WAKULIMA WA MPUNGA WATAKIWA KUCHA KUTUMIA MAJI KWENYE MAJARUBA KULIKO MPUNGA UNAVYOHITAJI | Tarimo Blog

 

Na: Calvin Gwabara – Mbarali.

Tafiti zinaonesha kuwa Kilimo cha mpunga kinahitaji maji kwenye jaruba yasiyozidi sentimeta mbili tu tofauti na sasa ambapo wakulima wanajaza majaruba ya mpunga maji yenye sentimenta zaidi ya 30 na hivyo kupelekea maji mengi kupotea na kushindwa kutiririka vyema kwenda kwenye
matumizi mengine muhimu kama uzalishaji umeme.

Kauli hiyo imetolewa na Mtafiti na Mtaalamu wa kufanya Tathimini ya Maji kwa Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Japhet Kashaigili wakati akiongea na Mkuu wa wilaya ya Mbarali Mhe. Kanali Denis Filangali Mwila juu ya matumizi sahihi ya maji kwenye mpunga na kupunguza changamoto ya mivutano ya wakulima na Serikali kuhusu matumizi hayo ya maji.

“Utafiti wetu tulioufanya kuhusu matumizi ya maji kwenye kilimo cha umwagiliaji yameonesha wazi kuwa maji tunayotumia kwenye kilimo cha umwagiliaji hasa mpunga kwenye majaruba ni kingi mno kuliko mahitaji halisi ya zao hilo”, alieleza Prof. Kashaigili.

Alifafanua “Ili uzalishe mpunga unahitaji two hydro modules yaani kama (milimita mbili tu au sentimeta mbili) kuzalisha mpunga lakini ukitembelea kwenye majaruba mengi yanayofanya kilimo cha umwagiliaji utakuta maji yamejaa urefu wa kuanzia sentimeta 20 na wengine hadi 60 ambayo kimsingi yanapotea kwa mvuke na ardhini wakati yangeachiliwa kutiririka kwenda kufanya shughuli zingine kwingine”.

Prof. Kashaigili amesema mradi huo ulilenga kuongeza uzalishaji wa mpunga na kuruhusu maji kwa matumizi ya sekta zingine zenye uhitaji kwa maana kuna sekta nyingine nyingi ambazo zinahitaji maji hayo ili kuziendesha.

Aidha amesema kutokana na utafiti huo wakulima hawana sababu ya kuchepusha maji zaidi ya sentimenta mbili kuingia kwenye majaruba yao ya mpunga na kuyatuamisha ili waweze kuacha maji mengine yatiririke mtoni kwenda kwa wengine wenye mahitaji na hivyo kuendeleza mtiririko salama
wa maji mtoni bila kuathiri wengine wenye uhitaji.

Amesema changamoto nyingine kwenye skimu za umwagiliaji na mashamba ya wakulima ya mpunga hakuna njia za kupitisha maji kurudi mtoni mara baada ya kuyatumia na hii kuchangia maji mengi kupotea bila sababu wakati hayahitajiki na mmea.

Mtafiti huyo kutoka SUA amesema inashangaza kukuta mashamba ya mpunga yamejaa maji hadi sentimeta 40 wakati zinatakiwa sentimeta mbili tuu na hivyo kufanya suala matumzi sahihi ya maji kwenye mmea kutozingatiwa kwakuwa kitaalamu sio wakati wote maji yanatakiwa kwenye
shamba bali yanatakiwa kuwekwa pale yanapohitajika tu na kuacha pakauke.

Kwa upande wake Msaidizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais upande wa Bionuai Thomas Bwana amesema Wilaya ya Mbarali ni moja kati ya maeneo ambayo viongozi wanapata shida katika kuweka mizani ya matumzi ya maji ya wananchi kwenye kilimo na shughuli zingine za
mazingira na miradi ya maendeleo.

“Nitumie nafasi hii kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kuwapa pole sana Viongozi wa wa Wilaya hii maana kati ya maeneo ambayo changamoto hii ni kubwa sana ya kuweka mizani hiyo kwa wananchi ni Wilaya ya Mbarali lakini bado tunayo nafasi ya kufanya uzalishaji na kuacha mazingira nayo yakiwa hai kwa faida yetu sote maana tunategemeana na hata hivyo sio kila sehemu ilimwe na sio lazima kila maji yatumike”, alisema Bw. Thomas.

Amesisitiza kuwa kupitia tafiti hizo ni ushahidi wa wazi wa kisayansi kuwa maji yanayotumika Mbarali kwenye kilimo sio yote yanayohitajika na kwamba kuna maji mengi wanayachukua bila sababu na hivyo kuomba watafiti waendelee kusaidia kutoa elimu katika eneo hilo ili jamii ibadili
mtazamo huo hasi wa muda mrefu wa matumizi ya maji.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo ya Mbarali Kanali Denis FilangaliMwila amesema wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kwa kushirikiana na Serikali kuu kwa ukaribu na kuwashuru watafiti hao kwa kazi nzuri ambayo ikiwafikia wakulima wengi itasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima na Serikali yao lakini amesisitiza kuwa lazima maslahi ya wengi yapewe kipaumbele dhidi ya maslahi ya wachache na ikifika maamuzi magumu yafanyike kwa maslahi ya taifa.





Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2