TIRA KASKAZINI YATOA ELIMU YA BIMA KWA WAKULIMA HANANG’. | Tarimo Blog
Na John Walter-Manyara
Mamlaka ya usimamizi wa Bima (TIRA) imewataka wakulima kukata Bima kwa ajili ya mashamba yao na mashine wanazotumia katika kilimo, ili kujilinda dhidi ya majanga mbalimbali ambayo yanaweza kuwarudisha nyuma kiuchumi.
Wito huo umetolewa na afisa Uhusiano na Mawasiliano wa TIRA Kanda ya Kaskazini Caroline Modest Makiluli wakati akitoa elimu kwa wakulima wilayani Hanang’ mkoa wa Manyara juu ya umuhimu wa kuwa na Bima kwenye mali zao mbalimbali wanazomiliki.
Amewaambia wanachama wa Sayuni Saccos na Amcos kuwa Bima za Mazao zitawasaidia kuwarudisha katika hali ya awali pindi wanapopata majanga ikiwemo changamoto za ya hali ya hewa pia endapo mazao yao yatashambuliwa na wadudu waharibifu.
Amesema kwa kuwa wananchi wengi wanajishughulisha na kilimo ni muhimu kukata Bima za mazao na Mifugo ili kuendelea kujihakikishia usalama wakati wote na kuepuka hasara ambazo zinaweza kusababishwa na kutokuwa na Bima.
Aidha amewataka wananchi katika mkoa wa Manyara wenye sifa ya kuwa watoa huduma za Kibima, wafike katika ofisi za TIRA Kanda ya Kaskazini Kaloleni Jijini Arusha au kupitia website yao ya www.tira.go.tz.
Afisa ushirika wilaya ya Hanang’ Damford Mpangala, amesema wilaya hiyo ina jumla ya vyama vya ushirika 17, ambapo 8 vinatoa huduma ya akiba na mikopo (SACCOS) yenye masharti nafuu huku nane vikitoa huduma ya kilimo na masoko (AMCOS) na kimoja kinajishughulisha na Madini.
Amesema vyama hivyo vimekaguliwa na vimetimiza sharti la kuwa na Bima ili kupunguza viatarishi ili kulinda fedha na rasilimali za chama.
Mwenyekiti wa kikundi cha Sayuni AMCOS kinachojishulisha na kilimo cha ngano Elizabeth Nko, amesema kikundi chao chenye wanachama 96 kimepata mafanikio makubwa kwa kuwa wameshajua umuhimu wa kuwa na Bima.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment