TUME YA USHINDANI KUCHUNGUZA KUPANDA BEI YA BIDHAA | Tarimo Blog




NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Ushindani nchini (FCC) William Erio,amesema wameanza kuchukua hatua kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa na vifaa mbalimbali vya ujenzi kunakofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Tume hiyo pia imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anazofanya kitaifa na kimataifa kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanapatikana ikiwemo kuvutia wawekezaji ndani ya kipindi cha mwaka mmoja madarakani.

Kauli hiyo ilitolewa na Erio wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza,kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani ambayo huadhimishwa Machi 15,kila mwaka pamoja na mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kupitia taasisi hiyo.

Alisema FCC inachunguza ongezeko la bei kwenye bidhaa na vifaa vya sekta ya ujenzi,kuona kama kupanda kwake kumesababishwa na gharama za uzalishaji au wafanyabiashara kutaka kujipatia faida kubwa bila kuzingatia kipato cha mwananchi.

Mkurugenzi mkuu huyo wa FCC alisema ongezeko la bei kwenye biashara ni kitu cha kawaida kinachoweza kutokana na sababu za ndani au za nje ya nchi zilizo nje ya uwezo wetu zinazotokea nchini.

“Katika biashara ongezeko la bei ni jambo la kawaida,pia ongezeko lisilosababishwa na mahitaji sasa FCC tunafanya nini katika kudhibiti hilo, tunaangalia bidhaa kwa nini zimepanda kama kuna dalili za uvunjifu wa sheria kwa wafanyabiashara kutaka kujipatia faida kubwa,hatua za zitachukuliwa,”alisema.

Erio alisema siku zote wafanyabiashara wanalenga faida kubwa iwe kwa njia halali au isiyo halali,na kusistiza taasisi hiyo inachunguza na kupitia nyaraka mbalimbali zinazohusiana na bidhaa zinazolalamikiwa kupandishwa bei bila kuzingatia sheria na kuchukua hatua baada ya uchunguzi huo.

Aidha kuhusu mafanikio ya serikali ya awamu ya sita, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Rais Samia aingie madarakani, uwekezaji nchini umeimarika ambapo FCC imepokea maombi 83 ya uwekezaji katika sekta mbalimbali kulinganisha na maombi 54 mwaka mmoja kabla hajaingia madarakani.

“Tumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayofanya kitaifa na kimataifa kuhakikisha maendeleo yanapatikana,katika kuhimiza uwekezaji kukuza uchumi na ushindani shirikishi lakini pia uamuzi wa kuruhusu chanjo ya Covid-19 umefungua milango kwa wageni kuja kuwekeza na kufanya biashara nchini,”alisema.

Erio alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita imeonyesha fursa za kuvutia wawekezaji ambazo FCC inaona zilivyoimarika ambapo kati ya maombi hayo 83, yamo ya sekta ya madini 18,kilimo 4,benki 10,nishati na petrol 6, afya 3, bima 4,uzalishaji 12,mawasilino na simu 11, utalii 2 na sekta mtambuka 11.

Alieleza kuwa ili kuwalinda watumiaji wamefanya kaguzi kwenye kanda tano, mikoa 10 na taasisi 151,kuona namna gani mlaji analindwa kutokana na mikataba, isipoangaliwa inaweza kumwuumiza mlaji,lazima masharti na vigezo vizingatiwe vikiwa kwenye lugha inayoeleweka kwa wananchi.

Pia mkurugenzi mkuu huyo wa FCC alitumia fursa hiyo kuwaonya wafanyabishara wa vyakula wasitumie ibada ya mfungo wa Ramadhani itakayoanza karibuni kuacha kujinufaisha kwa kuficha bidhaa na kupandisha bei ya vyakula mbalimbali vikiwemo mafuta ya kula na sukari,hivyo waachwe wafanye ibada hiyo bila vikwazo.

“Tabia ya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa kwa kipindi cha msimu wa sikukuu hasa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kama atafanya au watafanya hivyo itakuwa ni kuvunja sheria, FCC itachukua hatua,”alisema Erio

Akizungumzia kilele cha Siku ya Haki ya Mtuhumiaji Duniani,yenye kauli mbiu ya Kumlinda Mlaji katika Huduma za Fedha Kidijitali,alisema kitaifa maadhimisho yatafanyika jijini Mwanza Machi 15,ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Biashara na Uwekezaji, Dkt. Ashatu Kijaji.

Alisema kuwa yanalenga kutoa elimu kwa wananchi wapate ufahamu wa haki zao na kuhakikisha zinakuwepo, pia haki hizo za huduma za mtumiaji kidijitali ni muhimu katika kukuza uchumi.


Alifafanua kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia huduma nyingi duniani zinafanyika kidijitali zikiwemo za kifedha,huduma za luku,kulipa tozo, matumizi Ankara za maji na kodi za serikali,mikopo na bima, kuuza na kununua bidhaa.

“Huduma nyingi duniani zinafanyika kidijitali na ipo hatari ya mtumiaji kukutana na wezi,hivyo ni eneo tunaloliangalia katika kupata huduma huku mtumiaji akichukua tahadhari,hadi mwaka 2024 watu bilioni 3.6 duniani watakuwa wanapata huduma za fedha kidijitali sawa na nusu ya watu bilioni 7.2,hivyo Tanzania si kisiwa tutakuwa katika matumizi hayo,”alisema. Kwa mujibu wa Erio mwaka 2017 asilimia 70 ya watu wenye akaunti benki walikuwa wakifanya shughuli zao kidijitali ambapo asilimia 39 ya kampuni zinatumia teknolojia ya Fintec na kuwataka wazalishaji wa bidhaa na watoa huduma kuzingatia haki na huduma zinakuwa zenye ubora.


Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani nchini (FCC),William Erio, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jana kuhusiana na kilele cha maadhimisho ya Siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani hapo Machi 15, mwaka huu, jijini Mwanza.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2