ILALA YAJA NA MKAKATI WA KAMPENI YA UPANDAJI MITI KUIFANYA DAR KUWA KIJANI | Tarimo Blog

 


Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

MKUU wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Edward Mpogoro amesema katika kuunga mkono kampeni ya kulifanya kuwa la kijani wameweka mikakati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha Wilaya hiyo inakuwa kijani kwa kupanda miti.

Pia amesema kuanzia sasa watahakikisha ramani zote za ujenzi zitatolewa lazima asilimia tano ya eneo liwe kijani kwa maana ya kupanda miti au bustani katika maeneo yao.

Mpogoro ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akifanya mahojiano na chombo kimoja cha habari hapa nchini mara baada ya uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti katika Jiji la Dar es Salaam.

"Ni muhimu kwa kila mtu kupanda miti katika eneo lake ili kuweza kufanya mazingira kuwa mazuri na yakuvutia katika kuhakikisha Jiji linakuwa la kijani.Tumekubaliana na baadhi ya wadau wenye majengo ya viwanda kuanzia uwanja wa ndege mpaka Ikulu kila jengo lazima waboreshe garden yao ya mbele ya majengo yao, watapanda miti ili kuvutia Jiji la Dar es Salaam."

Ameongeza katika kampeni hiyo wamejipanga kupanda miche milioni 1.5 kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)pamoja na wadau wengine mbalimbali wa Ilala katika Jiji la Dar es Salaam.

"Kwenye hii kampeni tutahakikisha tunapanda miche katika shule zote za msingi na sekondari kwa kushirikiana na wadau wetu NMB ambapo wameweka mashindano kwa shule zitakazopanda miche 2000 na kuikuza yote,"amesema.

Pia watahakikisha miche hiyo wanaipanda katika ofisi za kata na mitaa na pia sehemu nyingine ni barabarani ambapo mpaka sasa wanaendelea kuhamasisha wananchi wanapanda miti.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe.Amos Makala akipanda mti aina ya Mkongo kuashiria uzinduzi wa upandaji miti mkoa wa Dar es Salaam,kushoto MKUU wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Edward Mpogoro akishuhudia tukio hilo.
MKUU wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Edward Mpogoro akishiriki zoezi kupanda miti akiunga mkono uzinduzi wa upandaji miti mkoa wa Dar es Salaam.

 Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi kutoka Benki ya NMB,Filbert Mponzi akikabidhi mti aina ya Mgunga kwa Mkuu wa wilaya ya Ilala Mhe.Edward Mpogolo akikabidhiwa,anaeshuhudia pichani kati ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Amos Makala ambaye aliongoza zoezi la uzinduzi wa upandaji miti Kimkoa April 8,2023 katika shule ya Sekondari Tarimo,Wilaya ya Kinondoni,jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Amos Makala akiongoza zoezi la uzinduzi wa upandaji miti Kimkoa. Zoezi hilo lilizinduliwa April 8,2023 shule ya Sekondari Tarimo,Wilaya ya Kinondoni,kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ilala Mhe.Edward Mpogolo na katikati ni Balozi wa Mazingira .
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2