Na Mwandishi Wetu
KUNDI la waimbaji wa Qaswida la Fanny Crew linatarajia kuimba kwenye mkutano mkubwa wa viongozi wa dini mbalimbali utakaofanyika Julai 30 kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi, kiongozi wa Fanny Crew, Naslim Haroun 'Naslim Tz' alisema katika tamasha hilo ataimba Qaswida yake inayokwenda kwa jina la 'Amani'.
Naslim alisema katika tamasha hilo ambalo litashikirisha viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ambako lina mlengo wa kutoa elimu kuhusu suala la amani kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
"Nimepata mwaliko wa kuimba qaswida yangu ya Amani kwenye Mkutano mkubwa wa viongozi wa dini mbalimbali, mkutano huo una malengo ya kuzungumzia amani kuelekea uchaguzi mkuu, najifua vilivyo kwa ajili ya kuonesha umahiri wangu," alisema Naslim.
Aidha Naslim alitumia fursa hiyo kuweka bayana kwamba pamoja na kualikwa kwenye tamasha hilo, ameandaa tamasha la Qaswida linalotarajia kushirikisha waimbaji wengi wa Tanzania bara na Zanzibar litakalofanyika Idd Mosi kwenye ukumbi wa City Mall, Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Naslim alisema katika tamasha hilo utafanyika uzinduzi wa Filamu ya Kiislam na mafundisho yake inayokwenda kwa jina la 'Siku ya Raha'.
Naslim alisema viingilio katika tamasha hilo kwa viti vya kawaida ni shilingi 7000 huku VIP ni shilingi 15000.
Wageni rasmi katika tamasha hilo ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Wanawake, Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Aisha Sululu, Sheikh Anuary Jongo na mama mzazi wa mwanamuziki, Nasib Abdul 'Diamond Platnumz'.
Naslim alisema katika tamasha hilo kutakuwa na michezo mbalimbali ya watoto sambamba na wachekeshaji mbalimbali watasindikiza tamasha hilo.
Wadhamini wa tamasha hilo ni Kanzu Empire, Women Destination, Menee Styles, Nofel Wedding Dress na Nofel Saloon.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment