MAZINGIRA HAYA NI MABAYA,NI MAGUMU NA YANAUMIZA SANA KISAIKOLOJIA,MTU ASIOMBE KABISA KUKOSA UHURU WA KUTOKA NDANI-TOGOLANI | Tarimo Blog

Utangulizi

Nianze ujumbe wangu kwa kutangaza maslahi binafsi. 

Hapa nilipo, hii ni wiki ya pili tunamaliza tukiwa chini ya “total lockdown”. Nchi nzima tunalazimika kukaa ndani muda na hatujui tutatoka lini. Sina hakika na watu wengine waliowahi kuishi mazingira ya aina hii, ila niseme kwa ujasiri kabisa kwamba mazingira haya ni mabaya, ni magumu, na yanaumiza sana kisaikolojia. 

Muda mwingi huwezi kufanya lolote la maana kwa kuwa unakua kama umepoteza "network". Mtu asiombe kabisa kukosa uhuru wa kutoka ndani. Ninapingana kwa 100% na kila ambaye anaishawishi, anaishauri, au anailazimisha serikali kutangaza karantine kama nchi nyingine au anailaumu kwa kutokufanya hivyo.

Nini msingi wa hoja yangu?
Labda nieleze kwa kifupi nini maana ya kuwa kwenye karantini katika uhalisia ili kuweka ninachoongea kwenye muktadha:

1. Wazazi, watoto na munaoishi nao munashinda mukiwa mumejifungia ndani: usiku unakuja, asubuhi inafika, munaaendelea na zoezi kama jana. Mbaya zaidi hamujui zoezi hili litakwisha lini. Wakati mwingine munasahau siku au tarehe maana hakuna matukio yanayowakumbusha. Serikali inasema inaweza kuwa hivi hadi miezi 6.

2. Haijalishi munakokuita nyumbani au ndani kukoje kwa maana ya ukubwa/udogo, ubaya/uzuri na kuna nini cha kufurahisha au kufanya: munazunguka humohumo mchana na usiku.

3. Munatoka ndani mara moja au mbili kwa wiki kwenda kutafuta mahitaji ya lazima. Na mahitaji ya lazima ni chakula na madawa maana maduka ya mahitaji mengine yamefungwa. Munashauriwa kama inawezekana muagize vyakula online.

4. Wakati mwingine vitu vya lazima hakuna madukani/supermarkets maana kutokana na hofu, watu wananunua kwa wingi hivyo vinakwisha.

5. Ukifika supermarket mnapanga foleni ndefu ya kuingia ndani kwa vile mnatakiwa muwe umbali wa mita 2 kati ya mtu na mtu na hamutakiwi kuingia wengi kwa wakati mmoja ili msisongamane. Unaweza kufika ndani unakosa unachotaka.

6. Kwa anayeweza, munaruhusiwa kutoka nje mara moja kwa siku kufanya zoezi moja (kutembea au kukimbia) na uwe mwenyewe au na mtu wa familia yako maana hakuna kukutana zaidi ya watu wawili.

7. Makazi mengi hayana viwanja vya nje kama kwetu Afrika maana nyumba zimejengwa kwa mipango na kubana nafasi. Mara nyingi, nje ya mlango ni bararaba ya mtaa.

8. Sheria imepitishwa na bunge kwamba ukikamatwa kwenye mkusanyiko au unazurura unaweza kutozwa faini na polisi ya hadi milioni tatu za Tanzania (zile faini za papo kwa hapo kama za makosa ya barabarani)

Unajua kwa nini wanaweza kufanya haya?
Wenzetu wanapochukua hatua hizi za kukaa ndani ni kwa sababu mazingira yao yanaruhusu ya yameandaliwa hivyo. Kwa mfano:

9. Wao kukaa ndani sio jambo geni. Maisha yao kwa sehemu kubwa ni ya kibinafsi. Watu wanakaa ndani muda mwingi maana yale maisha ya kijamaa/kijamii wameyaacha. Munaweza kuiishi milango imetazamana na jirani zako lakini musisalimiane hata munapogongana mukitoka au kuingia ndani. Unaweza usimjue jirani yako munayetazamana au kutengwa na ukuta kua ni nani, anafanya nini, nk. Huku ndiko tumeiga msemo wa “mind your own business” na “I don’t care what yu think about me” na tunadhani ni maendeleo.

