Na Mwandishi wetu
CHUO Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Dar es salaam, kimesema tangu vyuo kufunguliwa hali ni shwari na kwamba wanaendelea kukabiliana na janga la ugonjwa wa Corona kwa kuhakikisha wanafunzi wanazingatia maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali katika kujikinga na maambukizi, sambamba na kuendelea kufundisha masomo ya muhula wa pili wa masomo kwa mwaka 2019/20 masomo ambayo yalianza tangu tarehe 01 Juni 2020.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kampasi ya Dar es Salaam, Prof. Honest Ngowi, wakati akieleza hatua ambazo zimechukuliwa mpaka sasa kuhakikisha kunakuwepo mazingira salama kwa wanafunzi kusoma.
"Tumejipanga vizuri kukabiliana na janga la Corona kwa kuhakikisha tunawalinda wanachuo, watumishi pamoja na wageni wanaokuja chuoni hapa, kwa kuhakikisha kila mmoja anavaa barakoa, kunawa maji tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono, pamoja na kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima kila wanapokuwa katika eneo la chuo” alisisitiza.
Amesema pamoja na hatua hizo, pia chuo kina wataalamu wa afya ambao wako tayari kutoa huduma za awali iwapo mtu atahisiwa kuwa na dalili za maambukizi ya homa ya mapafu, pamoja na kuhakikisha elimu ya kutosha inaendelea kutolewa kwa wanafunzi na wahadhiri ili kuendelea kuchukua tahadhari.
Maboresho mengine yaliyofanyika ni pamoja na kubadilisha mfumo wa ukaaji darasani unaozingatia umbali kutoka mwanafunzi mmoja hadi mwingine, kubadilisha mfumo wa kukusanya mahududhurio pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa mienendo ya wanachuo wanapokuwa eneo la chuo.
Kufunguliwa kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe kunafuatia maagizo ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kutangaza kuvifungua vyuo vyote nchini kuanzia Juni Mosi mwaka 2020.
Baadhi ya wanachuo wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam wakinawa kwa maji tiririka na sabuni mara baada ya kuwasili chuoni hapo.
Afisa Udahiri, Edward Shana akiwa katika zoezi la usajili wanachuo wanaoingia kuendelea na awamu ya pili ya masomo huku tahadhari kubwa ikiwa imechukuliwa dhidi ya Corona.
Wanachuo wakiwa darasani kuendelea na masomo kwa kuzingatia tahadhari zote zilizotolewa za kujikinga na kuenea kwa Virusi vya Corona.
Wanafunzi wakiwa wamevaa barakoa darasani, wakati masomo yakiendelea.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment