MADIWANI SIMANJIRO WATAKA SHAMBA LA MARO LIPIMWE | Tarimo Blog


Na Mwandishi wetu, Simanjiro


BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, limemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Samwel Warioba kupima maeneo ya shamba la Maro na eneo la wazi lMji mdogo wa Mirerani baada ya mgogoro kukamilika.

Upimaji huo unatakiwa kufanyika ili kupata maeneo ya kujenga kituo cha afya cha Kata ya Mirerani na shule nyingine ya msingi kwenye kata hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Baraka Kanunga ameyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mji mdogo wa Orkesumet.

Kanunga amesema kwa hivi sasa hawawezi kuingilia mamlaka ya mkuu wa wilaya hiyo Dk Suleiman Serera ambaye hivi sasa anashughulikia mgogoro wa shamba la Maro kwa kuagiza polisi na TAKUKURU wachunguze.

"Mkurugenzi mtendaji kupitia timu yake ya idara ya ardhi wakapime eneo hilo mara baada ya mgogoro uliopo pale unaoshuhulikiwa na mkuu wa wilaya kumalizika," amesema Kanunga.

Diwani wa kata ya Mirerani Salome Mnyawi amesema mgogoro wa shamba hilo la Maro unasababisha kuzorotesha shughuli za maendeleo ya kata hiyo.

Mnyawi amesema wameshindwa kuanza kujenga kituo cha afya cha kata ya Mirerani na shule mpya ya msingi ili kupunguza mrundikano kutokana na ukosefu wa eneo.

Amesema ataendelea kupigania eneo hilo kwani baadhi ya wanasiasa walikuwa wanauza ardhi ya eneo hilo na yeye akipinga anapata upinzani ila atasimama na wananchi.

"Mkuu wetu wa wilaya Dk Serera ninampongeza sana kwa kuingilia kati mgogoro wa shamba la Maro, kwani kuna baadhi ya viongozi walikuwa wanauza maeneo ya wazi kama shamba la bibi," amesema Mnyawi.

Amesema kuna eneo la wazi linadaiwa kuwa ni la kigogo wa kisiasa kwenye shamba la Maro ila linaendelea kuuzwa na wenye uchu wa ardhi bila kuangalia maslahi ya wananchi.


 
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2