Na Jane Edward, Arusha
Wananchi wa kata ya Olmoti Wilayani Arumeru Mkoani Arusha wamepatiwa elimu ya utunzaji wa mazingira ikiwa pamoja na kuotesha miti katika maeneo yao ikiwa ni kupambana na ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Hayo yamebainishwa na mratibu wa zoezi la utoaji elimu ya upandaji miti na mazingira kutoka Club ya utunzaji mazingira (Lions club) Chief Masanya Kabena wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kwa Wananchi wa vijiji vya kata hiyo.
Amesema maeneo mengi ya jamii ya wafugaji ni maeneo makame ambayo hayana miti ya kutosha kutokana na miti hiyo kuliwa na mifugo hali inayosababisha kuwepo na changamoto ya upepo mkali unaoezua nyumba za wananchi hao .
"ukiangalia hata nyumba nyingi zinazoezuliwa paa katika maeneo mbalimbali utagundua ni kwa sababu hakuna miti,"Alisema
Kwa upande wa wananchi hao Meishili Kivuyo anasema wao kama wajumbe wa serikali ya mtaa wanaahidi kuwa watunzaji wazuri wa miti hiyo kwa kuwa changamoto ya kuezuliwa nyumba ni kubwa.
Vilevile watahakikisha wanawekeana sheria za kuhakikisha anayeachia mifugo ikala miti hiyo anatozwa kiasi cha shilingi elfu hamsini na hivyo kuwataka wananchi wenzake kuwa walinzi.
Naye afisa mazingira kutoka Club hiyo ya mazingira Lions Club Evah Benson anasema uhitaji wa miti katika maeneo ya vijiji ni mkubwa na kwamba watahakikisha wanaendelea kupanda miti na kutunza mazingira.
Hata hivyo miti takribani laki moja inatarajiwa kupandwa kwa nchi nzima ambapo kwa Mkoa wa Arusha miti zaidi ya elfu mbili imeshapandwa.
Vijana wa kata ya Olmoti wakiongoza zoezi la upandaji miti.
Meya wa Jiji la Arusha wa pili kushoto Maximilian Iraghe akitoa maelekezo kwa wadau wa mazingira.
Afisa mazingira wa Lions club akimkabidhi kaimu mganga mkuu wa jiji mti kwaajili ya kupanda mti huo.
Meya wa jiji la Arusha Maximilian Iraghe akipanda mti katika hospital ya wilaya ya Arusha
Picha ya pamoja wadau wa mazingira.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment