Wafanyakazi STAMICO wapata mafunzo dhidi ya Corona | Tarimo Blog

 Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeungana na taasisi nyingine za umma na binafsi nchini katika kuwaasa wafanyakazi wake kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID -19).

Katika kufanikisha hilo, uongozi wa STAMICO uliandaa mafunzo ya siku moja yaliyofanyika kwenye viunga vya wazi vya ofisi hiyo  kwa ajili ya wafanyakazi wake waliopo Dar es Salaam ambapo, pamoja na mambo mengine, walihimizwa kujilinda na maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19 na kutakiwa kuripoti kwenye vituo vya afya vilivyoteuliwa mara waonapo dalili za ugonjwa huo.

Wafanyakazi hao waliambiwa kuwa kupata huduma ya afya mapema kutawaepusha na athari kubwa zinazoweza kutokea kutokana na maambukizi.

Taarifa iliyotolewa na STAMICO imesema mafunzo hayo yalilenga pia kuwatahadharisha wafanyakazi dhidi ya magonjwa mengine yanayoambukiza kwa njia ya virusi kama homa ya ini (Hepatitis B) na Ukimwi (HIV-AIDS).

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Bahati Mwasse, amenukuliwa na taarifa hiyo akisema kuwa maeneo ya kazini ndipo wafanyakazi wanapokutana kwa muda mrefu zaidi na hivyo kuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa hayo.

“Dkt. Mwasse aliwahimiza wafanyakazi wa STAMICO kuwa makini na kufuata maelekezo yanayotolewa na viongozi wetu wa Serikali, kama vile kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono mara kwa mara na kuendelea kufanya kazi kwa umakini mkubwa ili waweze kujikinga wao (nguvu kazi ya Shirika) na familia zao,” ilisema taarifa hiyo.

Miongoni mwa hatua ambazo watumishi wa STAMICO na wageni wametakiwa kuzingatia ili kupunguza uwezekano wa maambukizi ya ugonjwa wa Corona ni pamoja na kunawa mikono na sabuni, maji tiririka, kutumia vitakasa mikono (sanitizer) na kupima joto kwa kutumia thermal scanner waingiapo ofisini.

Hatua nyingine ni kuandaa mafunzo mbalimbali ya jinsi ya kujikinga na magonjwa yatokanayo na virusi, imeeleza taarifa hiyo.

 Aidha, kaimu mkurugenzi huyo ameahidi kuendelea kudhibiti maambukizi sehemu ya kazi kwa kuanza zoezi la kusafisha vitasa/milango kwa kutumia dawa (chlorine), kufanya upuliziaji (fumigation) na kuwachukulia hatua wale  watakaopuuzia zoezi hili la kujikinga dhidi ya maambukizi.

Katika mafunzo hayo yaliyoendeshwa na wataalam, Dkt Macha Njile na Dkt Ally Juma kutoka Kitengo Maalumu cha Kuzuia Magonjwa Sugu Yanayoambukizwa kilicho chini Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, mada mbalimbali juu ya magonjwa yanayosababishwa na virusi zilitolewa. Mada hizo zilihusisha pia maelezo kuhusu jinsi magonjwa hayo yanavyoenezwa, dalili zake na namna ya kujikinga.

STAMICO imekuwa kinara katika utoaji wa mafunzo mahali pa kazi hususan yanayohusu afya na usalama wa wafanyakazi ambapo jumla ya wafanyakazi 48 waliweza kupatiwa mafunzo ya ugonjwa wa Corona na magonjwa mengine ya virusi yanayoambukiza.

Aidha, wafanyakazi walipata pia fursa ya kupima afya kujua hali zao na wengine kupatiwa chanjo ya kwanza ya kujikinga na homa ya ini.

Awali mafunzo ya kujikinga na virusi vya Corona yalifanyika kwa watumishi ya Shirika walioko mgodini Kiwira pamoja wale walioko ofisi za Dodoma.
  Kaimu Mkurugezi Mkuu wa STAMICO Dr Venance Mwasse (Kulia) akichukuliwa kipimo kwa ajili ya kuangalia virusi vinavyosababisha Homa ya ini (Hepatitis B) baada ya kupata mafunzo ya siku ya moja ya kujenga uwezo wa kukabiliana na maambukizi ya Ugonjwa  wa COVID 19 na magonjwa mengine ikiwemo yanayoambukiza kwa njia ya virusi kama homa ya ini (Hepatitis B) na Ukimwi (HIV-AIDS). Mafunzo hayo ya siku moja yalitolewana maofisa kutoka Wizara ya Afya na  yaliyofanyika kwenye viunga vya wazi vya ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.
 Mmoja wa wafanyakazi wa STAMICO Bibi Pili Athuman (Kulia) akichukuliwa kipimo kwa ajili ya kuangalia virusi vinavyosababisha Homa ya ini (Hepatitis B) baada ya kupata mafunzo ya siku ya moja ya kujenga uwezo wa kukabiliana na maambukizi ya Ugonjwa  wa COVID 19 na magonjwa mengine ikiwemo yanayoambukiza kwa njia ya virusi kama homa ya ini (Hepatitis B) na Ukimwi (HIV-AIDS). Mafunzo hayo ya siku moja yalitolewana maofisa kutoka Wizara ya Afya na  yaliyofanyika kwenye viunga vya wazi vya ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.

 Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wakiongozzwa na Kaimu Mkurugezi Mkuu wa STAMICO Dr Venance Mwasse (alievaa koti jeusi) wakifuatilia kwa umakini mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo wa kukabiliana na maambukizi ya Ugonjwa  wa COVID 19 na magonjwa mengine ikiwemo yanayoambukiza kwa njia ya virusi kama homa ya ini (Hepatitis B) na Ukimwi (HIV-AIDS). Mafunzo hayo ya siku moja yalitolewana maofisa kutoka Wizara ya Afya na  yaliyofanyika kwenye viunga vya wazi vya ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2