UFAHAMU UGONJWA WA KISUKARI NA MAMBO 10 YA KUZINGATIA KWA MGONJWA WA KISUKARI




Kisukari ni hali inayotokea wakati sukari inapozidi ile inayotakiwa katika damu kwa sababu ya upungufu au ukosefu wa insulini. Insulini ni kichocheo kinachotengenezwa kwenye kongosho na hutumika kusaidia mwili kutumia sukari inayotokana na vyakula tunavyokula. Ugonjwa wa kisukari unatokana na kichocheo hiki kupungua, au kutokufanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha sukari kinabaki kuwa kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye chembe chembe chembe hai za mwili.


DALILI ZA KISUKARI
Zifuatazo ni dalili za kisukari;
 Kiu isiyoisha
Kukojoa mara kwa mara
Kupungua uzito
Kusikia njaa kila wakati
Mwili kukosa nguvu
Kuchoka haraka
Jasho jingi
Kizunguzungu 
Vipele mwilini

TIBA YA UGONJWA WA KISUKARI
Ugonjwa wa kisukari hauna tiba kamili, ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa kwa malazi mazuri, virutubisho na mazoezi.

VYAKULA VYA MGONJWA WA KISUKARI
Mgonjwa wa kisukari anapaswa kula vyakula vya aina nyingi kila siku ili apate vitamini na madini ambayo mwili wake unahitaji ili kukua na kuwa  mwenye afya. Mgonjwa wa kisukari azingatie zaidi ulaji wa vyakula vitokanavyo na mimea, aache kula vyakula vya kusindika, vyenye sukari na mafuta mengi. Anatakiwa pia kula mchanganyiko wa matunda, mboga na nafaka zisizokobolewa. Hii ina maana kwamba mgonjwa anatakiwa asisikie njaa wala shibe muda wote wa siku. Kula kidogo au viwango vichache vya chipsi, biskuti, karamu, peremende, siagi, majarini, kachumbari, chumvi, vyakula vilivyokaangwa, aiskrimu na soda. 

 Kula vyakula vidogo ambavyo vimekaangwa au vilivyo na wanga yenye mafuta mengi. jaribu mikate iliyo na nafaka na mahindi kama vile mkate wa ngano, Kula matunda na mboga nyingi.Tumia mafuta kidogo sana, au siaga wakati unapopika. Epuka matumizi ya pombe, sigara, tumbaku na madawa ambayo hushusha kinga ya mwili kupigana na maambukizi. Epuka vyakula vyenye sukari na usile chakula kingi. unaweza kula kidogo kidogo kulingana na matumizi ya dawa. Punguza kiasi cha chumvi kwenye chakula na kununua vyakula vilivyotengenezwa tayari. Maharage, samaki, mtindi, soya  nyanya, mayai na wali pia ni vyakula visivyo na ghalama sana na ni salama kwa mgonjwa wa kisukari.

VITU MHIMU VYA KUZINGATIA KWA MTU YEYOTE ANAYESUMBULIWA NA UGONJWA WA KISUKARI:
  • Acha kabisa soda ya aina yeyote pamoja na juisi za viwandani hadi hapo utakapopona\
  • Acha chai ya rangi na kahawa
  • Jishughulishe zaidi na mazoezi
  • Ongeza unywaji maji na utumiaji wa chumvi hasa ya mawe ile ya baharini
  • Dhibiti uzito wako, hakikisha una uzito ule unaotakiwa kuwa nao kwa mjibu wa urefu wako
  • 6Tumia vyakula ambavyo havijakobolewa, mfano kama ni ugali tumia unga wa dona na siyo wa sembe
MAMBO 10 MUHIMU YA KUZINGATIA KWA MGONJWA WA KISUKARI

1. KUACHA KUTUMIA VYAKULA VYENYE SUKARI YA MOJA KWA MOJA
·         Kuacha matumizi ya Sukari pamoja na vyakula au vinywaji vyenye sukari ya moja kwa moja kama soda na juisi iliyotiwa sukari
o    Matumizi ya vitu hivi huongeza sukari mwilini kwa wingi na hivyo kuleta shida katika kudhibiti kiasi cha sukari mwilini
·         Kama unahitaji kuongeza utamu kwenye chai au vinywaji vingine tumia sukari bandia (artificial sweeteners).
 2. TUMIA VYAKULA VYA WANGA KWA KIASI KIDOGO
·         Mlo kamili unatakiwa uwe na vyakula vya wanga, protini, mafuta, matunda na mboga za majani katika uwiano stahiki.
·         Ni muhimu kupunguza matumizi ya vyakula vya wanga kwa mgonjwa wa kisukari. Kwa kuwa vyakula vya wanga mf mahindi, ngano, mchele, ndizi nk vina kiwango kikubwa cha sukari.
o    Kipimo cha wastani cha vyakula vya wanga ni ukubwa wa ngumi yako katika kila mlo. Mfano kiasi cha ugali unachotakiwa kutumia ni ukubwa wa ngumi yako, vivyo hivyo kwa vyakula vingine kama wali n.k.
·         Pia punguza vyakula vya wanga unavyotumia wakati wa kupata kifungua kinywa kama chapati, mikate n.k.
 3. TUMIA MBOGA ZA MAJANI KWA WINGI ZAIDI PAMOJA NA PROTINI
·         Tumia mboga za majani kwa wingi, hizi zitakufanya ushibe vizuri bila kuongeza kiasi kikubwa cha sukari mwilini. Na pia husaidia kwenye usagaji wa chakula mwilini na kupata choo mara kwa mara.
·         Hakikisha mlo wako pia una vyakula vya protini kama samaki, nyama nk. Vyakula hivi ni muhimu kwa kuwa vinasaidia kujenga mwili. Ni vizuri kutumia hivi vyakula kwa kiasi na siyo kutumia kwa wingi.
 4. PUNGUZA MATUMIZI YA CHUMVI NA MAFUTA MENGI KWENYE CHAKULA
·         Punguza kiasi cha chumvi unachotumia kwenye chakula na epuka kuongeza chumvi wakati wa kula chakula mezani
·         Chumvi husababisha ugonjwa wa shinikizo la damu, na kwa wale wenye ugonjwa wa shinikizo la damu hufanya dawa zisifanye kazi vizuri
·         Ni muhimu kutumia mafuta kwa kiasi kidogo kwenye chakula, kutumia mafuta mengi huongeza kiasi cha mafuta mwilini (unene). Unene hupunguza ufanisi wa insulin mwilini.
·         Wagonjwa wanashauriwa kupunguza vyakula vya kukaangwa kwa kutumia mafuta mengi (deep fried foods) na kutumia zaidi vyakula vilivyoandaliwa kwa kuchemshwa na vilivyowekwa mafuta kidogo.
 5. PUNGUZA NA IKIWEZEKANA ACHA MATUMIZI YA POMBE
·         Matumizi ya pombe ni hatari kwa mgonjwa wa kisukari
·         Pombe kama bia zina kiwango kikubwa cha sukari hivyo husababisha udhibiti wa sukari mwilini kuwa mgumu
·         Matumizi ya pombe kali ni hatari pia kwa kuwa husababisha athari kwa viungo vya mwili kama figo na ini ambavyo pia huathiriwa na ugonjwa wa kisukari.
6. FANYA MAZOEZI YA MWILI NA TUMIA MAJI YA KUTOSHA
·         Ni muhimu kufanya mazoezi walau dakika 30 kila siku, mazoezi yana faida zifuatazo
o    Kuongeza utengenezaji wa insulini
o    Kupunguza unene
o    Kuboresha afya ya mwili pamoja na kudumisha kinga ya mwili
·         Kunywa maji kwa wingi ni muhimu kwa afya hasa wakati wa mazoezi ili kurudisha maji yaliyopotea mwilini
·         Inashauriwa kunywa lita moja na nusu mpaka mbili za maji kwa siku
o    Ushauri huu ni kwa wagonjwa wa kisukari ambao hawajapata madhara ya ugonjwa huu kama shida ya figo au shida ya moyo. Wagonjwa waliokwisha kupata madhara ya ugonjwa wa kisukari watafuata ushauri wa kiasi cha maji kama watakavyoelekezwa na wataalamu wa afya wanaowapatia huduma.
7. UTUNZAJI WA MIGUU
Ugonjwa wa kisukari husababisha ganzi kwenye mwili, hasa miguuni na mikononi. Ganzi hupelekea wagonjwa wa kisukari kupata majeraha hasa ukizingatia hawasikii maumivu hata wakikanyaga moto au msumari.
Majeraha hupona kwa tabu sana kwa wagonjwa wa kisukari, hii inatokana na wingi wa sukari kwenye damu ambayo huchelewesha uponaji wa vidonda na pia husababisha maambukizi ya bakteria kwenye vidonda. Ili kumuepusha mgonjwa na majeraha mambo yafuatayo ni muhimu kuyazingatia;
·         Mgonjwa anashauriwa kuvaa viatu muda wote, kabla ya kuvaa viatu tazama ndani ya viatu kuhakikisha hakuna kitu kinachoweza kuumiza mguu.
·         Viatu bora kwa wagonjwa wa kisukari ni vile vyenye nafasi ya kutosha, vyenye ngozi laini, na kama ni vya wazi viwe na mikanda ya kuvishika miguuni (kandambili hazishauriwi kwa wagonjwa wa kisukari)
o    Viatu virefu ni hatari kwa mgonjwa wa kisukari
·         Kuvaa soksi ni muhimu hata pale mgonjwa anapovaa viatu vya wazi. Soksi ziwe na nafasi ya kutosha na zisiwe zinabana.
·         Ni muhimu kukata kucha na kuhakikisha zinakuwa fupi na safi, kucha ndefu zinaweza kuleta majeraha kwa urahisi.
o    Ukataji wa kucha ufanyike kwa uangalifu ili kuepuka majeraha.
·         Ni muhimu kusafisha miguu kwa sabuni na maji ya moto kisha ikaushe kwa taulo. Usafishaji huu ufanyike kila siku.
·         Kuangalia miguu kila siku kama kuna vidonda, michubuko, wekundu, vipele. Hakikisha umeangalia kila upande na kama huwezi kuangalia kila sehemu omba msaada wa ndugu aliye karibu nawe kukuangalizia.
8. TUMIA DAWA KAMA ULIVYOSHAURIWA NA WATAALAMU
·         Tumia dawa za sukari kadiri ulivyoelekezwa na wataalamu
·         Hakikisha unazo dawa za kutosha hasa pale unapokuwa na safari
·         Hakikisha unatumia pia dawa nyingine ulizopatiwa na daktari wako
9. PIMA KIASI CHA SUKARI MWILINI
·         Tafuta mashine ya kupimia sukari na hakikisha unatunza rekodi ya vipimo vya sukari unavyofanya nyumbani.
·         Pima kiasi cha sukari walau mara moja kwa wiki kujua kiwango cha sukari mwilini. Ni vizuri unapopima sukari upime kabla hujala kitu na masaa mawili baada ya kula (asubuhi,mchana na jioni). Ukiweza kupima kwa mtindo huu utaweza kutambua jinsi mwili wako unavyodhibiti wingi wa sukari mwilini mwako.
·         Mwonyeshe daktari au mtaalamu wa afya rekodi ya vipimo vyako vya sukari ulivyofanyia nyumbani.
10. HAKIKISHA UNAFANYA VIPIMO MARA KWA MARA
·         Ugonjwa wa sukari husababisha shida ya figo, moyo, mishipa ya fahamu na kiharusi (stroke). Hivyo ni muhimu kumkumbusha daktari wako ili ufanye vipimo vifuatavyo mara kwa mara;
o    kipimo cha mkojo kuangalia kama kuna protini, hiki ni kiashiria cha awali cha kuathirika kwa figo
o    kipimo cha damu cha creatinine ambacho huonyesha ufanyaji wa kazi wa figo (creatinine huongezeka iwapo kuna shida ya figo)
o    Kufanya kipimo cha moyo (echocardiography) kwa wagonjwa wenye shinikizo la damu, kuangalia utendaji wa moyo.
o    Kupima macho walau mara moja kwa mwaka, macho ni kati ya viungo vinavyoathiriwa na ugonjwa wa kisukari.



0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2