WANAFUNZI WA SEKONDARI YA WASICHANA NGANZA WAIBUKA WASHINDI WA TUZO YA YST | Tarimo Blog

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari ya wasichana Nganza iliyopo jijini Mwanza, Glory Kirochi na Martha Machumu wameibuka washindi wa  tuzo ya wanasayansi chipukizi inayotolewa na Taasisi ya Young scientists Tanzania(YST) .

Washindi hao Glory na Martha wamechukua tuzo  hiyo baada ya kubuni mradi wa namna ya kuzalisha chakula cha mifugo katika kipindi cha ukame (hydroponic fodder).

Kwa hatua hiyo washindi wamepata kikombe, ngao, medali na fedha taslimu Sh 1,350,000, pamoja na kupata  zawadi hizo wamepata ufadhili wa masomo yao ya elimu ya chuo kikuu kwa kulipiwa gharama zote na Taasisi ya Karimjee Jivanjee.

Nafasi ya pili imechukuliwa na wanafunzi kutoka mkoani Arusha katika  Shule ya Kisimili  ambao ni Albert Mhagama na Stella Kasalla ambao walipata kikombe, ngao, medali na Sh 900,000.

Tuzo ya kumbukumbu ya Hatim Karimjee  ilichukuliwa na Rugambwa Sekondari iliyopo mkoani Kagera ambapo wanafunzi Ivony Rio na Dorris Kilonzo waliokuwa na mradi wa kuboresha usalama wa ndani ya gari ambapo wamepata Shilingi milioni moja, ngao na medali.    

Aidha, Lameck Obeid na Dennis Ndahaje wa Shule ya Sekondari ya Katubuka iliyopo Kigoma walipata ufadhili wa masomo baada ya kuja na mradi wao waliouita ‘siri kwa nini wanafunzi wanaotoka familia duni wanashindwa kufikia malengo ya elimu’.

Akizungumza katika utoaji wa Tuzo hizo uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, Mwanzilishi mwenza wa YST, Dk Gozberth Kamugisha amesema kwa mwaka huu wamekutana na changamoto ya ugonjwa wa Covid 19 uliosababisha kuharibu mawasiliano na maonesho ya sayansi.

“Hii ilitufanya tubadilishe mifumo yetu na kutumia njia za kidigitali kuwafikia wanafunzi na majiji kukagua kazi hizo na kufanya maamuzi kupitia mtandao,” amesema Kamugisha na kuongeza kuwa maonesho hayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuongeza chachu kwa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

Amesema  wakiwa wanasherekea kufikisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, wana mengi ya kujivunia kwa kuzifikia shule nyingi zaidi na kuleta mabadiliko makubwa katika Nyanja ya sayansi na teknolojia.

Amesema kupitia maonesho hayo ya sayansi kwa wanafunzi, wamekuwa wakibuni miradi mbalimbali ya kisayansi ambayo inaweza kutoa suluhu kwa jamii kulingana na dhana halisi ya maisha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee ambao ndio wadhamini wakuu, wa maonesho hayo Yusufu Karimjee amesema mpaka mwaka jana jumla ya wanafunzi 29 waliofanya vizuri katika YST wanafadhiliwa masomo yao ya elimu ya juu.

“KJF tunaamini katika kuwawezesha vijana kupata elimu ndio maana tunawasaidia wanasayansi kuonesha vipaji na ubunifu walionao ili kuleta maendeleo Tanzania,” amesema Yusufu.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Nganza iliyopo jijini Mwanza, Glory Kirochi na Martha Machumu wakiwa meshikilia kikombe walicho kabidhiwa baada ya kuibuka washindi wa  tuzo ya wanasayansi chipukizi inayotolewa na Taasisi ya Young scientists Tanzania(YST) jana  jijini Dar es Salaam.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2