SIMULIZI-NIKICHEKA, UTALIA!!!! SEHEMU YA 04


Mtunzi::Eligi Gasto Tarimo.    
Simu: 0766054094/0718878887
Betty hakuwa na habari kuwa mlinzi aliyempiga kibao ndiye aliyefariki kwa kudondoka ghorofani jengo la Mwanjonde lakini alisikia taarifa za kifo cha huyu mlinzi.
Kwakua hakumfahamu wala hakutilia maanani sana. Betty hakukumbuka kuwa siku aliyofariki mlinzi ilikua jumamosi na Mwanaidi alifariki jumapili.
          Betty alimkumbuka rafiki yake kipenzi Mwanaidi alitamani wangekua pamoja na mgeni huyu ili wote waambulie kujua kilichomchekesha. Alikumbuka jumapili ya kifo cha Mwanaidi alimwacha amelala asubuhi hiyo. Betty aliaga kwenda kanisani na siku hiyo aliamua kwenda mbali kidogo eneo la Mkuyuni ambapo ni lazima apande gari mpaka kanisani, ni kama kilomita zaidi ya 5. Kwakua alikua anakwenda kanisani simu aliiacha sababu asingekua na matumizi ya simu kanisani. Betty anakumbuka majira ya saa 6 mchana aliporejea kutoka kanisani anakutana na vikundi vilivyompokea kwa habari ya kushtua. Alikumbuka vyema alipoondoka amechanganyikiwa kwenda hospitali ya Bugando alipoambiwa ndipo alipopelekwa Mwanaidi. Hawezi kamwe kusahau alipoitwa na daktari kwa upole na kupewa taarifa za kifo cha rafiki yake kipenzi Mwanaidi. Asichokumbuka ni muda gani alizinduka baada ya kuzimia kwa habari zile za kutisha na kuogofya.

             "Yatupasa kushukuru kwa kila jambo" utamskia mtu akimshukuru Mungu kwa kupata kazi, wengine kwa kufaulu vyema masomo, wengine kufanikishiwa mambo yao, wengine baada ya harusi hushukuru kwa jambo walilolingojea kwa muda mrefu lakini NI NADRA kuwasikia wafiwa wakimshukuru Mungu kwa kumtwaa mmojawapo wa wapendwa wao. Hata wengine wakifeli sidhani kama wanakumbuka kumwambia Mungu asante. Je haipaswi kushukuru?
          Akiwa katika mawazo haya mara akaingia mgeni akiwa mikono mitupu bila chakula chochote. Mgeni aliingia moja kwa moja kitini akaketi kisha akashusha pumzi haijulikani za uchovu wa kutembea au za kukosa kitu alichokifuata. Betty alimtumbulia macho kuanzia kichwani mpaka miguuni alishindwa amwanzie wapi, alijiuliza amuulize swali gani mgeni huyu.
“mamito Ukistaajabu ya Musa mbona ya firauni utayaona. Usiogope chakula nmeacha wanatengeneza fulu madikodiko huwezi kula viporo mrembo kama wewe, nmeacha oda wanaanda chakula cha moto cha leo leo, eti mla mla leo mla jana kala nini? Wahenga wenu bana hawajui mla jana kashinda nja au kala kiporo cha juzi cha mlenda” Mgeni alibwabwaja maneno.
Kama ni kucheka Betty nusura aanguke, aliangua kicheko akacheka sana.
“Kwakweli leo nimepatikana, kama ningepata wageni watata kila siku hivi haina hata haja ya kula, yaani…..” Betty aliongea kwa mkato.
          Mgeni alifungua kibegi chake akatoa juisi kubwa ya boksi ya embe kampuni ya Azam.
“Waooooo!!!” Betty akatanabahi.
“Sasa kabla sijaiombea ebu pekua popote unapojua tafuta vya kunywea hii karamu aidha glasi au vikombe si mbaya suuza suuza na maji ndio baraka uje tufungue shampeni hii” Mgeni alizidi kutokwa na maneno.
Betty aliishaanza kumzoea mgeni huyu mwenye visa, alinyanyuka na kusogea kwenye kijikapu kilichokuemo kwenye kona kisha akatoa glasi mbili zenye urembo wa maua maua kisha akalifuata jagi lililokua mezani akamimina maji kwenye glasi zote mbili kisha akatoka nje akimwacha mgeni akifungua simu ya Nokia tochi.
“Ngoja nisuuze glasi, iyo simu unahangaika haina umeme nini huenda uko porini kwenu hamna hata sola” Betty alitania kisha alitoka nje na zile glasi akasuuza kisha akarudi ndani. Mgeni alifungua boksi la juisi kisha akamimina juisi kwenye glasi zote mbili.
“ayaaaaa! Nmesahauu. Shake well before use(tikisa vizuri kabla ya kutumia) Mgeni alisema kisha alichukua glasi zote akapunguza zile juisi kwa kuzirudisha kwenye boksi kisha glasi zote zikawa nusu.
“Sasa ntafutie kijiko nikuoneshe nilivo mjanja” mgeni akasema.  
Betty alichukua kijiko akatoka nje na jagi la maji kwenda kukisuuza huku akisema;
“mgeni msumbufu huyu ntakomaje leo” Betty akaongea kwa utani. Alisuuza kijiko kisha akarudi, mgeni alimimina juisi akajaza glasi zote mbili kisha akachukua kile kijiko na kukoroga vyema. Akachukua glasi moja akampa Betty nyingine akabaki nayo kisha akasema;
          “Hapo nisha shake well, kukoroga ni sawa na kutikisa mchanganyiko umekamilika sasa kisheria glasi ya kwanza unakunywa mfululizo adi iishe na pili ndio unakunywa taratibu, hii ya kwanza ni ya kukata kiu haya moja, mbili tatuuu…..”  Mgeni akaongea kisha wote kwa pamoja wakanywa mpaka glasi zikawa tupu kisha akamimina tena glasi zikajaa.
“Haya sasa unaweza kunywa taratibu, nipe kwanza simu yako nimtumie ujumbe kule nlipotoka kamati ya maakuli nijue kama msosi umeiva, najua simu yako meseji unazo mia 3, nyie hamkosi meseji kila siku mnajiunga” mgeni alinena.
“Chukua tuma meseji mpaka uchoke lakini hakikisha unaemtumia hanisumbui maana nyie….” Betty alikabidhi simu.
          Riziki mgeni wa Betty alichukua simu kisha akaandika ujumbe akautuma sekunde chache majibu yakarudi.
          “Yeees hapo safi, sasa ngoja nikalete mazagazaga kibao uko, ngoja niende na hiki kibegi nikabebe kweli kweli, tukishakula ndio nitaweza kutamka jina langu ulimi utalainika, haya tafuta njaa ya kutosha endelea na juisi nakuja sa ivi” Mgeni akaongea kisha akachukua kibegi chake akatoka nje akimwacha mwenyeji wake akicheka.
                                                                                 XXXXXXXXXXX
          Ndani ya mahabusu kituo kikuu cha polisi Nyamagana jijini Mwanza Pascal Mtumbuka aliketi kona moja akilia kwa uchungu. Ni kilio cha kilichodhihirisha huzuni aliyonayo na pengine uchungu alionao. Ni mara yake ya kwanza kukamatwa na polisi na haijawai kutokea katika maisha yake akanasa kwenye mikono ya watu hawa kwani hakua mtu wa makosa na wala hajawai kutegemea au kufikiria kuna siku ataingia mikononi mwa polisi. Siku zote aliwashangaa wote wanaokamatwa na polisi akisahau msemo usemao sio wote waendao jela wana makosa. Hakika mcheka kilema hafi bali humpata.
          Akiwa amejikunyata kwenye ukingo wa chumba hiki machozi yaliendelea kumtiririka akawaza hili na lile bila kujua hatima yake. Kama ni kulia ameshalia sana alitamani muujiza utokee na yote yasahaulike lakini kamwe mambo hayakua kama ilivyo maombi yake akaukumbuka msemo wa wahenga ulipendalo hupati, hupata ujaliwalo. Machozi yalimkauka baada ya kulia sana. Ama kweli ukiambiwa kua uyaone ukadhani ni maghorofa uko sahihi kwani maghorofa ni kweli utayaona lakini maghorofa yenyewe si haya ya kuonekana kwa macho yaani majengo, bali maghorofa ni pale unapoachana na kutegemea wazazi au walezi na kuingia kwenye utegemezi wako mwenyewe kwani ndo kukua na umetoka kwa wazazi ni mkubwa sasa, ukipata mtiririko wa shida, raha, umaskini, magonjwa utajiri, uhuni, dhiki, taabu nk hivyo ni miongoni mwa vyumba utakavyoishi kwene maghorofa uliyodhani. Na hakika hutakaa chumba kimoja ni juhudi yako mwenyewe kung'ang'ania vyumba fulani kwenye hayo maghorofa ambavyo unavutiwa kukaa, ukipenda utajiri au dhiki ni hiari lakini elewa kuwa kuna vyumba lazima uvipitie kwa kupenda au kutopenda..........
          Mawazo lukuki yaliendelea kumwandama katika kichwa chake na ndipo akaanza kuukumbuka mkasa mzima uliomfanya kuingia katika chumba hiki kigumu na kisichopendwa na mtu yeyote. Labda wapo wanaokipenda lakini si yeye.
          Siku ya ijumaa wanachuo wa kozi ya BASO kwa mwaka wa kwanza wana kipindi kimoja tu ambacho huanza saa kumi na moja kasorobo jioni. Pascal mtumbuka ni mmoja wa wanaochukua kozi ya BASO akiwa ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa shahada hii. Ijumaa hii alichelewa kuamka na hakuwa na sababu ya kuwahi kuamka sababu hakua na kazi yoyote ya kufanya hivyo alilala hadi akaridhika na usingizi ulipomwishia bado aliendelea kujilaza kitandani mpaka kijua kilipoanza kupenya kwenye chumba chake hiki kidogo. Aliamka kisha akachukua mswaki na kuingia bafuni kufanya usafi wa kichwa. Chumba anachoishi ni kidogo lakini kina choo na bafu ndani (Self container) Vile vile anaishi pamoja na mwenzake ambaye anasoma kozi ya ualimu lakini yeye yupo mwaka wa pili. Baada ya kumaliza usafi ikiwa ni pamoja na kuoga aliwasha jiko la gesi lililokuwa ndani kisha akatenga chai, hakusubiri ichemke bali alitoka nje kutafuta vitafunwa. Baada ya muda alirudi na kuandaa kifungua kinywa chake.
          Baada ya chai aliketi kutazama runinga ndogo iliyokuwa chumbani humu huku amejiegesha katika kitanda na simu yake akikagua hili na lile. Mara simu ikaanza kuita na alipoitazama namba iliyopiga haikuwa na jina ikiwa na maana ni namba ngeni kwenye simu yake. Aliipokea akaongea;
“Haloo”
“haloo, shwari kaka” Upande wa pili ulinguruma.
“Mi poa, naongea na nani?” Pascal akasaili.
“Unaongea na aliyefumuliwa kibao na mlinzi pale bustanini” Sauti ya upande wa pili ilijibu.
Pascal kicheko kilimtoka, alikumbuka vyema siku aliyokaa bustanini akiwa pamoja na Mwanaidi na Bertha kisha mwanachuo mmoja akavuka kuingia ndani zaidi ya bustani kufuata kivuli. Alikumbuka mlinzi alipomtandika kibao ndipo mwanachuo huyu akageuka na kumtazama. Alikumbuka vyema badala ya kukasirika alitumia sekunde chache kisha akamcheka mlinzi yule.
“Kaka vipi mbona kimya?” upande wa pili ulisikika.
“aaagh pamoja mkubwa, niambie?” Pascal aligutuka kwenye kumbukumbu yake hii fupi.
“Sasa……. Vipi leo ratiba yako ngumu nataka tumeet tuchonge ishu flani ivi” upande wa pili ulisikika.
“kwa leo niko free mida hii, ntaingia pindi jioni sana” aliongea Pascal.
“Poa bro, ntakucheki mida tupeane michongo” mpigaji alijibu.
“Haina kwere kaka” Pascal alijibu kisha simu ikakatwa.
          Pascal alijiuliza asipate jibu la uhakika, kwanza ni mtu ambae hamfahamu zaidi ya kumuona akizawadiwa kibao na mlinzi, pili hata jina halifahamu na wala hajui ni kozi gani anayosoma. La kushangaza zaidi anakuja eti waongee na wapange mambo fulani.
Ajabu!
Aliamua avute subira kumsubiri. Labda ni kweli mgeni njoo mwenyeji apone. Pascal alijaribu kujikumbusha kama amewai kukutana mahali popote na mgeni huyu tofauti na siku aliyomshuhudia akiadhibiwa na mlinzi. Alikumbuka alipomcheka mlinzi na hakuishia hapo baada ya mlinzi kumkaripia tena kwa maneno makali bado alirudia kucheka. Hakusahau alipowageukia na kuwacheka na ndipo alipowajongelea na kuchukua namba zao.
“ahaaa, nlikua najiuliza katoa wapi namba zangu, kuumbe” Pascal alijisemea kimoyo moyo baada ya kukumbuka jambo fulani. Alishtuka kidogo baada ya kukumbuka nia na madhumuni ya mwanachuo huyu wasiyefahamiana kuchukua namba zao ilikua ni kwa lengo la kuwaambia ni kwanini na kipi kilichomchekesha. Fikra zake zilimrudisha na kumkumbusha kauli aliyotamka “NIKICHEKA UTALIA” 
“Ina maanisha nini?” alijiuliza.
Ni dhahiri kicheko ni ishara ya furaha na mtu akicheka humaanisha kafurahi sasa mambo ya kilio yanatoka wapi? Alifikiri zaidi huwa anasikia kuna machozi ya furaha yaani inakua kinyume mtu analia lakini si kwa huzuni bali kwa furaha lakini kamwe hajawahi kusikia kicheko cha huzuni.
“Aaagh, Nia njema ni tabibu nia mbaya huharibu” alijisemea kisha akaachana na mawazo yale ya kuchanganya akaongeza sauti ya runinga iliyokua inabamba mziki akaburudisha akili yake.
NINI KITAFUATA??????
FUATILIA SEHEMU IJAYO.....................

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2