kila mmoja afurahie huduma za Umeme.


Kwa upande mwingine amewatadharisha wananchi na vishoka wanaofika kuwarubuni kuwa gharama za kuunganisha umeme ni shilingi elfu 27,000 pekee wasikubali kuib
iwa na kwamba .


Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Bashnet Peter Joseph na Galgano Lucas wameishukuru TANESCO kwa kuwatembelea wakieleza wamejifunza mambo mengi ambayo walikua hawajui kuhusu shirika hilo na huduma zake.


Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Bashnet John Sulle amempongeza meneja wa TANESCO Mhandisi Fadhili Kalisa na watumishi wa shirika hilo kwa kutenga muda wa kuwatembelea wananchi kwani hatua hiyo itawapunguzia maswali mengi yaliyokuwa yanaulizwa na wananchi hao kuhusu bei mpya za kuunganisha umeme.




 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2