Shirika la ndege linaloongoza Tanzania, Precision Air ndio msafirishaji rasmi wa maonyesho ya utalii ya kimataifa yanayoitwa ‘KARIBU-KILIFAIR 2022’, ambayo yatafanyika Arusha kuanzia Juni 3 hadi 5.
Maonyesho haya ambayo yatafanyika kwa mara ya kwanza baada ya kusitishwa kwa miaka miwili kutokana na janga la Uviko-19, yanategemea kuvutia washiriki kutoka Afrika mashariki na wanunuaji kutoka masoko ya kimataifa.
Akizungumzia ufadhili huo, Meneja masoko na mawasiliano wa Precision Air, Bw. Hilary Mremi alisema, Precision Air inajivunia kuwa sehemu ya maonyesho hayo ambayo yatakuza utalii nchini Tanzania.
“Tunafurahi kwa mara nyingine tena kuwa sehemu ya maonyesho haya muhimu kwa ajili ya utalii wetu, sisi kama wadau wakubwa wa utalii nchini tunawajibika kuunga mkono matukio ya aina hii. Tunaamini kupitia ufadhili huu kwa KARIBU-KILIFAIR tutakuwa tunamuunga mkono Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuitangaza nchi yetu duniani” aliongeza.
KARIBU-KILIFAIR ni muunganiko wa maonyesho mawili ambayo ni KARIBU FAIR na KILIFAIR, maonyesho haya yamevuta zaidi ya washiriki 450 kutoka Afrika mashariki, wanunuzi 600 kutoka duniani kote na zaidi ya wahudhuriaji 7000 ndani ya siku tatu. Mwaka huu maonyesho haya yatafanyika katika viwanja vya Magereza mkabala na kiwanja cha ndege cha Arusha kuanzia Juni 3 hadi 5, 2022.
Akizungumzia udhamini huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro Promotion Bw. Dominic Shoo alisema,”Tukio hili linalenga kujenga biashara na kufanya wadau wa utalii kukutana baada ya changamoto ya muda mrefu ya Uviko-19. Tukio la mwaka huu limevuta hisia kubwa kutoka kwa wadau jambo ambalo linaonyesha kuwa watu wana hamu ya kukuza biashara zao zaidi ya hapo awali.
Akifafanua zaidi, “Tunawashukuru sana Precision Air kwa msaada wao. Kupitia ushirikiano wao, tukio letu limekuwa na mafanikio kila mwaka”.
Precision Air ni kampuni ya ndege ya Kitanzania inayofanya safari zake kutoka makao yake makuu Dar es salaam kwenda Arusha, Bukoba, Dodoma, Kahama, Kilimanjaro, Mbeya, Mtwara, Tabora, Mwanza, Seronera(Serengeti), Zanzibar na Nairobi.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment