AFUGWA JELA MIAKA 30 KWA KOSA LA KUPATIKANA NA MICHE YA BHANGI. | Tarimo Blog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa ANOSISYE AMOS MWAKITEGA [60] Mkazi wa Kyimo halmashauri ya Rungwe Mkoa wa Mbeya kwa kosa la kupatikana na miche ya bhangi 192 kinyume na kifungu cha sheria namba 11 (1) (a) cha sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya 2019.
Mtuhumiwa alikamatwa Machi 10, 2022 huko Kyimo halmashauri ya Wilaya ya Rungwe na kufikishwa mahakama ya Wilaya ya Rungwe ambapo alisomewa mashitaka matatu, 1. Kulima miche ya bhangi 192 kinyume na kifungu namba 11 (1) (a) cha sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kelevya ya mwaka 2019, 2. Kupatikana na bhangi gramu 410 na 3. Kupatikana na bhangi gramu 12.3 kinyume na kifungu namba 17 (1) (a) na (b) ya mwaka 2019 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2021.
Mnamo Machi 15, 2022 mtuhumiwa alipatikana na hatia kwa makosa yote matatu na kuhukumiwa kifungo jela miaka thelathini [30].
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anatoa rai kwa wananchi kuacha kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na badala yake watafute shughuli nyingine halali zitakazowapatia kipato halali. Aidha Kamanda MATEI anawataka wananchi kuacha mara moja matumizi ya dawa za kulevya kwani ni kinyume cha sheria n ani hatari kwa afya zao na watakapo kamatwa na kufikishwa mahakamani watafugwa.
KUKAMATWA MTUHUMIWA WA WIZI WA PIKIPIKI.
Mnamo tarehe 15.03.2022 majira ya saa 12:00 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Kijiji cha Mpakani kilichopo Kata ya Ubaruku, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata ALEX MWAPAMBA [19] Mkazi wa Igamba – Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe akiwa na mali ya wizi Pikipiki aina ya Kinglion yenye namba za usajili MC.451 CXY, Engine Na. KL162FMJ10540582, Chasis Na. LZ15L15P902MHE40582.
Mtuhumiwa amehojiwa na kukiri kuiba Pikipiki hiyo nyumbani kwa ASHURA MWALEMBA [43] Mkazi wa Mpakani – Ubaruku na kisha kutoroka na Pikipiki. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Imetolewa na:
[ULRICH O. MATEI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment