MWAROBAINI WA MIUNDOMBINU KOROFI SERENGETI WAPATIKANA | Tarimo Blog

Kamishna Kuji atoa maelekezo mahususi Serengeti

Na. Edmund Salaho/Serengeti.


Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA Juma Kuji leo amefanya ziara ya kukagua miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuiagiza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kushughulikia mara moja maeneo korofi ya barabara ndani ya hifadhi hiyo, ili watalii wafikie adhma yao ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Akizungumza baada ya kukagua maeneo hayo Kamishna Kuji, ameielekeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kurekebisha maeneo yote korofi na kuhakikisha kuwa hakuna maeneo ambayo hayatapitika licha ya uwepo wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ili kupunguza adha kwa wageni.

“Licha ya changamoto ya mvua kubwa zinazoendelea hatuwezi kusubiri ziishe tumeazimia kushughulikia kwa haraka maeneo yote korofi ikiwa ni hatua za haraka, lakini lengo kuu ni kuhakikisha  barabara hizi zinakuwa na tabaka gumu, haya ni maagizo yangu kwa menejimenti kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote”.

Aidha,Kamishna Kuji alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchi nzima.

Vile vile, Kamishna Kuji amebainisha kuwa TANAPA imejipanga kuhakikisha miundombinu yote katika Hifadhi za Taifa Tanzania inaboreshwa ili kukidhi matamanio ya wageni wanaotembelea Hifadhi za Taifa zilizosheheni  sifa lukuki za kuwa na utajiri mwingi wa bayoanuai.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu Mhandisi. Dkt. Richard Matolo alibainisha kuwa Shirika limekuwa likitumia teknolojia mbalimbali kutafuta mwarobaini wa changamoto za barabara na kubainisha kuwa mwaka huu hali imekuwa tofauti kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha tofauti na miaka mingine.

“Shirika limefanya majaribio mbalimbali na kuja na teknolojia ambazo zitapelekea barabara hizi hususani hii ya Naabi iwe inapitika wakati wote tafiti nyingi zilionekana haziwezi kuleta matokeo chanya katika maeneo haya kutokana na asili ya udongo wa hifadhi zetu hivyo kutokana na stadi zote imethibitika kuwa tunaweza  kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizi”

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moronda Moronda amesema, Menejimenti ya Serengeti imejipanga kuhakikisha maeneo korofi yanarekebishwa na kutoa rai kwa waongoza watalii kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali katika Hifadhi ikiwemo alama mbalimbali za barababra ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza hasa wakati huu wa mvua.

Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mkuu anayeshughulikia Mawasiliano Catherine Mbena, alisema
"Lengo letu kama Shirika ni kuhakikisha wageni wetu(watalii) wanapofika maeneo yetu wanaondoka na kumbukumbu nzuri, ndio maana timu nzima ya TANAPA iko hapa kuhakikisha kipande hiki korofi kinapitika na tumekuwa na mipango ya muda mrefu na mfupi na yote tutaitekeleza lengo likiwa ni wageni wetu wafurahie vivutio hivi vya kipekee duniani"

Hifadhi ya Taifa Serengeti hivi karibuni imekumbwa na changamoto ya barabara kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Tanzania na nchi jirani, hivyo ukarabati wa miundombinu ya barabara hizo unaofanywa na TANAPA utaondoa adha hiyo na kuzifanya barabara za hifadhi za Hifadhi ya Taifa Serengeti kupitika mwaka mzima.

 










Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2