10. Nchi za Ulaya zina msimu wa baridi kuanzia mwezi wa 10 na wa 11 hadi mwishoni mwa mwezi wa tatu. Kipindi hiki hali ya hewa inaweza kua mbaya muda mwingi sababu ya upepo mkali, mvua nyingi, baridi ni kali, na kunaweza kuwa na barafu. Giza linakua muda mrefu kuliko mchana. Kuna kipindi linaanza kuingia saa tisa jioni na linaendelea hadi kesho yake saa mbili asubuhi. Hivyo mchana kwa maana ya mwanga unaweza kuwa kama masaa 6 hadi 8 tu. Kwa jumla, mazingira hayaruhusu kukaa nje wala kutembea hivyo kama mtu hana anapolazimika kwenda basi muda mwingi ni kukaa ndani.

11. Nyumba za wenzetu hazijengwi kienyeji kama sisi ambapo kila mtu anajijengea atakavyo na atakapo. Nyumba zinajengwa na makampuni au na serikali kwa mipango na viwango maalumu. Kutokana na hali ya hewa ya baridi na majanga kama vimbunga, nyumba zinajengwa zikiwa na uwezo wa kustahimili baridi na upepo mkali. Madirisha yana vioo viwili; ukuta wa nyumba una kuta mbili na katikati unajazwa vitu vya kupunguza hewa ya baridi; paa linadhibitiwa kiasi kwamba mvu akinyesha unaweza usijue iwapo hujatazama nje.

12. Kila nyumba ina maji yasiyokatika; ina bomba la gesi linaloingia ndani kama maji; ina umeme wa uhakika usiokatika. Nyumba zisizo na mabomba ya gesi basi umeme ndio unatumika kupikia na kwenye mifumo ya kupasha maji na nyumba joto.

13. Kila nyumba inapojengwa, inaingiziwa waya (connection) ya TV, simu ya landline na internet. Huduma hizi ni za uhakika kwa kila nyumba labda uwe tu huwezi kulipia bills. Internet ni rahisi sana hivyo kwa gharama ambayo hapa kwetu mtu anatumia kununua bando la GB kama ya 20, kwao unapata internet ya kutumia vifaa zaidi ya kumi kwa wakati mmoja (simu, computers, smart tv, tablets) usiku na mchana mwezi mzima mukifanya kila munachotaka kwenye internet bila kupimiwa.

14. Huduma za maji, umeme, internet, gesi, simu, tv hazikatiki na hazikatwi kienyeji hata ukishindwa kulipa bills. Tarehe ya kulipia ikifika huna pesa kwenye akaunti utafutatiliwa na kukumbushwa kwanza kwa muda ingawa ukichelewa sana utapigwa faini ya kukuumiza.

15. Unaweza kuagiza KITU CHOCHOTE online (kwa kupiga simu au internet) na kikaletwa hadi mlangoni iwe dawa, chakula, nguo, viatu, mashuka, vinywaji, nk.

16. Ukiumwa unawasiliana na daktari kituo cha afya uliposajiliwa kabla ya uamuzi wa kwenda iwapo sio matatizo ya dharura. Matatizo yote ya dharura ukipiga simu ndani ya dakika chache ambulance iko mlangoni na ukichelewa kufungua wanaweza kuvunja mlango wakaingia wakidhani umezidiwa.

17. Ukipata tatizo kama kupigwa na mke au mume, kuingiliwa na wezi, au mtoto kupigwa na mzazi; ukipiga simu ndani ya dakika chache polisi wako mlangoni.

Haya ndio mazingira ya wenzetu yanayowaruhusu kutangaza TOTAL LOCKDOWN au KARANTINI kirahisi kama vile wanatangaza mshahara kupanda. Wanaposema watu wakae ndani wasitoke, wana hakika kwa zaidi ya 95% mazingira ya kila mtu yanamruhusu kukaa ndani na akaishi bila matatizo makubwa. Pia, kwa kuwa wana mifumo inayofanya kazi na makazi yamepangika, kwa sehemu kubwa wanajua kila mtu anayefanya kazi (binafsi au kijiajiri), kipato chake, na anaishi wapi. Hivyo serikali wanaweza kutangaza kutoa ruzuku za kuishi kwa kiwango fulani kwa kila raia au mfanyakazi kipindi hiki cha mlipuko na watu wakazipata bila mizengwe.

Sasa linganisha mazingira haya yao nay a kwetu.

18. Sisi wananchi wengi hawana uwezo wa kununua chakula cha kesho. Inamlazimu mtu kutoka ndani kila siku ili angalau aweze kuweka mlo mezani.

19. Sisi tumezoea kwenda dukani/sokoni kila siku au mara kadhaa kwa wiki kununua kila kitu kidogokigogo: tubamia, kaunga, tudagaa, tunyanya, tuvitunguu, tumchicha, nk.

