SALAMU ZA PONGEZI ZA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS MSTAAFU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI AKIKABIDHI TUZO YA “VIP GLOBAL WATER CHANGEMAKERS AWARDS” KWA MHE. DKT. HUSSEIN ALI MWINYI, RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, IKULU, ZANZIBAR TAREHE 05 APRILI, 2023 | Tarimo Blog

Mheshimiwa Rais,

Niruhusu nianze kwa kukushukuru kwa dhati kwa kunikaribisha Ikulu – Zanzibar. Nimeshakuja hapa mara kadhaa lakini safari hii nimekuja maalumu kwa ajili ya kukukabidhi Tuzo ijulikanayo kwa jina la “VIP Global Water Changemakers Awards”, yaani Tuzo ya Watu Mashuhuri Wanaoleta Mabadiliko katika Sekta ya Maji Duniani.


Niliipokea Tuzo hii kwa niaba yako Mheshimiwa Rais wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Maji uliofanyika New York, Marekani kuanzia tarehe 22 hadi 24 Machi 2023. Mara tu baada ya kurejea, nilikuomba, na kwa bahati nzuri ukaridhia, nije kukukabidhi mwenyewe Tuzo hii. Hongereni kwa maandalizi mazuri ya hafla hii. Kwa hakika yanaakisi uzito, na kushahabiana na umuhimu, wa Tuzo hii kitaifa na kimataifa.


Mheshimiwa Rais,

Kazi yangu asubuhi ya leo ni ndogo sana; ni kukukabidhi Tuzo yako. Hata hivyo, kabla ya kufanya kazi hiyo, naomba uniruhusu niseme machache kuhusu Tuzo hii kwa ajili ya kusaidia uelewa wa watu waliopo hapa na wananchi wanaofuatilia shughuli hii kupitia vyombo vya habari.


Jambo la kwanza kwamba Tuzo hii ni mpya kabisa na imeandaliwa na kutolewa kwa mara ya kwanza mwaka huu wa 2023 kwa ushirikiano wa pamoja kati ya Benki ya Dunia (WB), Taasisi ya Ubia wa Maji Duniani (GWP) pamoja na Shirika la K – Water la Jamhuri ya Korea, ambalo ni kinara katika kuendeleza sekta ya maji duniani.


Jambo la pili kwamba, Tuzo hii inatolewa kwa makundi mawili.

  • i.)  Kundi la kwanza ni Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali kwa kutambua
    dhamira na mchango wao katika kusimamia na kuendeleza sekta ya maji
    katika nchi zao; na
  • ii.)  Kundi la pili ni Wataalamu wa tasnia ya Maji wanaobuni mbinu na mifumo ya
    kisasa ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya maji katika nchi zao duniani.

Hivyo basi, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar umepata Tuzo hii katika kundi la kwanza.


Kwa mwaka huu, Viongozi sita wametunukiwa Tuzo hii. Miongoni mwao wapo Mheshimiwa Macky Sall, Rais wa Jamhuri ya Senegal; Mheshimiwa Hage Geingob, Rais wa Jamhuri ya Namibia; na Mheshimiwa Mark Rutte, Waziri Mkuu wa Ufalme wa Uholanzi. Hawa Viongozi watatu kwa pamoja ni Wenyeviti Wenza wa Jopo la Ngazi ya Juu la Kimataifa la Uwekezaji wa Maji barani Afrika (Co – Chairs of the International High-Level Panel on Water Investments for Africa). Mimi pia nimepokea Tuzo hiyo kwa nafasi yangu la Mwenyekiti Mbadala (Alternate Co – Chair) wa Jopo hilo.


Jopo lina wajumbe kutoka Afrika na Duniani kote. Kwa upande wa Afrika wajumbe wamepatikana kutokana na kanda zao ambapo kwa upande wa kanda ya kusini mwa Afrika mjumbe ni Mhe. Cyril Ramaphosa, Rais wa Afrika Kusini, kutoka kanda ya kati ni Mhe. Felix Tshekedi, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kanda ya kaskazini mjumbe ni Mtukufu Muhamad VI, Mfalme wa Morocco, ukanda wa magharibi mjumbe ni Mhe. Adama Barrow, Rais wa Gambia, na ukanda wa mashariki kuna wajumbe wawili: Mhe. William Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Tuzo zimetolewa kwa Viongozi hao wanne kwa kutambua utashi wao wa kisiasa na kazi kubwa waifanyayo katika kuongoza Jopo hilo na kuweka mikakati na mipango thabiti ya kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya maji barani Afrika, uwekezaji wenye lengo la kutekeleza Programu ya Uwekezaji katika sekta yam aji Afrika, yaani Continental Africa Water Investment Program (AIP). Kiasi cha dola za kimarekani bilioni 30 zinahitajika kuwekezwa kila mwaka barani Afrika hadi kufikia mwaka 2030.


Kiasi hicho cha fedha ndicho kitaziwesesha nchi za Afrika kutimiza Lengo la 6 la Maendeleo Endelevu (SDG 6) ambalo ni Kuhakikisha Upatikanaji wa Maji Safi na Salama ya Kunywa na ya Usafi wa Mazingira (availability of safe drinking water and decent sanitation for all) ifikapo mwaka 2030.


Mheshimiwa Rais,
Ndugu Wananchi,
Viongozi wengine wawili wa Afrika waliotunukiwa Tuzo hii ni wewe Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na Mhe. Haikande Hichilema Rais wa Jamhuri ya Zambia. Viongozi hao wawili wamepewa Tuzo hiyo kwa kutambua mchango maalumu walioutoa wao binafsi na Serikali zao kwa hatua za kutengeneza Programu za Uwekezaji katika Maji (Water Investment Programs), Programu ambazo shabaha yake kuu ni kuwa na mikakati thabiti ya kuendeleza sekta ya maji na usafi wa mazingira.


Na ukweli ni kwamba Zanzibar ndiyo ilikuwa ya kwanza barani Afrika kutayarisha na kuzindua Programu ya Uwekezaji katika Sekta ya Maji na baadaye ikafuatia Zambia. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa ya kwanza katika zile Serikali mbili za mwanzo kuwa na Programu ya namna hiyo. Hongera sana Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Hongereni sana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Ndugu zangu,
Waswahili husema Mcheza Kwao Hutunzwa na Chanda Chema Huvikwa Pete. Wananchi wa Zanzibar na Tanzania. Tuna kila sababu ya kuwa na furaha na kupokea kwa mikono miwili Tuzo hii aliyotunukiwa Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Pamoja na mambo mengine, Tuzo hii ni ishara kuwa Jamii ya Kimataifa imetambua jitihada zinazoendelea kufanywa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza sekta ya maji Unguja na Pemba.


Hivyo basi, Tuzo hii ni heshima kubwa kwake yeye binafsi, kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwa Wazanzibari wote. Tuzo hii imeiheshimisha Zanzibar Kimataifa na hamna budi kutembea kifua mbele mkijivunia na kufurahia. Napenda kusema tena Hongera sana Mheshimiwa Rais, Hongera Serikali ya Mapinzuzi Zanzibar na Hongereni Wananchi wote wa Zanzibar.


Mheshimiwa Rais,

Tunawatakia mafaniko mema katika utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Maji Zanzibar. Ni matumani ya International High Level Panel on Water Investments for Africa kwamba kama vile ambavyo Zanzibar ilikuwa ya kwanza Afrika kutayarisha na kuzindua the Zanzibar Water Investment Program, mtakuwa wa kwanza katika kufanikisha utekelezaji wa Programu hii. Tunatumai kuwa kupatikana kwa Tuzo hii kutakuwa kichocheo cha kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuongoza katika utekelezaji pia.


Jopo linatambua changamoto ya upatikanaji wa rasilimali fedha, nguvu kazi na vifaa ili kuleta ufanisi wa utekelezaji wa Continental Africa Water Investments Program na National Water Investment Programs, ikiwemo the Zanzibar Water Investment Program. Kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo, Jopo limepanga kuzindua Kampeni maalumu ya kutafuta rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Uwekezaji wa Maji Afrika mwezi Septamba 2023 mjini New York, Marekani.



Ni matumaini yetu kuwa Serikali za Nchi za Afrika zitashiriki kwa ukamilifu katika Kampeni hiyo kwani wao ndiyo wanufaika wenyewe wa kile kitakachopatikana kutokana na Kampeni hiyo.

Mheshimiwa Rais,

Kwa nia, dhamira na uwezo wako uliouonesha wa kutaka kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya maji Zanzibar, naamini kabisa wewe na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unayoiongoza mtakuwa mstari wa mbele kushiriki katika Kampeni hiyo. Sisi hapa nyumbani tunaona kazi nzuri unayoifanya, na Tuzo hii ni ushahidi tosha kuwa Jumuiya ya Kimataifa nayo pia wameona.


Mwisho kabisa japo si mwisho kwa umuhimu, nimalizie kwa kukuahidi kukupatia ushirikiano wowote utakaohitajika kutoka Jopo la Ngazi ya Juu la Kimataifa la Uwekezaji wa Maji barani Afrika katika kutekeleza programu mbalimbali za maji hapa Zanzibar. Nitafanya hivyo pia kwa nafasi yangu ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya GWPSA.


Daima nitakuwa tayari kusaidia kwa kadri nitakavyoweza ili kuhakikisha Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wananufaika na uwekezaji wa kimataifa unaofanyika katika Sekta ya Maji barani Afrika. Baada ya kusema hayo ninakutakia kila la kheri na mafanikio zaidi.


Kwa heshima na taadhima, ninakuomba sasa uridhie nikukabidhi Tuzo hiyo. 

Asante.
























 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2