BILIONI 11 KUSAIDIA MRADI WA KITITA CHA UZAZI SALAMA | Tarimo Blog

 

Na Mwandishi wetu, Haydom.

BENKI ya dunia kupitia kitengo cha Global Financing Facility imetoa zaidi ya sh11 bilioni kupitia mpango wa kitita cha uzazi salama kwa ajili ya kupunguza vifo vya watoto wachanga na wanawake wajawazito kwa asilimia 50.

Mikoa mitano ya Manyara, Tabora, Mwanza, Geita na Shinyanga na itanufaika na mpango huo wenye lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga vifo vya kina mama wakati wa kujifungua.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel ameyasema hayo wakati akizungumzia mradi huo wa kitita cha uzazi salama kwenye hospitali ya rufaa ya Haydom wilayani Mbulu mkoani Manyara.

Dk Mollel amesema jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan zimefanikisha upatikanaji wa fedha hizo ambazo ni ruzuku siyo za mkopo ambazo zitasaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga na vifo vya kina mama kabla na baada ya kujifungua.

“Fedha hizo kutoka benki ya dunia, zitasaidia kutokomeza vifo vya watoto na wanawake wajawazito na hizi ni jitihada za dhati za Rais Samia katika kupambania sekta ya afya ambayo ipo moyoni mwake,” amesema Dk Mollel.

Amesema mradi wa kitita salama wa miaka mitatu una manufaa makubwa nchini kwani matukio ya vifo vya watoto wachanga na wanawake wajawazito vitapungua.

Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Kheri James amesema kupitia mradi huo wa kitita cha uzazi salama, jamii itaondokana na changamoto ya vifo vya watoto na wanawake wajawazito.

“Mradi huu ni mkubwa wenye manufaa kwa watanzania na tumeona tumetembelewa na Naibu Waziri wa maendeleo wa Norway Bjorg Sandkjaer na balozi wa Norway nchini Elizabet Jacobsen,” amesema James.

Naibu Waziri wa maendeleo wa Norway Bjorg Sandkjaer amesema nchi mbili za Tanzania na Norway zitaendelea kushirikiana kwani viongozi na wananchi wana umoja.

“Nimefurahishwa na watanzania kupitia Rais Samia kwa namna mnavyomuunga mkono na yeye anavyokuwa na mashirikiano na nchi mbalimbali hususani nchi ya Norway,” amesema Sandkjaer.

Mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya rufaa ya Haydom, Dk Paschal Mdoe amesema japo kuwa Manyara hakuna idadi kubwa ya vifo vya watoto wachanga, kama Mwanza na Geita ila mradi huo umeleta mafanikio makubwa.

Dk Mdoe amesema watoto wanaozaliwa wafu vifo vya kina mama wakati wa kujifungua hasa kwa sababu ya kutokwa kwa damu nyingi vimepungua kutokana na mradi huo.

Mwanamke mjamzito mkazi wa Haydom, Rose Umbay aliishukuru serikali kwa kufanikisha mradi huo kwani kwa namna moja au nyingine utakuwa na manufaa kwao.












Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2