20. Sisi tuna familia nyingi hazijui umeme ni nini. Hata walionao, hauna uhakika wa kuwaka kila siku. Kwa wenzetu umeme kukatika kwenye nyumba kwa nusu dakika tu ni moja ya miujiza kwa mwaka labda kuwe na majanga kama vimbunga, mafuriko, nk.

21. Sisi watu wengi hawana maji ya bomba ndani. Wengi inawalazimu kila siku kwenda kuteka maji mtoni, bombani, kisimani, chemchem, bwawani au hata kuomba kwa jirani mwenye uwezo. Wengi inawalazimu kutembea umbali mrefu kupata maji.

22. Makazi yetu hayana anuani za kueleweka hivyo hatuwezi kuwa na huduma za kununua vitu online na kushushiwa nyumbani hata kama tukitaka.

23. Wengi wetu tunaishi kwenye nyumba mbovu, mbaya, hazina mvuto, na wengine ni ndogo sana ukilinganisha na ukubwa wa familia. Pia wote nchi nzima tunaishi na mifugo kadhaa ndani ya nyumba. Kama sio mbuzi, kuku, kondoo au ng’ombe, basi tunaishi na mende, panya, viroboto, nzi na mbu.

24. Hatuna maduka makubwa (supermarkets) kila mahali karibu na watu ambapo utasema watapata mahitaji ya lazima kwa urahisi wakiwa kwenye karantini. Wengi hutembea au kusafiri mbali kununua chakula madukani au sokoni

25. Wananchi wengi wanatumia mkaa, kuni au mafuta ya taa kupikia. Wengine wakitaka kuwasha moto lazima wakaombe kiberiti au kaa la moto kwa jirani.

26. Wengi wetu hatuna vyoo vya ndani na vya nje havitamaniki.

Sasa niambie, serikali ikitangaza karantini ya kumtaka kila mtu akae ndani na asichangamane hata na jirani yake tutaishije kwenye mazingira haya? Tutaweza kuishi hivyo hata kwa wiki moja? Na kama tukilazimika kwa kiboko kama kule Kenya, unadhani ni madhara kiasi gani tutapata?

Mwisho
Msukumo wa kuishauri serikali kutangaza total lockdown, kama ilivyo kwa misukumo mingine kwenye janga hili, inatoka kwa kundi dogo la watu wenye uwezo (middle class). Duniani kote kundi hili hujisahau na kudhani kila mtu ana maisha kama yao. Lina kiwango kikubwa sana cha ubinafsi na wakati mwingine wanasahau kabisa kwamba hata ndugu zao wa karibu hawana uwezo walionao wao. Lakini ukweli ni kwamba kwa watanzania walio wengi karantini ya kututaka kukaa ndani ni janga kubwa mara nyingi kuliko Covid-19. Wanaoshawishi hatua hii wakumbuke kwanza kijijini kwao walikotoka wao au wazazi wao kukoje kabla hawajashauri total lockdown.

Serikali ichukue kila tahadhari na hatua wanazoshauriwa na wataalamu kuhusu kuzuia au kupunguza maambukizi ya Covid-19. Tusikilize wataalamu ni kwa jinsi gani tunaweza kuwakinga watu ambao wakipata maambukizi watadhuruka zaidi (wazee, wenye magonjwa ya kupua, na wenye chronic diseases). Ila isikubali wala kusikiliza ushawishi wa mtu, watu, taasisi, au nchi yoyote kuilazimisha kutangaza karantini katika hatua ya sasa.

Karantini ya kuwataka watu kukaa nyumbani (tena kwa muda usiojulikana) ni njia isiyofaa kwa wananchi wetu. Itakua na madhara makubwa sana kiafya, kijamii, na kimaisha iwapo itachukuliwa katika hatua hii. ndio tuko mwanzoni kabisa mwa maambukizi na hatuna hata mgonjwa mmoja aliye na hali mbaya. Kutangaza lockdown itakua ni sawa na kumkimbia mbwa kwa kuingia kwenye zoo walipo simba na chui huku ukidhani unatafuta kinga.

Kwa ngazi ya maambukizi tuliyopo sisi (ukilinganisha na nchi zilizoathirika sana na tabia ya mlipuko), bado tunaweza kuwa na maambukizi hadi miezi 5 au 6 kuanzia sasa. Njia ya lockdown naweza kusaidia kama suluhisho la mwisho kabisa wakati maambukizi yamezidi uwezo wa kukabiliana nayo: kwa maana ya kwamba watu wengi walioambukizwa watakua na hali mbaya kiafya (critical conditions). Ikifika hatua hiyo, mlipuko utakua umefika kileleni na kukaribia kushuka hivyo muda wa watu kukaa ndani utakua ni mfupi na madhara yatakua kidogo. Kitu cha kushauri serikali kwa sasa ni namna ya kuandaa mikakati ya nini cha kufanya iwapo tutalazimika kufikia hatua hiyo (worse case scenario). Ukiweka watu ndani sasa wakati hujui utawaweka kwa muda gani na huna uwezo wa kuwahudumia, madhara yake ni makubwa sana.

Pia tukumbuke sio lazima kila nchi ifikie hatua ya kua na vifo vingi kama tunavyoona Italy, Spain na kwingine. Ni makosa kuchukulia kinachotokea kwenye nchi hizo kama kielelezo na sababu ya kujengea hofu na taharuki katika kufanya maamuzi.

MM Togolani (mmtogolani@gmail.com)
Mwathirika wa "Total Lockdown"

------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Ziada na hitimisho
Kwenye uzi huu nimefafanua na nimejibu hoja kinzani na maswali ya wachangiaji kadiri nilivyoweza. Kwa kufanya hivyo nimefafanua mambo mengine ambayo sikuyataja kwenye makala yangu. Kwa ujumla ninaweza kuhitimisha hoja namaswali yao kama ifuatavyo:

Nikisoma maoni, matusi, maonyo, hofu na taahadhari ya wanaotamani serikali itangaze total lockdown, hakuna hata mmoja anayetoa suluhisho au mbinu ya utekelezaje wake. Hakuna anayetoa data yoyote kiuchumi, kijamii, afya, nk. Hawatuambii watanzania wasio na maji, ajira, umeme, nk ambao wataathirika kuanzia siku ya kwanza ni asilimia ngapi na watasidikaje. Hoja yao ni moja tu, HOFU na watu wengi watakufa tusipotangaza Lockdown sasa. Hakuna scientific argument yoyote wanayotoa yenye ushawishi au theory and practices za crisis management or outbreaks control/response.

Kauli zao zinaonesha kifo kinachotisha ni cha Corona pekee. Vifo vitokanavyo na njaa, malaria, kipindupindu, kuhara, na utapiamlo (baadhi ya maradhi ambayo yatakumba wengi kukiwa na lockdown ya muda mrefu) havitishi wala sio tatizo. Tatizo ni Corona tu kwa madai kwamba tutakufa kama Italy na Spain. Wakati hofu hizi ni za msingi ila hazitakiwi kuwa msingi wa maamuzi na kufikiria kwetu.

Watu hawa hawaelevi bado inamaanisha nini hasa kuwa kwenye total lockdown. Hawatazami multiplying effect ya lockdown. Hawaelewi makampuni mengi yatafungwa na wafanyakazi watapoteza kazi. Hakuna mwajiri ataendelea kulipa mshahara watu wasiofanya kazi na yeye hazalishi. Hata makampuni yatakayooperate yatapunguza wafanyakazi kwa sehemu kubwa maana hakuna biashara. Nimeongea na wafanyakazi kadhaa wa sekta ya utalii wako majumbani hawana kazi na hawajui kazi itarejea lini. Waliobahatika kubaki na ajira wengine wameahidiwa wanalipwa nusu ya mshahara kwa miezi 3 au 5 wakati kisha maamuzi mengine yatafuata.

Kinachotokea na kitakachotokea zaidi, uwezo wa serikali kukusanya kodi utakua mdogo maana hakuna biashara; uzalishaji unapungua; PAYE itapungua maana watu wamepoteza kazi. Nchi yetu bado inategemea makusanyo ya kila mwezi kugharamia mahitaji muhim ya nchi kama kulipa wafanyakazi, kununua madawa, ulinzi na usalama, na kazi za utawala wa nchi.

Hivyo unapoishauri serikali kukimbilia total lockdown sasa na kwa muda usiojulikana (maana ndio tuko asubuhi mwa mlipuko), tuiambie pia itaendeshaje nchi. Kama hatuelewi complexity ya lockdown basi tuendelee tu kuisilikiliza kwenye vyombo vya habari kuliko kujiona sisi ni wataalamu wa utekelezahi wa total lockdown. Nirudie tena, huwezi kukimbia kung'atwa na mbwa (Corona) kwa kukimbilia walipo chui na simba (madhara ya total lockdown).

Namishukuruni waliosoma, waliochangia, waliokosoa, waliosahihisha, walioniita mjinga, na hata walionitukana. Wote wametumia uhuru weo kadiri ilivyowapendeza. Bado kuna mambo mengi ya muhim ya kuchambua na kujadili kuhusu Covid-19.

Mubarikiwe.

MM Togolani.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2