Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma ya Hali ya Hewa Dkt. Hamza Kabelwa akitoa mwelekeo wa Mvua za Msimu (Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023) jijini Dar es Salaam.
MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imesema mikoa 14 inayopata msimu mmoja wa mvua inatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani kuanzia mwezi Novemba 2022 na kati ya mwezi Aprili mwaka 2023.
Pia hali ya sasa ya joto la bahari la chini ya wastani katika eneo la kati la Bahari ya Pasifiki inatarajiwa kuendelea kuwa chini ya wastani (La Nina) katika nusu ya kwanza ya msimu ingawa joto linatarajiwa kuongezeka kidogo hasa katika nusu ya pili ya msimu.
Mkurugenzi wa Utabiri wa TMA, Dkt. Hamza Kabelwa amesema hayo leo Oktoba 26, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka.
Ameitaja mikoa inayotarajiwa kupata mvua hizo ni Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodima, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na kusini mwa Morogoro.
Dkt.Kabelwa amesema katika nusu ya kwanza ya msimu kuanzia Novemba mwaka 2022 hadi Januari mwaka 2023 vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza.
"Ongezeko la mvua linatarajiwa katika nusu ya pili ya msimu kuanzia Februari hadi Aprili mwaka 2023 na mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kunyesha Mei mwaka 2023 katika maeneo mengi," alisema Dkt. Kabelwa.
Ameongeza kuwa, licha ya kunyesha mvua za chini ya wastani hadi wastani, pia matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani.
"Pia upo uwezekano wa kutokea kwa migandamizo midogo ya hewa kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi ikiwa ni pamoja na rasi ya Msumbiji, hivyo kusababisha vipindi vya mvua katika nusu ya pili ya msimu".
Dkt. Kabelwa amezitaja athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika kipindi hiki ni pamoja na upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo katika maeneo hayo yanayopata mvua hizo na kuathiri ukuaji wa mazao na upatikanaji wa malisho kwa mifugo na uzalishaji kwa ujumla huku uwezekano wa kujitokeza kwa matukio ya moto kutokana na vipindi virefu vya ukavu.
Pia wakulima wanashauriwa kupanda mazao na mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi na zinazostahimili upungufu wa mvua na kutumia mbinu na teknolojia bora za kilimo himilivu za kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo ikiwa ni pamoja na uvunaji wa maji ya mvua na matumizi ya matandazo.
Amesema athari zingine zinazotarajiwa kujitokeza kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kupungua na kuathiri upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali kama vile umwagiliaji na uzalishaji wa nishati.
Pia Dkt. Kabelwa amezishauri mamlaka kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa pamoja na kuweka miundombinu ya uvunaji maji na kuandaa na kutekeleza mipango mkakati ya kuhimiza kilimo himilivu.
"Hali hii inaweza kuathiri uoteshaji na ukuaji wa mazao hususan katika kipindi cha Novemba na Desemba 2022 kutakuwa na ongezeko la visumbufu vya mazao kama vile mchwa,viwavijeshi ,panya vinatarajiwa kujitokeza katika msimu na kuarhiri mazao ya uzalishaji kwa ujumla pamoja na matukio ya moto yanaweza kujitokeza kutokana na vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa," amesema Dkt. Kabelwa.
Mamlaka zinashauriwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa pamoja na kuweka miundombinu ya uvunaji maji sambamba na kuandaa na kutekeleza mipango mkakati ya kuhimiza kilimo himilivu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment