SIMULIZI-NIKICHEKA UTALIA!!! SEHEMU YA 05

NIKICHEKA, UTALIA!!!!!!

Mtunzi::Eligi Gasto Tarimo.  
Simu: 0766054094/0718878887
Michezo ya kigeni haina maadili,
sababu watu wanajidhalilisha hadharani kwa yeyote,
hata kwa ndugu zao.
Kila mwanaume ana mwanamke,
Ingawa si mke wake,
wanacheza ndani ya nyumba,
na hakuna taa,
bila aibu, wanakumbatiana pamoja,
wamegandana, wamegandana
hawawezi hata kupumua....Pascal aliwaza akiwa anatazama nyimbo zile za kizungu zilizokua zinarushwa runingani.

          Majira ya saa saba kama na nusu mchana ujumbe mfupi uliingia kwenye simu ya Pascal uliandikwa hivi;

          SWEETHEART  NIPO PEKE YANGU MPWEKE, NAJUA UPO FREE, PLEASE NJOO UNIPE KAMPANI NA KUNA KITU KIZURI NATAKA NIKUPE. NJOO NA JUISI YA AZAM MANGO PLEASE. NIJIBU NIKUPE DAKIKA NGAPI?
Looh, ujumbe huu ulimsisimua sana, aliingia sehemu ya kujibia ujumbe akajibu kama ifuatavyo;
USIHOFU NDANI YA DAKIKA 5 NITAKUA NIMEFIKA.
Kisha akatuma haraka, akakurupuka akavaa shati na suruali haraka kisha akachomea sendozi miguuni akajipulizia kipafyumu akatoka akafunga mlango kwa funguo akanyoosha moja kwa moja duka lililo jirani. Alipokamilisha alichohitaji aliikimbilia pikipiki iliyo karibu dereva akatia gia kufuata maelekezo nyuma liliachwa vumbi linapaa hewani.
          Kutoka Nganza anapoishi Pascal mpaka Hosteli za Kwa Mashau kwa kina Betty alitumia dakika sita akaingia akamkuta Betty akinywa juisi taratiibu. Ni kama ile ambayo amemwagiza.
          “wooouu na wewe pia umeniletea juisi. Leo mbona leo sherehe tena afadhali umekuja maana mchekeshaji ameenda kuchukua chakula anakuja sasa hivi, na wewe una machal….” Betty alimkaribisha Pascal na maneno kibao lakini kabla hajamaliza ghafla alianza kujishika tumbo. Pascal hakumjali aliisogelea meza iliyokua na komputa mpakato ambamo mziki uliimba akaanza kubonyeza.
“Wengine mnalazimisha tu hata taarabu mkipelekwa hamuwezi” Pascal alilalama.
          Pascal aliendelea kucheza na kompyuta lakini mara alisikia Betty akilalama kwa maumivu huku amekumbatia tumbo lake. Pascal alimtazama akitaraji ni utani lakini Betty aliendelea, hatimae akaanza kutoa machozi hakika alilia huku akilitaja jina la Pascal.
“Pascal tumbooo….. tumbo linauma Pascal, nisaidie Pascal ….. tuumboooo……” Betty alizidi kulalama.
Pascal alikagua huku na huku kutafuta maji alipoyaona alimnyeshwa kisha akamhimiza ajilaze litatulia. Betty alijitahidi kulala lakini maumivu yalizidi alizidi kulia huku akilikumbatia tumbo lake. Kilio kiliongezeka sauti ikapaa kwa nguvu.
“Pascal tumbooooo…… Paaaaascaaaaal Paascaaal. Wanachuo waliokua vyumba vya jirani waliingia ghafla kuuliza kulikoni baada ya kilio kikubwa cha Betty. Utaratibu ulifanyika usafiri ukatafutwa Betty akakimbizwa zahanati ya chuo lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya. Betty hakuwa na nafuu ni kilio cha uchungu wa maumivu ya tumbo. Alilia sana mpaka akazimia. Zahanati ya chuo walishauri apelekwe Bugando. Gari likatafutwa ni Ambulance ya chuo, gari ikateleza kwenye lami kumuwahisha Hospitali kubwa ya Bugando. Pascal na baadhi ya wanachuo walikua katika gari kwenda Bugando.
          Walipokelewa na manesi akaingizwa moja kwa moja kwa daktari kufanyiwa uchunguzi. Pascal na wenzake wakiwa nje wameketi kwenye benji wakisubiri hatma ya mwenzao Betty. Muda mfupi baadae daktari akatoka kumtazama usoni sura yake iliongea jambo.
Ilitangaza huzuni!!
Daktari akawafikia, alikuja kutoa taarifa za mgonjwa, akasimama akawatazama kisha akaitafuta kauli, akarekebisha koo kisha akanena;
Mgonjwa wenu amefariki!!!!!
Pascal hakushtuka, au pengine alishtuka lakini bila mtu yoyote kugundua lakini ni dhahiri kuna jambo lilimpata.
Alipigwa na bumbuwazi!!
Betty amefariki??!!!
Haiwezekani!!!
“Haiwezekani doktaaaaaa………mpime vizuriiiiiiii……” Pascal alipoupata utimamu wake aliropoka. Wenzake hawakumjali. Si kwamba walimpuuza. La Hasha. Wengine walikua wanalia kwa nguvu, wengine wamestaajabuu, wengine walikua katika butwaa, wengine walijihisi ndotoni, kila mtu alikua bize.
          Taarifa za uchunguzi zilizokuja baadae zilikua za kushtua zaidi. Ndio, kila mtu alishtuka. Taarifa zilidai.
Betty alitumia kitu chenye sumu!!
Loooh ni mauza uza haya!!!
Kitu chenye sumu??
Kutoka wapi??
          Uchunguzi wa kipolisi ulifanyika, ukaguzi ulifanywa kuanzia chumba alichoishi Betty. Majirani walihojiwa, marafiki walihojiwa, chumba kilipekuliwa. Ilikutwa juisi ilichukuliwa ikapimwa.
Glasi ilithibitika ilikua na sumu!!
Majirani walithibitisha mara ya mwisho alikua na Pascal!!
Simu ilionyesha mtu wa mwisho kuwasiliana nae alikua Pascal!!
          Pascal alikamatwa kama mtuhumiwa namba moja  kwa mauaji ya Betty, ushahidi wote ulimhusisha moja kwa moja na kesi hii ngumu ya jinai. Alikamatwa na kuwekwa moja kwa moja katika mahabusu hii. Pascal aliendelea kukumbuka mambo mbali mbali.  
                                         xXXXXXXXXXXXXXXXXX
          Siku hii ya jumatatu ni majira ya karibu saa sita mchana msaidizi wa Mhadhiri wa somo la uhariri wa habari Shawo alikua darasani akiendelea na somo. Katikati ya somo Mr. Shawo alitoa swali la ghafla kwa chuoni ni maarufu(Quiz) ambalo linaweza kuwa ni rahisi lakini lengo lake ni kuchukua Mahudhurio ya waliofika darasani. Ilibakia dakika kama 10 ndipo kipindi kimalizike kwani kilikuwa kimoja tu. Kwa kawaida vipindi vya chuo kipindi kimoja huchukua dakika 60 yaani takribani saa moja na kama ni viwili inamaanisha masaa mawili.
          Riziki alikaa kiti cha karibu na Jovin Odelo ambaye alianza kuingia darasani siku ya Ijumaa ambayo wakati anatambulishwa Riziki hakuwepo darasani kwa siku hiyo. Riziki alimtazama Jovin akatanabahi kuona ni sura ngeni hajawai kuiona kabla darasani. Ingawa si rahisi kufahamiana majina kwa Kozi nzima sababu ya wingi wa wanachuo lakini haiepukiki kufahamiana sura kwani mnaonana darasani kila siku. Msemo wa Kiswahili kuku mgeni hakosi kamba mguuni. Riziki alimwinamia akamnong’oneza;
“sorry, we ni muhusika wa hili darasa?” Riziki akamsaili.
“yeah ni mhusika, kwani hukuwepo juz……………? Kabla hajamaliza Mr Shawo aliyekua anafundisha aliwaona na kuwaita mbele ya hadhira.
“Mimi nafundisha halafu wengine wanafundishana. Haya nataka muniambie neno la mwisho nimeongea nini?” Shawo akauliza kwa hasira. Kwakuwa walikua wanajadili jambo wakati Shawo anafundisha ni dhahiri hawakua na jibu. Walijaribu kujitetea lakini hakuwaelewa kabisa akaamua kufanya maamuzi.
“Sasa mtoke nje, na kuanzia leo darasani kwenye kipindi changu nisione sura zenu, hata akiwepo Profesa Mfumbuka siwahitaji nitamweleza mna utovu wa nidhamu, haya ondokeni nisiwaone tena” Shawo aliongeza kwa hasira. Walijaribu kumsihi kwa namna walivyoweza lakini haikusaidia. Ilikua ni fedheha na hasa kwa Jovin ambae hakuwa hata na zaidi ya siku tatu darasani. Mara alisimama Sarapia Pelemunge na kuongea;
“Jamani mwalimu amewaambia mtoke nje muende mnatupotezea muda, kama ni kujadili mtamuona baadae tuacheni sisi tusome”
“aaaggh…… kaa chini…… kwani wewe nani……..” Darasa likagawanyika wengi hawakufurahishwa na maneno ya Sarapia. Wengine walimponda, wengine walinyoosha mikono juu, wengine walimzomea na wengine walikaa kimya.
Riziki alimtazama Sarapia kisha akacheka!!
Kisha akamtazama Mr Shawo akaendelea kucheka!!
Baadhi ya wanachuo nao wakacheka!!
Riziki akaongea “Sawa mwalimu tunatoka”. Kisha wakaongozana nje pamoja na Jovin kutoka nje wengine wakendelea na somo.
                                                       XXXXXXXXXXXXXXX
          Kituo cha polisi Nyamagana uchunguzi wote ulikua umekamilika. Pascal baada ya kuhojiwa sana maelezo yote yalimtia hatiani moja kwa moja. Kulingana na ushahidi majirani wa Betty waliohojiwa walikiri mpaka wakati hali inakua mbaya ni Pascal ndiye alikuwa na Betty. Walienda mbele zaidi na kudai hata wakati anaumwa alikua analitaja jina la Pascal kwa sauti ya juu. Pia Pascal alikiri ni kweli alimletea Betty juisi na ni yeye aliyemwagiza lakini alidai alimkuta Betty anakunywa juisi kama aliyoleta. Hapo hakuna aliyemwelewa eti amkute mtu anakunywa juisi ambayo ndio aliagiza aletewe?! Ujumbe wa mwisho uliopatikana kutoka katika simu ya Betty ulikua ni msumari mwingine kwa Pascal.
          Shida, taabu, raha, matatizo magonjwa vyote kaumbiwa binadamu na kila kitu kinachotokea katika maisha labda kinatokea kwasababu fulani au bahati mbaya lakini lazima kitokee, yawezekana hiyo sababu ukawa unaipenda au huipendi lakini hiyo haifuti ukweli kuwa mambo hutokea na ni lazima yatokee. Yawe ni mabaya, mazuri, ya kuumiza au ya namna yoyote. Kuna muda mambo hutokea kulingana na mazingira au mahali fulani ambapo hutokea bila kutarajia, ni kama ajali fulani ya ghafla.
          Wazazi na ndugu wengine wa Pascal walikuja kumtembelea baada ya kusikia masaibu yaliyomkuta. Siku zote aliishia kulia na kuomba iwe ndoto lakini haikuwa hivyo. Ukweli halisi ulibaki pale pale. La kuvunda halina ubani. Kesi ya mauaji ilimkabili.
ITAENDELEA.......................

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2