UKISTAAJABU YA WASANII UTAKUTANA NA YA WANASIASA | Tarimo Blog


Charles James, Michuzi TV

UNAFIKI! Ndiyo. Kwanini nisiuite unafiki ilihali jana walipendana na kuliana yamini kwamba hawatogombana wala kuachana lakini sasa kutwa kurushiana maneno kwenye Televisheni baada ya kugombana.

Wapo wale ambao jana waliitana wanafiki, wazandiki. Mwingine akasema fulani anakwamisha michongo yangu, ila leo wanaenda wote Kidimbwi kula bata. Unafiki.

Siyo siasa, maisha ya kawaida wala mapenzi. Kote huko ni maeneo yenye kuonesha unafiki wetu sisi binadamu. Wanafiki wenye sura mbili. Wanafiki wenye kusema haya, kesho tukaongea yale.

Hebu kifikirie Chama cha Wananchi (CUF), Nani angegusa moto wao kwa miaka 10 ya kuanzia 1995 hadi 2005?

Wangesema chochote na kingefanyika kwa sababu wanachama, mashabiki na wafuasi wao walikua wakiwasikiliza na kuvutiwa nao.

Nyuma ya ushawishi wa CUF walikuepo majabali mawili ya kisiasa. Prof Ibrahim Lipumba mchumi mwenye rekodi isiyogusika akitikisa upande wa Bara na Maalim Seif Shariff, Gwiji lisilo na mfano kwa miaka yote Zanzibar.

Yaite maandamano ngoma ingeitika, leta mkutano wa hadhara siyo Pemba wala Mtwara nyomi lingeshona. Usijifanye umesahau maandamano ya Januari 2001 kule visiwani.

Yote hayo yalitokana na ushirika wa Maalim na Lipumba. Uswahiba na urafiki wao haukua na mfanano wao.

Hakuna ambaye angeamini kwamba itafikia kipindi CUF ife au ianguke kwa sababu ya kuvunjika kwa urafiki wa wawili hawa.

Leo hii hawapo pamoja, CUF hii ya sasa siyo ile ya mwanzo na hata wenyewe wanajua hawana nguvu ile waliyonayo mwanzo. Maalim anatesa na ACT yake. Lipumba anajikongonya na CUF. Usimuamini binadamu.

Edward Lowasa bwana! Nani atasimama leo aizungumzie siasa yake kwa mtazamo 'negative'. Hili ni jabali la kisiasa nchini. Laigwanani ambaye hakuwahi kuficha msimamo wa ndoto zake za kuwa Rais.

Alijaribu kwa muda mrefu lakini 2015 ndiyo haswa nguvu yake ilikua kubwa. Kabla ya hapo alishachafuliwa sana na kashfa nyingi mbaya za kifisadi. Wala sihitaji kuzirudia. Wote mnazikumbuka.

Muda ulipofika akachukua fomu ya kugombea kupitia CCM yake iliyomlea toka ujana wake. Mchakato ukaenda. Lowasa akawaambia wafuasi wake "Tulieni hakuna wa kunikata".

Ngoma ikaenda tano bora, jina la Lowasa halipo, Simba akaona msinizingue, akaamua kubwaga manyanga. Chadema waliozunguka Nchi nzima kuitangazia Dunia kwamba Lowasa ni fisadi wakamwambia 'Dingi' karibuni Ufipani.

Edo akaona isiwe tabu akajifanya amesahau kashfa zote alizomwagiwa na Chadema. Akavua gamba akavaa gwanda. Mzee akawa Kamanda, akahubiri mabadiliko.

CCM alipotoka wakamchafua tena, stori nyingi zikasambazwa kuhusu afya yake na wala hafai kuwa Rais.

Baada ya Dk Magufuli kuwa Rais na Lowasa kukosa akarejea CCM akisema anarudi 'home' kule kule kwa waliohubiri kuhusu afya yake wakati wa kampeni. Siasa isikufanye umuamini mtu.

Hebu yatazame mapenzi. Angalia anachopitia Rapa Mabeste hivi sasa na aliyekua Mke wake Mrembo Lisa.

hivi karibuni Mabeste katika Kituo cha Polisi baada ya Lisa kwenda kumshtaki kuwa anamchafua na kumdhalilisha kupitia wimbo wake wa Back Off.

Sikudhani kama ipo siku Mabeste na Lisa wataachana. Safari yao imekua fupi sana. Labda ni unafiki, kujisahau au ndo mapenzi yameisha. Nani anajua zaidi yao wawili?

Tukumbushane tu: Miaka mitano nyuma afya ya Lisa haikua nzuri. Alikua mgonjwa. Mabeste akaacha kila kitu ili amhudumie mke wake.

Akatembea kwenye Vyombo vya Habari na mitandaoni kuomba msaada ili mke wake aweze kutibiwa na kupona. Muziki wa Mabeste ulidorora kwa sababu ya kuwa bize kumhudumia Lisa.

Sasa hawapo wote tena. Mabeste anasema Lisa amechukuliwa na mshikaji wake tena wamezaa wote. Lisa anasema familia ya Mabeste haikumtaka.

Ile I love you, I love you too haipo siku hizi. Vurugu zimekua nyingi hadi wanafikishana Polisi. Unafiki wa maisha yetu unatufanya tuyasahau mazuri tuliyofanya jana.

Mtu asikudanganye kwamba hawezi kuishi bila wewe kwenye mapenzi. Ni sawa na mwanasiasa kukwambia hawezi kuhamia chama kingine. Wala usimuamini mchezaji mpira atakaekuambia hawezi kuhama Timu yenu. Ni uongo na unafiki.

Linapokuja suala la maslahi binafsi, madaraka au pesa usijaribu kumuamini binadamu yoyote. Kila mmoja analo hitaji la moyo wake. Ukimuamini ukubali kuadhirika kesho.

Leo mtu atasimama jukwaani kusifia Sera za CCM kesho akikosa nafasi anayoitaka akihamia Chadema ataeleza mabaya yote ya CCM.

Katani Katani aliyekua Mbunge wa Tandahimba Mtwara kupitia chama cha CUF aliwahi kulia bungeni na kuilaumu serikali ya CCM kushindwa kuwahudumia wananchi vizuri kwenye ishu ya Korosho.

Mwaka mmoja mbele akayafuta machozi yake na kutangaza kuhamia CCM ile ile ambayo aliitolea maneno mengi machafu. Unapata wapi ujasiri wa kumuamini mwanasiasa.

Nani angedhani ipo siku Diamond na Zari wangetemana? Watoto wawili Mungu aliwajalia. Mapenzi yalikua moto moto. Diamond akasema wala hawazi 'kumcheat' Bi Zari.

Haikupita kitambo zikavuja za Diamond kuzaa na kimwana Hamisa Mobetto. Yale mahaba ya Rais wa Wasafi na Bosslady wa Kusini kwa Madiba yakayeyuka.

Umesahau Harmonize alichora tattoo ya Diamond kwenye mwili wake? Alifanya hivyo kwa mapenzi na heshima yake kwa Diamond ambaye alikiinua kipaji chake na kumsogeza Mjini.

Harmonize akahubiri kuwa Wasafi ni sehemu ya maisha yake. Hawezi kuondoka, hawezi kupaacha. Kwenye Bio yake ya Instagram akaandika 'Wasafi for Life'.

Tunavyozungumza sasa hayupo tena Wasafi, tena hakuondoka kwa amani na kupata baraka zote. Hawako sawa na Diamond tena. Watu wawili ambao miaka mitatu nyuma walikua Baba na Mwana leo hii ni maadui wa biashara. Sitaki kukumbuka ndoa ya Dogo Janja na Irene Uwoya.Ama kweli ukistaajabu ya wasanii utakutana na ya wanasiasa.
Rapa Mabeste akiwa na aliyekua Mke wake aitwaye  Lisa.


0683 015145.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2