-Waajiri Waaswa Kuepuka Rushwa Wakati wa Zoezi
Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia Watumishi wa Serikali walioondolewa kazini kwa sababu ya kughushi vyeti kurudishiwa michango yao waliyochangia katika Mifuko ya Hifadhi za Jamii ambapo katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ni asilimia 5 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ni asilimia 10 ya mshahara wa mhusika na haitahusisha malipo mengine yoyote ya ziada.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma.
“Marejesho ya michango ya watumishi hao yataanza kufanyika kuanzia Novemba 1, 2022 na tungependa jambo hili likamilike ndani ya muda mfupi, ili kuwezesha malipo hayo kufanyika mtumishi husika atatakiwa kwenda kwa mwajiri na nyaraka za kibenki za akaunti iliyo hai, picha mbili, nakala ya Kitambulisho cha Taifa, Mpiga Kura au Leseni ya Udereva pamoja na kujaza na kusaini hati ya aliyekuwa mwajiri wake” Amefafanua Prof. Ndalichako.
Prof. Ndalichako ameongeza kuwa, “waajiri watawajibika kuwasilisha kwenye Mifuko hati za ridhaa pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu ulipaji wa mafao kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya Mifuko hiyo ya Hifadhi za Jamii ili malipo yafanyike kupitia akaunti za benki”.
Prof. Ndalichako amewataka watumishi wote walioondolewa kazini baada ya kugundulika kuwa na vyeti vya kughushi kukamilisha taratibu zinazotakiwa ili Mifuko iweze kukamilisha taratibu za kuwarejeshea michango yao.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama, amesema kuwa Rais Samia amefanya maauzi magumu na ameonesha moyo wa utashi na huruma kwa watumishi hao na hivyo kumshukuru kwa uamuzi huo wa busara.
“Navishukuru sana Vyama vya Wafanyakazi, kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) wamekuwa wakija sana ofisini pamoja na watumishi wenyewe wamekuwa wakiandika sana barua kwetu hata kwa Rais Samia kumuomba aone na afikirie jambo hili kwa wafanyakazi kwa hiyo tunawashukuru,” amesema Waziri Jenista.
Waziri Jenista ameeleza kuwa Ofisi yake ipo tayari kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa suala hilo linatekelezeka kwa mafanikio na kutoa maagizo, “Ofisi yangu inawaagiza waajiri wote ambao wanasimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mamlaka za Serikali Kuu, Taasisi za Umma na Wakala mbalimbali hapa nchini kuwajibika ipasavyo na kutoa ushirikiano kwa watumishi hao wanaohusika ili waweze kukamilisha na kuwasilisha nyaraka zinazotakiwa kufanikisha kwa watumishi kurudishiwa michango yao.”
Sambamba na hilo, Waziri Jenista, amewataka waajiri wote katika Sekta ya Umma kuhakikisha wanaandaa dawati maalum litakalotoa msaada wa haraka ili kufanikisha zoezi hilo kwa urahisi kwa kuwapokea na kuwasaidia watumishi husika pindi wanapofika katika ofisi zao.
“Waajiri wote wahakikishe wanazingatia misingi ya utawala bora ikiwa ni pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa zoezi hili. Tunaamini Waajiri watalifanya zoezi hili kwa ufanisi, weledi na uadilifu kwa kuzingatia Maadili ya Utumishi wa Umma nchini. Pia niwaagize wenzetu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuanzia sasa wahakikishe wanatumia kila mbinu mkakati kuzuia kitendo au kiashiria chochote cha rushwa katika kufanikisha azma,” amehitimisha Waziri Jenista.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment