Asilimia 25 ya ushuru kwenye chupa za kioo àutavuruga biashara soko la Afrika Mashariki | Tarimo Blog

Nchi ya Kenya imeweka asilimia 25% ya ushuru wa bidhaa za chupa za kioo (glass bottles) zinazotengezwa na kampuni ya kioo Limited kutoka Tanzania.

Kioo Limited ni kampuni ya kizalendo ambayo imekuwa kwa muda mrefu ikizalisha bidhaa za chupa za kioo na kuuza ndani na nje ya Tanzania.

Kampuni hii imekuwa ikibadili malighafi zinazopatikana hapahapa nchini na kuzigeuza kuwa bidhaa zenye thamani kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa na Rais wa awamu ya tano, Dk. John Pombe Magufuli katika hotuba zake mbalimbali kuhusu Tanzania ya viwanda.

Kioo ni moja ya makampuni makubwa ya kutengeneza chupa za kioo kwa ajili ya vinjwaji baridi kama soda, juice, bia, pombe kali na kwa ajili ya vyakula mbalimbali kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kati.

Mitambo ya Kioo Limited ni ya kisasa zaidi na yenye uwezo mkubwa sana katika ukanda mzima wa Afrika ambayo inauwezo wa kuzalisha bidhaa bora za chupa na kutoa fursa kwa wateja wake kupunguza gharama za uzalishaji mali kwa kutumia bidhaa zake,kwa muda wa miaka mitano iliyopita kampuni imeweza kuwekeza  vya kutosha kwenye mitambo yake ili kuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa bora kwa wateja wake.

Kampuni hii imeajiri wafanyakazi zaidi ya 600 kwa  ajira za moja kwa moja na zingine nyingi zisizo za moja kwa moja kwa wafanyakazi wanaosaidia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kiwandani.

Kwa sasa mitambo yake inauwezo wa kuzalisha tani 400 za bidhaa za chupa za kioo kwa siku na inauza  asilimia 60% ya bidhaa hizo nje ya nchi na kutosheza soko la ndani kwa asilimia 100% ya bidhaa za chupa kwa viwanda vya ndani ya nchi vinavyo tumia bidhaa hizi.

Kampuni ya kioo Limited ni miongoni mwa kampuni chache zinazo uza nje bidhaa katika sekta ya uzalishaji hapa nchini, na imekuwa ikiingizia Nchi fedha nyingi za kigeni.

Hivi karibuni Nchi ya Kenya ilifanya mabadiliko kwenye Sheria ya Biashara ya mwaka 2020 ikiwa ni mabadiliko Sheria ya Biashara ya mwaka 2015 ya ushuru wa forodha kwa kuweka ushuru wa forodha wa asilimia 25% kwa bidhaa za chupa zinazoingia nchini humo kuanzia Machi mwaka 2020.

Chini ya sheria hiyo ya ushuru huo wa forodha hakuna msamaha wowote uliowekwa kwa bidhaa zinazouzwa nchini humo kutoka kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ushuru huo wa bidhaa kwa asilimia 25% utahusu pia bidhaa za chupa zinazoingizwa nchini Kenya kutoka Tanzania.

Ni dhahiri mabadiliko hayo yatasababisha ongezeko kwa gharama za bidhaa za chupa zinazoagizwa kutoka nje ya Kenya ikilinganisha na bidhaa za chupa za kioo zinazozalishwa na viwanda vya nchini Kenya.

Kampuni ya Kioo inauza bidhaa zake nchini Kenya hivyo ushuru huo wa asilimia 25% utasababisha bidhaa za chupa ya kioo kutoka Tanzania kushindwa kushindana kwenye soko la Kenya kwani bidhaa hiyo ya chupa inayotengenezwa Kenya itakuwa rahisi kuliko zile zinazoagizwa kutoka Tanznia.

Mwingiliano au utengamano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unajumuisha kuanzishwa kwa Ushuru wa Pamoja na soko la Pamoja.  vifungu vya 75 na 76 vya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki vilihusisha kuanzishwa kwa ushuru wa pamoja na soko la pamoja.

Ushuru wa Pamoja ndiyo msingi mkuu wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) na ilianzishwa chini ya protokali ya Ushuru wa Pamoja.

Chini ya Itifaki ya Ushuru wa Pamoja nchi wanachama waJumuiya ya Afrika ya Mashariki  (EAC) zinapaswa kuimarisha biashara baina yao na miongoni mwa makubaliano ni kuondoa tozo za ndani na tozo mbalimbali na kupunguza vizuizi kwaajili ya kutengeneza mazingira bora ya biashara kwa ukanda huo.

Soko la pamoja lilianzishwa chini ya protokali ya kuanzishwa kwa Soko la Pamoja kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki lengo likiwa ni kurahisisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi wanachama kwa kutoa ushuru wa kuingizwa kwa bidhaa, fursa za kazi, huduma na  mitaji kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hatua ya Kenya kuweka asilimia 25% kwa bidhaa za chupa za kioo zinazotoka Tanzania inapingana na vifungu vya sheria ya mkataba na Itifaki ya Ushuru wa Pamoja.

Kenya ni soko muhimu sana kwa bidhaa za chupa za kioo zinazozalishwa na Kampuni ya Kioo Limited  hivyo kwa kuweka kiwango hicho cha ushuru wa chupa za kioo zinazotoka Kioo Limited, Tanzania kutamaanisha kwamba bidhaa kutoka Tanzania zinakuwa ghali zaidi ya zile zinazozalishwa nchini Kenya hali ambayo itasababisha viwanda vinavyo tumia bidhaa za chupa za kioo vya nchini Kenya  kutoagiza tena chupa za kioo kutoka Tanzania  kwani zitashindwa kushindana kwenye soko.

Hali hii itaathiri sana wanunuzi wa chupa za kioo kwani watalazimika kutegemea chupa za kioo zinazozalishwa nchini Kenya pekee ambako kuna wazalishaji wawili tu wa chupa za kioo ambao hata hivyo hawawezi kutosheleza mahitaji yote ya viwanda vya nchini Kenya.

Tanzania na Kenya zina usawa linapokuja suala la mfumo wa bei wa bidhaa na fursa za masoko. Wakati Tanzania kuna gesi asilia Kenya kuna magadi(Soda Ash) bidhaa ambazo zinaziweka nchi hizi kwenye nafasi nzuri ya kupunguza gharama za uzalishaji kwenye mataifa haya.aa

Kioo Limited inalipeleka suala hili kwenye mamlaka husika Tanzania na pia kwenye mahakama ya haki ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuingilia suala hili haraka kwani wakati soko la bidhaa zake limeathiriwa kutokana na janga la Covid 19, ushuru huo wa bidhaa ni kama umetonesha kidonda.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2