MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango anatarajia kuongoza nchi 10 wanachama wa ushirikiano wa mpito wa bonde la MTO Nile (Nile Basin Initiative,) katika maadhimisho ya 16 ya bonde la Mto Nile yatakayofanyika Februari 22 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi. Anthony Sanga amesema maadhimisho hayo yanakwenda na kauli mbiu ya "Urithi Wetu kwa Amani na Ustawi" ujumbe unaolenga kuzikumbusha nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile umuhimu wa ushirikiano katika usimamizi, uendelezaji na matumizi ya Maji ya Mto Nile kwa kudumisha amani na ustawi wa nchi wanachama na wananchi wake.
Ameeleza kuwa maadhimisho hayo yatawakukutanisha washirika 1500 kutoka nchi mbalimbali duniani wakiwemo wajumbe wa baraza la mawaziri wa nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile, mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mabalozi, Wadau wa Maendeleo, taasisi za Serikali na sekta binafsi.
"Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Bonde la Mto Nile wameandaa maadhimisho haya kupitia mkutano wa 29 wa Baraza la mawaziri wa nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile uliofanyika Novemba 26 mwaka jana Juba, Nchini Sudan ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilichaguliwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho kwa mara ya pili." Amesema.
Mhandisi. Sanga amesema Mto Nile wenye urefu wa Kilomita 6,695 ukishikilia nafasi ya kwanza kwa kuwa Mto mrefu zaidi duniani chanzo chake ni Ziwa Victoria na umekuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kupitia matumizi ya maji yake katika sekta za kilimo, umwagiliaji, uzalishaji umeme, usafirishaji na matumizi ya nyumbani.
Maadhimisho hayo yataanza saa moja na nusu asubuhi kwa maandamano maalumu yakiongozwa na bendi ya Polisi kutoka hosteli za Hayati Magufuli chuo kikuu Dar es Salaam na kupokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango katika ukumbi wa Mlimani City.
Ushirikiano wa mpito wa bonde la Mto Nile unajumuisha Nchi kumi wanachama ambazo ni Tanzania, Burundi, Ethiopia, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini na Uganda na ulianzishwa Februari 22, 1999 jijini Dar es Salaam Tanzania kwa malengo ya kusimamia, kuendeleza na kuratibu matumizi ya rasilimali za maji za Bonde la Mto Nile.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia yaliokuwa yakijiri ndani ya mkutano huo
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment