Na WAMJW – Dar es Salaam
05/05/2020 Vifo vya watoto wachanga wenye umri wa chini ya siku 28 vimepungua kutoka 25 kwa kila vizazi hai 1000 kwa mwaka 2015/16 na kufikia saba kwa kila vizazi hai 1000 kwa mwezi Machi mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo jijini jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akipokea msaada wa vifaa kinga, mabango,vipeperushi na vifaa vya kutoa elimu kwa Umma kuhusu ugonjwa wa Corona kutoka kwa Benki ya Absa Tanzania Ltd na Shirika la UNESCO.
Waziri Ummy alisema kupungua kwa vifo hivyo kumetokana na jitihada zilizofanywa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuimarisha sekta ya afya hapa nchini hii ni pamoja na kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya, upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba.
“Kwa namna ya kipekee niwapongeza na kuwashukuru wakunga wote hapa nchini kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kila siku ya kuwahudumia akina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano”,.
“Pamoja na kuwa maambukizi ya Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) yapo na watu wanaumwa ugonjwa huu, lakini tusisahau kuwa kina mama wajawazito wanajifungua kila siku na wakunga wanaendelea kuwahudumia kinamama hawa”, alisisitiza Waziri Ummy.
Waziri huyo aliwahakikishia wananchi kuwa pamoja na kuwa ugonjwa wa Corona upo huduma zingine zinaendelea kama kawaida katika vituo vituo vyote vya kutolea huduma za afya zikiwemo huduma za kliniki za akina mama wajawazito na watoto, upimaji wa magonjwa mbalimbali pamoja na upasuaji.
“Ninawashukuru wadau mliotoa vifaa hivi, ninawaomba wadau wengine waendelee kuiunga mkono Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Corona ambao ni janga la Dunia”,.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Mabula Mchembe alisema vifaa hivyo vitaboresha utoaji wa huduma za afya katika vituo vilivyopo Dar es Salaam pamoja na maeneo mengine nchini.
“Ninawahakikishia wananchi pamoja na wadau mliotoa vifaa hivi kuwa vitatumiwa na wataalamu wetu katika kutoa huduma mbalimbali za matibabu kwa wagonjwa wanaotibiwa katika vituo vyetu vya afya”, alisema Prof. Mchembe.
Akikabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa Rasiliamali watu wa benki ya Absa Tanzania Ltd. Patrick Foya alisema vifaa kinga walivyovitoa vyenye thamani ya milioni 20 ambavyo ni glovu, barakoa na vitakasa mikono vitawasaidia watoa huduma za afya wakati wanawahudumia wagonjwa.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungumza akipokea msaada wa vifaa kinga,vipeperushi,mabango na vifaa vya kutoa elimu kwa umma kwa ajili ya watoa huduma za afya na waandishi wa habari nchini
Waziri Ummy Mwalimu ameishukuru UNESCO na bank ya Absa kwa msaada wao.Kutoka kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe na kulia kwa Waziri ni Mkurugenzi wa Rasiliamali watu kutoka banki ya Absa Tanzania Ltd. Patrick Foya
Mwakilishi Mkazi wa UNESCO nchini Tanzania, Tirso Dos Santos akikabidhi msaada wa vifaa kinga pamoja na vifaa vya elimu kwa umma kwa ajili ya waandishi wa habari
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto-Idara Kuu Afya Prof.Mabula Mchembe akiongea wakati wa kupokea msaada kutoka UNESCO na Benki ya Absa Tanzania Ltd
Mwakilishi Mkazi wa UNESCO nchini Tanzania, Tirso Dos Santos akiongea wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa Wizara ya Afya
Mkurugenzi wa Rasiliamali watu kutoka banki ya Absa Tanzania Ltd. Patrick Foya akiongea wakati wa kukabidi vifaa kinga ambavyo vitapelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma nchini
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment