Na Mwandishi wetu, Uvinza.
Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe amesema ipo haja kwa watu waliovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Uwekezaji yanayomilikiwa na Kituo hicho kuondoka ili kupisha shughuli zilizotengwa kwa matumizi ya maeneo hayo.
Maeneo hayo yaliyovamiwa tayari yametengwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo kikubwa cha michikichi na kumilikishwa TIC ikiwepo shamba Na. 205 lenye ukubwa wa hekta 3,249.76 lililopo eneo la Basanza na Shamba Na. 206 lenye ukubwa wa hekta 10,529.86 yote yakiwa Wilayani Uvinza, MkoaniKigoma.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga akifafanua jambo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe aliyetembelea kituo hicho hivi karibuni.
Mashamba hayo yametengwa mahsusi kwa ajili ya Uwekezaji wa kilimo cha zao la michikichi kwa ajili ya kuzalisha mafuta ya kula ya mawese ili kuondokana na changamoto ya kuagiza mafuta nje ya nchi, kwani takwimu za wizara ya Kilimo zinaonyesha kuwa Tanzania inaagiza tani laki nne (400,000) za mafuta ya mawese huku ikitumia zaidi ya shilingi bilioni 600 kila mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi ili kufidia pengo la uhaba wa bidhaa hiyo nchini.
Mpango wa sasa wa nchi ni kuepukana na kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi ambayo pamoja na kutumia gharama kubwa lakini bado usalama wake unatiliwa shaka na pia hutumia fedha za kigeni ambazo zingeweza kufanya mambo mengine ya msingi.
Serikali kwa kuliona hilo imeongeza zao la michikikichi kuwa ni moja wapo ya mazao ya kimkakati ambapo mazao mengine ni pamba, chai, kahawa, korosho, katani na tumbaku.
Mwambe alifanya ziara Mkoani Kigoma na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa huo Brigedia Generali Mstaafu Emmanuel Maganga na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza ambako mashamba hayo yanapatikana Bi. Mwanamvua Mrindoko ili kupanga mikakati ya kuwaondoa wavamizi pamoja na kulinda maeneo hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe pamoja na Maafisa wengine wa Kituo hicho pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
"Nimekuja Kigoma kwa ajili ya kuangalia na kufanya majadiliano na uongozi wa Mkoa na Wilaya juu ya namna bora ya kulinda mashamba yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya Uwekezaji, lakini Wananchi wameingia na kufanya shughuli za kibinaadam jambo ambalo si afya katika kufanikisha uwekezaji, haya maeneo yalishatengwa na Serikali kwa ajili ya Uwekezaji, hivyo waliovamia ni wakati wao sasa kuondoka" alisema Mwambe.
Aidha amewataka Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kuwekeza katika maeneo hayo ya uzalishaji wa michikichi kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta ya kula.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga alisema kazi iliyopo sasa ni wao kuongeza ulinzi kwenye maeneo hayo yasivamiwe zaidi jambo ambalo alisema linaathiri uwekezaji katika Mkoa wa Kigoma.
Aidha amewataka waliovamia maeneo ya uwekezaji Mkoani humo kuondoka, n huku akisisitiza kuwawenye nia ya kuingia wasitishe mara moja kwa maana eneo hilo lina mwenyewe.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuondoka katika maeneo hayo na kuelekeza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuweka matangazo maalum ya mabango yenye kusisitiza kwamba eneo hilo lina mmiliki halali ambaye ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania.
"Sisi Mkoa tunamtambua mmiliki halali wa maeneo hilo ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kazi yetu ni kuyalinda, sasa TIC mlete mabango yenu tuyabandike ili Wananchi wajue eneo hilo lina mwenyewe" alisema Maganga.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Bi. Mwanamvua Mrindoko alisema wanaandaa mpango wa kutoa elimu kwa wakazi waliovamia na kuweka makazi na shughuli za uzalishaji kwenye eneo hilo la uwekezaji ili wapishe shughuli za uwekezaji kwa maendeleo ya Uvinza, Kigoma na Taifa kwa ujumla.
"Ni muhimu wakazi hawa wakaondoka katika maeneo ya Serikali ambayo yametengwa kwa uwekezaji na kuacha kuendelea kuishi humo walikovamia. Wilaya yetu ya Uvinza tunataka Wawekezaji watakaoanzisha miradi mikubwa ikiwemo kilimo cha michikichi sambamba na kiwanda cha kuzalisha mafuta. Miradi hii inatarajiwa kuleta mapinduzi chanya ya uchumi (ajira, pato) hatua itakayosaidia kutufanya kukua.
"Tutawaelimisha tu Wananchi waweze kuondoka kwa amani na utulivu kwani mashamba hayo yamelenga kuleta faida kubwa za kiuchumi, kwa Taifa, Mkoa, Wilaya, Vijiji na Mwananchi mmoja mmoja" alisema Bi. Mrindoko.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment