Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa na Umoja wa Mataifa kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali yake ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha demokrasia nchini, na kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengi duniani.
Pongezi hizo zimetolewa katika Kikao cha 52 cha Baraza la Haki za Binadamu cha Umoja wa Mataifa ambacho kilianza rasmi tarehe 27 Februari 2023 na kimehitimishwa tarehe 4 Aprili 2023.
Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva, Mhe. Maimuna Tarishi, hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita hadi kupongezwa ni pamoja na kuwezesha vyombo vya habari kuwa huru, kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa, kujenga mahusiano na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani ikiwa ni pamoja na kuruhusu mikutano ya kisiasa.
Mhe Tarishi, ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika kipindi chote wiki sita cha kikao hicho, amesema kwamba Tanzania imeweza kufuatilia mwenendo wa hali ya haki za binadamu duniani, mwenendo wa mahusiano ya kimataifa, pamoja na kuelezea hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwa na Serikali kulinda na kusimamia haki za binadamu.
Halikadhalika, Mhe Tarishi ameeleza kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishiriki katika ajenda mbalimbali na kutoa matamko kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu zikiwemo za vijana, watoto, watu wenye ulemavu, watu wenye ualbino, haki ya maendeleo, makaazi ya kutosha, chakula na mazingira salama.
“Juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita zimeonekana katika Baraza hili ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kuimarisha demokrasia nchini.
“Hatua hizo ni pamoja na kuwezesha vyombo vya habari kuwa huru, kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa, kujenga mahusiano na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani ikiwa ni pamoja na kuruhusu mikutano ya kisiasa”, ameeleza Mhe. Tarishi katika taarifa yake.
Ameeleza pia kwamba Tanzania imeliahidi Baraza hilo la Haki za Binadamu kuwa itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu kupitia mikataba ya haki za binadamu ambayo imeridhia ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo.
Aidha, Mhe Tarishi amesema kwamba Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), alishiriki katika kikao hicho kwa njia ya mtandao ambapo aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa haki za binadamu nchini ikiwemo haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamadani.
Pamoja na masuala mengine, taarifa hiyo ya Dkt. Ndumbaro ilieleza kuwa Mahakama ya Tanzania ina mchango mkubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa haki na kusogeza huduma zake karibu na wananchi; na kuwa Serikali ilizindua kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wa msaada wa kisheria iitwayo “Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia” ili kuhakikisha kuwa watu wasiojiweza na hasa makundi hatarishi ya wanawake na watoto yanapata msaada wa kisheria wanapohitaji. Kwa upande wa elimu, ilielezwa kuwa Serikali imeendelea kutekeleza sera yake ya elimu bila malipo ili kuhakikisha haki ya elimu inapatikana.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva, Mhe. Maimuna Tarishi, akiwa nje ya jengo la mikutano mjini Geneva
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment